Siku ya Chakula Duniani 2020: FAO inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake ili kukabiliana na changamoto ya baa la njaa na utapiamlo duniani. Siku ya Chakula Duniani 2020: FAO inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake ili kukabiliana na changamoto ya baa la njaa na utapiamlo duniani. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya Chakula Duniani 2020

Baba Mtakatifu Francisko anasema, baa la njaa si kwamba ni maafa tu, bali pia ni aibu kubwa kutokana na ugawaji mbaya wa rasilimali za dunia sanjari na ukosefu wa uwekezaji katika sekta ya kilimo. Kuna athari za mabadiliko ya tabianchi na vita. Sehemu nyingine za dunia, watu wanakula na kusaza, kiasi cha kutupa chakula ambacho kingeweza kutumika sehemu nyingine za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 16 Oktoba 2020 inaadhimisha Siku ya Chakula Duniani inayoongozwa na Kauli mbiu: “Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora na Endelevu.” Maadhimisho ya mwaka 2020 yanabeba uzito wa pekee kwa sababu, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, linaadhimisha pia Kumbukumbu ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake. Leo hii kuna watu zaidi ya bilioni 2 ambao wanapekenywa kwa baa la njaa, lishe duni pamoja na utapiamlo wa kutisha. Idadi ya watu duniani inakadiriwa kwamba, itafikia bilioni 10 katika kipindi cha mwaka 2050. Gharama ya kuwapatia watu wenye lishe duni duniani inakadiriwa kuwa ni kiasi cha dola za kimarekani trilioni 3.5. Tangu mwaka 2014, baa la njaa duniani limekuwa likiongezeka maradufu sanjari na ongezeko la watu wenye uzito wa kupindukia. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Mataifa kuhakikisha kwamba, inajikita zaidi na zaidi katika uzalishaji wa mazao mbali mbali ili kukidhi mahitaji ya chakula na lishe bora duniani, kwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Inakadiriwa kwamba, kiasi cha asilimia 14% cha chakula kinachozalishwa kinapotea katika hatua mbali mbali tangu katika uzalishaji hadi kwa mlaji wa mwisho. Kumbe, kuna haja ya kuwajengea uwezo wakulima wadogo wadogo kwa kuwapatia mikopo, elimu ya kilimo bora, pembejeo na uhakika wa soko na bei za mazao yao ili kuharakisha mchakato wa maboresho ya kipato na hali ya maisha ya wananchi wa kawaida! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2020 aliomtumia Bwana Qu Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa FAO, amekazia kuhusu kumbukumbu ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa FAO, madhara ya COVID-19, kashfa ya baa la njaa duniani na umuhimu wa kusitisha biashara ya silaha duniani na kutumia fedha hizi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anaipongeza FAO kwa kuadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake kwa lengo la kupambana na baa la njaa; ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani pamoja na utapiamlo.

Kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ni “Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora na Endelevu.” Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kushirikiana kikamilifu na kuonesha utashi wa kuboresha hali ya upatikanaji wa chakula na lishe bora kwa kulinda na kudumisha mazingira bora zaidi, chachu ya matumaini kwa watu wengi duniani. Katika kipindi cha Miaka 75 ya FAO, imejifunza pamoja na mambo mengine kwamba, haitoshi tu kuzalisha chakula bali na pia kunahitajika mifumo itakayosaidia kupatikana kwa chakula na lishe bora kwa wote. Kinachotakiwa hapa ni kuwa na suluhu zinazopyaisha mchakato wa uzalishaji na ulaji kwa ajili ya mafao ya Jumuia ya binadamu na  Mama Dunia kwa ajili ya kuimarisha mfumo utakaodumu kwa siku nyingi. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha madhara makubwa kwa watu duniani. Kumbe kuna haja ya kuendeleza juhudi ambazo zimefanywa na Mashirika kama: Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuendeleza Kilimo na Chakula, IFAD., pamoja na kukuza kilimo endelevu, kwa kuwawezesha wakulima wadogo wadogo ili waweze kushiriki katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu vijijini na kwenye nchi maskini zaidi duniani.

Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga katika kipindi hiki chenye kinzani nyingi: kwa upande mmoja kuna maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, lakini upande mwingine kuna vipeo vinavyoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Licha ya juhudi kubwa zinazotekelezwa na FAO, lakini katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kuna mamilioni ya watu wanaoendelea kunyanyaswa kutokana na baa la njaa na ukosefu wa usalama wa chakula, hali ambayo imegumishwa zaidi kutokana na kipeo cha gonjwa la Virusi vya Corona, COVID-19. Idadi ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa inatarajiwa kuongezeka maradufu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, baa la njaa si kwamba ni maafa tu, bali pia ni aibu kubwa kutokana na ugawaji mbaya wa rasilimali za dunia sanjari na ukosefu wa uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo. Kuna athari za mabadiliko ya tabianchi, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Sehemu nyingine za dunia, watu wanakula na kusaza, kiasi cha kutupa chakula ambacho kingeweza kutumika sehemu nyingine za dunia.

Watu wanapaswa kuguswa na kutambua kwamba, watu wote wanawajibika. Kunahitaji mikakati na sera makini zitakazosaidia kufyekelea mbali baa la njaa duniani. Kuna haja ya kufanya maamuzi magumu kwa kuondokana na utengenezaji na biashara ya silaha duniani na badala yake, fedha hii isaidie kukuza mchakato wa maendeleo fungamani katika Nchi changa zaidi duniani. Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa ingeweza kuepuka vita na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ughaibuni. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa njia ya video kwa kumtakia Mkurugenzi mkuu wa FAO heri na baraka katika utekelezaji wa majukumu na dhamana hii muhimu sana ya kulima, kulisha wenye njaa pamoja na kulinda maliasili, ili watu wote waweze kuishi kwa heshima, kwa kuheshimiana na kupendana kama ndugu wamoja!

Siku ya Chakula Duniani 2020

 

16 October 2020, 14:58