Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake kuhusu fumbo la sala, Jumatano tarehe 14 Oktoba 2020 amezungumzia kuhusu Sala ya Zaburi. Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake kuhusu fumbo la sala, Jumatano tarehe 14 Oktoba 2020 amezungumzia kuhusu Sala ya Zaburi. 

Papa Francisko: Katekesi Kuhusu Fumbo La Sala: Sala Ya Zaburi!

Kitabu cha Zaburi kinachowafunda waamini jinsi ya kusali kwa kujadiliana na Mwenyezi Mungu. Zaburi ni Sala inayofumbata hisia nzito za mwanadamu zinazogusa: furaha, machungu, shukrani, matumaini pamoja na mashaka yanayosheheni katika maisha ya watu! Zaburi ni kioo cha maajabu ya Mungu katika historia ya watu wake na mazingira ya watu yalivyoonjwa na mtunga Zaburi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 6 Mei 2020 alianza mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Kutokana na kuzuka kwa janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Baba Mtakatifu alikatisha katekesi kuhusu Fumbo la Sala na kuanza kujikita katika katekesi kuhusu “Uponyaji wa Ulimwengu” mintarafu Mwanga angavu wa Injili, Fadhila za Kimungu pamoja na Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Jumatano, tarehe 14 Oktoba 2020, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI  mjini Vatican, Baba Mtakatifu amendelea na katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala mintarafu Sala ya Zaburi. Kuna Zaburi 150 ambazo waamini wanaalikwa kuzisali! Toka wakati wa Mfalme Daudi hadi ujio wa Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi wa ulimwengu, Maandiko Matakatifu yana matini ya sala yanayoonesha sala kwa ajili ya mtu binafsi na sala kwa ajili ya wengine. Zaburi zimekusanywa kidogo kidogo katika mkusanyiko wa Vitabu vitano: Zaburi, (au “Masifu”), kipeo cha kazi ya sala katika Agano la Kale.

Zaburi zilikuwa ni sala ya Taifa la Mungu kama kusanyiko na chimbuko lake ni Nchi Takatifu na Jumuiya ya Diaspora; jumuiya za waamini waliokuwa wametawanyika sehemu mbali mbali za dunia. Zaburi ni sala inayokumbatia kazi ya uumbaji, inakumbusha matukio makuu ya wokovu na inamngojea Masiha atakayezikamilisha kabisa. Zaburi zikisaliwa na kukamilishwa katika Kristo Yesu, zinadumu na ni za msingi kwa sala ya Kanisa lake. Rej. KKK. 2585-2587. Katekesi ya Baba Mtakatifu imeongozwa na Zaburi ya 13: 2-3.6. Maombi ya mwenye matumaini. Hii ni Zaburi ya Daudi isemayo “Hata lini lifanye mashauri nafsini mwangu, nikihuzunika moyoni usiku na mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu? ... Naam nimwimbie Bwana, kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu”. Maandiko Matakatifu yamesheheni aina mbali mbali za sala. Lakini kuna Kitabu cha Sala ya Zaburi, kitabu ambacho kimekuwa ni nguzo na chemchemi ya hekima kwa wachamungu. Hiki ni kitabu kinachowafunda waamini jinsi ya kusali kwa kujadiliana na Mwenyezi Mungu.

Zaburi ni Sala inayofumbata hisia nzito za mwanadamu zinazogusa: furaha, machungu, maombolezo, wasi wasi, shukrani, matumaini pamoja na mashaka yanayosheheni katika maisha ya watu!Zaburi ni kioo cha maajabu ya Mungu katika historia ya watu wake na mazingira ya watu yalivyoonjwa na mtunga Zaburi. Zaburi moja yaweza kuleta tukio lililopita, lakini bado unyofu ule hivi kwamba iweze kusaliwa katika kweli na watu wa hali zote na wa nyakati zote. Rej. KKK. 2588. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Zaburi zinawafunda waamini lugha ya sala. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu amemvuvia Mfalme Daudi moyoni mwake pamoja na watunga Zaburi wengine, ili kuwafundisha watu jinsi ya kumtukuza, kumshukuru, kumwomba na kumkimbilia wakati wa furaha na machungu; jinsi ya kutangaza na maajabu na matendo makuu ya Mungu na Sheria yake. Kwa ufupi kabisa, Zaburi ni Neno la Mungu ambalo binadamu analitumia kwa ajili ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu.

Katika Kitabu cha Sala ya Zaburi, mwamini anakutana na watu halisia wanaoshirikisha mang’amuzi ya maisha yao. Zaburi ni sala na mara nyingi ni sala inayobubujika kutoka katika mang’amuzi ya maisha ya mtu. Ili kuweza kusali vyema, kuna haja kwa waamini kubaki jinsi walivyo, ili kuonja ukuu wa Sala ya Zaburi. Haya ni maisha ya watu wote ambayo yanapambwa pia kwa uwepo wa shida na magumu; mateso, mahangaiko na wasi wasi katika maisha! Mzaburi anachukulia hali na mazingira kama sehemu ya maisha yake ya kawaida, lakini katika Sala ya Zaburi, mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanawasilishwa kama swali ambalo linatolewa katika mahangaiko!

