Tafuta

2020.11.29Papa katika maadhimisho ya Ekaristi na Makardinali wapya 2020.11.29Papa katika maadhimisho ya Ekaristi na Makardinali wapya 

Papa Francisko:Ukaribu na kukesha katika kungojea Bwana

Papa Francisko ameadhimisha Misa Takatifu na Makardinali wapya katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican.Katika masomo ya Dominika ya kwanza ya Majilio,yanaonesha ukaribu wa Bwana na kualika kukesha.Wakati wa kusubiri Bwana ni kwa njia ya sala na matendo ya upendo ili tusilale lepe la usingizi wa ubaya na kutokujali wengine.Kanisa linaloabudu Mungu na kuhudumia jirani haliishi katika usiku.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Dominika tarehe 29 Novemba 2020, katika mahubiri ya Papa Francisko, katika Dominika ya kwanza ya Majilio, ambapo akiwa amezungukwa na makardinali wapya waliosimika Jumamosi na yeye kwa kuongozwa na Injili amesema “Masomo ya leo yanashauri maneno mawili msingi kwa ajili ya kipindi cha Majilio. Ukaribu na kukesha. Ukaribu wa Mungu na kukesha kwetu unaonesha wakati Nabii Isaya anasema kuwa Mungu yuko karibu nasi, Yesu katika Injili anashauri kusubiri na kukesha naye. Papa Francisko amefafanua ukaribu kwamba Isaya anaanza kutumia neno la ‘Wewe’ kwani anasema “Wewe Bwana ndiwe Baba yetu (63,16) na anaendelea  kusema maana tangu  zamani watu hawakusikia wala kufahamu kwa masikio wala jicho halikuona Mungu ila wewe  atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye” Maneno hayo yanakumbusha maneno kutoka Kumbu kumbu la Torati yasemayo “ni nani kama Bwana, Mungu wetu ambaye yuko karibu nasi kila mara tunapomwomba? (Kumb 4,7).

Majilio ni kupindi cha kumbu kumbu ya ukaribu wa Mungu

Papa amesema Majilio ni kipindi cha kufanya kumbu kumbu ya ukaribu wa Mungu ambaye alishuka kwetu. Lakini nabii anakwenda zaidi ya hayo na kuomba Mungu akaribie tena: “ laiti ungepasua mbingu na kushuka ili milima itelemke mbele zako (Is 63,19)”. Vile vile hata katika zaburi iliyosomwa yapo maombi “ Ee Mungu tunakusii uje kutuokoa” na mara nyingi ndiyo sala ya mwanzo wa mwaka. Ni hatua ya imani ya kuweza kusema kwamba Bwana tuna haja naye  na ukaribu wake. Ni ujumbe wa kwanza wa Majilio na Mwaka wa kiliturujia ili kutambua Mungu aliye karibu na kumwambia kwa mara nyingine akaribie tena. Yeye anataka kuja kwetu lakini anapendekeza na hashurutishi. Ni juu yetu kutochoka kumwambia “Uje”. Majilio yanatukumbusha kuwa Yesu alikuja kati yetu na atakuja tena mwisho wa nyakati. Papa Francisko akiendelea ametoa maswali na kusema, lakini tujiulize inasaidia nini ikiwa haji leo hii katika maisha yetu? Tumwalike. Sala iwe ya kwetu ile ya kawaida ya Majilio” Uje Bwana Yesu (Ufu 22,20). Tunaweza kumwambia mwanzoni mwa kila siku na kurudia mara nyingi katika kila mikutano, masomo, kazi na maamuzi ya kuchukua katika wakati muhimu na wakati wa majaribu kwa kumwelezea “Njoo Bwana Yesu”.

Injili inapendekeza kukesha

Kwa kumwomba hivyo ni kufanya mazozoezi ya kukesha Papa Francisko amesisitiza. Injili ya Marko leo hii inapendekeza katika sehemu ya mwisho hotuba ya Yesu ambayo ina neno moja msingi ambalo ni ‘Kesheni’. Bwana anarudia mara nne katika aya tano (Mk 13,33-35.37). Ni muhimu kukesha kwa sababu kosa moja katika maisha ni kupotelea katika elfu ya mambo mengi  bila kukumbuka Mungu. Mtakatifu Agostino alikuwa anasema «Timeo Iesum transeuntem» (Sermones, 88,14,13) Ninaogopa kwamba Yesu anaweza kupita bila kumtambua”. Kwa maana hiyo katika kupendelea mafao yetu na kujisahau kwenye ubatiri, tunajihatirisha kupoteza kilicho muhimu. Leo hii Bwana anarudia kusema kwa wote ‘Kesheni ‘ (Mk 13,37). Lakini ikiwa tunapaswa kukesha ina maana tupo katika usiku. Ndiyo sasa hatuishi katika siku, lakini katika usiku wa kusubiri, kati ya giza na ugumu, na alfajiri itawadia tukiwa na Bwana. Itawadia tusife moyo. Usiku utapita na Bwana atatokeza, atatuhukumu Yeye ambaye alikufa msalabani kwa ajili yetu. Tukeshe na kusubiri na tusiishie katika mahangaikio na kukata tamaa. Bali kuishi na matumaini.

