Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu "Njoo Uone": Mawasiliano Kwa kukutana na Watu Jinsi na Mahali Walipo Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu "Njoo Uone": Mawasiliano Kwa kukutana na Watu Jinsi na Mahali Walipo 

Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni 2021: Kauli Mbiu! Njoo Uone!

Papa Francisko: “Njoo Uone”: Mawasiliano Kwa Kukutana na Watu Jinsi na Mahali Walipo” kama kauli mbiu itakayoongoza maadhimisho ya Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni yatakayoadhimishwa tarehe 13 Mei 2021. Njoo uone ni maneno ya Mtume Filipo ambayo ni kiini cha Injili kinachoonesha ushuhuda wa kikristo kabla hata ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amechagua sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Yohane, Sura 1: 46: “Njoo Uone”: Mawasiliano Kwa Kukutana na Watu Jinsi na Mahali Walipo” kama kauli mbiu itakayoongoza maadhimisho ya Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni yatakayoadhimishwa tarehe 13 Mei 2021 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni. Njoo uone ni maneno ya Mtume Filipo ambayo ni kiini cha Injili kinachoonesha ushuhuda wa kikristo kabla hata ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa maneno. Huu ni ushuhuda unaodhihirisha mchakato wa watu kuangaliana machoni, shuhuda mbalimbali, uzoefu na mang’amuzi; kukutana pamoja na kukazia ujirani mwema.

Mwinjili Yohane katika Sura ya 1:43-46 yanamwonesha Kristo Yesu aliyekuwa anataka kuondoka kwenda Galilaya, akamwona Filipo na kumpatia mwaliko wa kumfuasa. Naye Filipo alipokutana na Nathanaeli, akamwambia kwamba, wamemwona Masiha ambaye habari zake zimeandikwa na Musa kwenye Torati, lakini Nathanaeli akamwambia, laweza neno jema kutoka Nazareti? Ndipo alipomwambia “Njoo uone”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwanadamu anakabiliwa na mabadiliko makubwa kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, lakini maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, yanaweza kuwasaidia watu wa Mungu kujenga na kudumisha ujirani mwema kwa kutambua kile ambacho ni muhimu pamoja na kuwa na uelewa makini wa maana ya vitu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, si rahisi sana kuutambua ukweli bila ya kuwa na uzoefu, mang’amuzi pamoja na kukutana na watu! Si rahisi sana, ikiwa kama watu hawataweza kushiriki katika furaha na mateso ya jirani zao. Wahenga walisema, “Mwenyezi Mungu anakutana na mtu mahali alipo”. Hii inaweza kuwa ni dira na mwongozo kwa wadau katika sekta ya mawasiliano ya jamii wanaotekeleza dhamana na majukumu yao ndani ya Kanisa. Katika wito wa Mitume wa kwanza wa Kristo Yesu, alikwenda na kukutana nao; na hatimaye, akawaalika kumfuasa. Hata wadau wa mawasiliano ya jamii katika ulimwengu mamboleo wanaitwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano ya jamii, ili kuwafikia watu jinsi walivyo na mahali wanapoishi!

Mawasiliano 2021
01 October 2020, 16:01