Kati ya maswali endelevu ambayo bado yanaelea kwenye ombwe ni “Hata lini?” Kila mateso na mahangaiko yanapotokea katika maisha ya mwanadamu, ni mwaliko wa ukombozi, kila chozi linalo mwagika, linahitaji faraja; madonda yaliyo wazi, yanahitaji kugangwa na kuponywa; na kila kashfa inahitaji hukumu ya haki. Sala ya Zaburi inawahamasisha waamini kutobaki wakiwa wanalalama katika mateso na mahangaiko, kwani maisha yanapaswa kutakaswa kwanza na hatimaye, kuokolewa. Mwanadamu hapa duniani ni mpita njia tu, lakini Mzaburi anatambua kwamba, ni kito cha thamani kubwa machoni pa Mwenyezi Mungu, ndiyo maana hata kelele zake zina umuhimu wa pekee mbele za Mwenyezi Mungu kwa sababu ndani mwake, kuna Roho Mtakatifu anayewafunulia kwamba, wao kwa hakika wana thamani mbele ya Mungu.

Sala ya Zaburi ni ushuhuda wa kilio cha mwamini kinachofumbatwa katika mifumo mbali mbali ya maisha. Kilio hiki kinaweza kuwa ni ugonjwa, chuki, vita, dhuluma na nyanyaso na hata wakati mwingine, kukata tamaa ya maisha, kiasi cha kugusa kashfa ya hali ya juu kabisa ambayo ni kifo. Katika Sala ya Zaburi, kifo ndiye adui mkubwa sana wa binadamu! Ndiyo maana Mzaburi anamwomba Mwenyezi Mungu kumwokoa na adhabu ya kifo, pale ambapo nguvu za mwanadamu zimefikia ukomo! Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu Francisko, kimsingi sala ni mwanzo na njia ya wokovu. Watu wote wanateseka hapa duniani bila ubaguzi wowote ule. Katika Sala ya Zaburi, mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanakuwa ni kilio kinachohitaji kusikilizwa na kupewa majibu muafaka kwa sababu hiki ni kilio chenye lengo na maana kamili.

Ikumbukwe kwamba, kuna watu wengi ambao wametokwa machozi kutokana na mateso, lakini mateso ya mwanadamu ni matakatifu sana mbele ya Mwenyezi Mungu na kila mtu anafahamika kwa jina. Kila mtu anayo machozi yake binafsi. Katika Sala ya Zaburi, mwamini anapata majibu ya mahangaiko yake kwa sababu malango ya Mungu daima yako wazi, kwa wale wote wanaokimbilia huruma na upendo wake wa daima. Si kila tatizo linaweza kupata suluhu yake kwa njia ya sala na kwamba, mtu anayesali anatambua kwamba, wokovu unatoka kwa Mungu. Mwamini anafahamu fika kwamba, Mwenyezi Mungu daima anasikiliza sala yake, mateso na mahangaiko ya maisha, daima yataendelea kumwandama mwanadamu siku zote za maisha yake. Si rahisi sana kuteseka katika hali ya upweke na hali ya kutelekezwa katika maisha. Sala inamsaidia mwamini katika mateso na mahangaiko yake ya ndani, ili pole pole aweze kutambua mpango wa Mungu katika maisha yake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, “machozi ni sabuni ya roho”. Katika magumu na mahangaiko ya ndani, waamini wasisite kumlilia Mungu.

Ikumbukwe kwamba, hata Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alitokwa machozi, alipokuwa anauombolezea mji wa Yerusalemu. “Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia akisema: “Laiti ungelijua leo hii mambo yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako. Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote. Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa.” Lk. 19: 41- 44. “Baada ya kusema haya Martha alikwenda akamwita Mariamu kando akamwambia, “Mwalimu amefika na anakuita.” Mariamu akaondoka upesi akaenda alipokuwa Yesu. Yesu alikuwa bado hajaingia kijijini. Alikuwa bado yuko pale Martha alipokutana naye. Wale Wayahudi waliokuwa wakimfariji Mariamu walipoona ameondoka haraka, walidhani anakwenda kaburini kuomboleza, kwa hiyo wakamfuata. Mariamu alipomwona Yesu aliinama chini kwa heshima akasema, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.” Yesu alipomwona Mariamu akilia na wale Wayahudi waliokuja naye pia wanalia, alifadhaika sana moyoni; akauliza, “Mmemzika wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo uone.” Yesu akalia. Wale Wayahudi wakasema, “Tazameni jinsi alivyompenda Lazaro!” Lakini wengine wakasema, “Alimponya kipofu, kwa nini hakuweza kuzuia Lazaro asife?” Yn. 11:28-37.

Waamini wakitambua kwamba, Kristo Yesu anateseka na kulia pamoja nao, iwe ni faraja kubwa nyoyoni mwao! Faraja hii iwasaidie waamini kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu kwani Kristo Yesu, daima anawasindikiza na kuambatana nao katika hija yao ya maisha! Kilio cha mwamini kinapaa juu mbinguni kama moshi wa ubani na kumfikia Mwenyezi Mungu anayewafariji waja wake wote. Waamini wakibaki waaminifu mbele ya Mwenyezi Mungu, wataweza kutembea katika mwanga wa utimilifu wa maisha hata katika mateso na mahangaiko ya ndani!

Sala ya Zaburi

 

14 October 2020, 15:26