Tunasubiriwa kwa upendo na mtu kama ilivyokuwa wakati wa kuzaliwa kwetu

Kama ilivyo kwa kawaida kabla ya kuzaliwa kwetu tulisubiriwa na yule aliyekuwa anatupenda, na sasa tunasubiriwa kwa upendo na mtu. Na ikiwa tunasubiriwa mbinguni ni kwa nini tuishi hapa  duniani kwa majivuno? Kwa nini kuangaikia kidogo na fedha, umaarufu, mafanikio na mambo yote ambayo yanapita? Kwanini kupotea kwenye  kulalamika usiku wakati tunasubiri mwanga wa asubuhi? Papa Francisko amesema, kukesha wakati mwingine ni kugumu. Kwa kawaida usiku ni wa kulala. Hawakuweza  hata wafuasi wa Yesu ambao alikuwa amewambia wakeshe naye jioni, usiku wa manane, hadi kufikia wakati wa kuwika kwa jogoo asubuhi.  Katika masaa hayo kwa dhati hawakukesha. Usiku wakati wa karamu ya mwisho walimkana Yesu, kabla ya jogoo kuwika na asubuhi walimwacha ahukumiwe kifo. Hata kwetu sisi lepe la usingizi linashuka. Kuna usingizi wa hatari usingizi wa kutokuwa wema. Yesu anakuja tunaposahau upendo wa kwanza na kwenda mbele, kwa kuangaikia namna ya kuishi kwetu tu. Bila mwamko wa upendo kwa Mungu, bila subira ya matendo  yake, na kugeuka wasio wema, vuguvuga na walimwengu. Hayo ndiyo yanaharibu imani, kwani imani ni kinyume na kutokuwa na wema.

Sala ni kuwasha mwanga katika usiku na kuamsha walio na uvuguvugu

Shauku ya moto wa Mungu na ambayo inaendelea kufanya uongofu ni ujasiri wa kupenda, ni kwenda mbele, imani siyo kuwa maji yanayozima;  ni moto unaounguza; siyo dawa ya kutuliza ni historia ya upendo kwa yule anayependa. Kwa maana hiyo Yesu anachukizwa na uvuguvugu(Uf 3,16). Je ni kwa jinsi  gani ya kuweza kuondokana na ukosefu wa wema huo? Kwa njia ya kukesha katika maombi.  Sala ni kuwasha mwanga katika usiku. Sala inaamsha walio na uvuguvugu wa maisha yaliyolala na kutoa mwamko wa kutazama juu, na kuweka maelewano na Bwana. Sala inaruhusu Mungu kukaa karibu nasi, inatukomboa dhidi ya upweke  na kutoa matumaini.  Sala inaleta hewa nzuri ya maisha. Ni kama ambavyo siyo rahisi kuishi bila kupumua na ndivyo hivyo mkristo bila sala. Kuna haja ya wakristo waamke ambao wamelala, wanaoabudu, wanaoomba na  ambao usiku na mchana wanampeleka Mbele Yesu aliye mwanga wa ulimwengu katika giza la historia.

Usingizi wa kutokujali wengine na kulalamikia kila kitu

Papa Francisko aidha amesema kuna usingizi wa pili ambao ni usingizi wa kutokujali. Hasiyejali anaona kila kitu ni sawa, iwe siku wala mchana hajali yoyote aliye karibu, ni kujijali  sisi wenyewe na mahitaji yetu, na kutojali wengine,  hapo ndipo usiku unatelemka moyoni. Na mapema ni kuanza kulalamikia kila kitu, na kuhisi kuwa mwathirika wa wote na hatimaye ni mapambano kwa kila kitu.  Giza hili leo hii utafikiri limewashukia wengi kwa kujitangaza wenyewe na kutojali wengine. Je ni namna gani ya kuondokana  na kutojali huko? Papa Francisko amesisitiza ni kwa njia ya kukesha kwa upendo. Upendo ni moyo unaodunda wa kikristo. Kama jinsi ambavyo hatuwezi kuishi bila mapigo ya moyo, ndivyo hivyo mkristo hawezi kuishi bila kuwa na upendo.

Kusaidia na kuhudumia ndiyo ushindi mbele ya Mungu siku ya mwisho

Kuna wengine ambao wanafikiria kuwa na upendo mkuu wa kusaidia na kuhudumia ni kama kupoteza! Kiukweli  ndiyo moja ya ushindi, kwa babu tayari unaelekeza wakati ujao, yaani siku ya Bwana  ambapo kila kitu kitapita na kubaki upendo. Ni kwa njia ya matendo ya huruma ambayo yanatufanya kukaribia Bwana. Katika maombi tumeomba Papa amesema “Bwana atujalia kuwa na utashi wa kwenda kukutana na matendo mema kwa Kristo ambaye anakuja. Yesu anakuja na njia ya kwanza kukutana naye ni katika matendo ya upendo wa dhati”.  Kusali na kupenda ndiyo kukesha. Kanisa linapoabudu Mungu na kuhudumia jirani haliishi katika usiku. Hata kama linachoka na kujaribiwa katika safari ya kuelekea kwa Bwana. Kwa kuhitimisha Papa amesema “ Tuombe: Njoo, Bwana Yesu, tunakuhitaji. Njoo karibu nasi. Wewe ndiye nuru: tuamshe kutoka kwenye usingizi, tuamshe kutoka kwenye giza la kutokujali. Njoo, Bwana Yesu, ufanya mioyo yetu iliyovurugwa  ili kukesha na utujalie  tuhisi hamu ya kuomba na hitaji la kupenda.”

29 November 2020, 11:39