Papa Francisko, Jumamosi tarehe 17 Oktoba 2020 amekutana na kuzungumza na Kikosi cha Jeshi la Polisi cha "San Pietro" na kufafanua dhamana na utume wa Jeshi la Polisi kwa raia na mali zao. Papa Francisko, Jumamosi tarehe 17 Oktoba 2020 amekutana na kuzungumza na Kikosi cha Jeshi la Polisi cha "San Pietro" na kufafanua dhamana na utume wa Jeshi la Polisi kwa raia na mali zao. 

Papa Francisko: Dhamana na Wajibu wa Jeshi la Polisi

Baba Mtakatifu amewaambia Askari Polisi kwamba, wananchi wana imani nao! Wahakikishe kwamba wako tayari kusaidia kwa kutambua kuwa wao ni watu wenye hekima na busara wanaoongozwa na moyo wa sadaka na uwajibikaji. Papa anawataka Askari Polisi kuragibisha uraia wenye kuwajibika; kwa kulinda na kudumisha haki ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikosi cha Jeshi la Polisi cha “San Pietro” kwa kushirikiana kwa karibu sana na Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini Italia na Vatican katika ujumla wake, vinasaidia sana ili kuhakikisha shughuli mbali mbali zinatekelezwa katika hali ya amani, utulivu na usalama wa raia. Hii ni huduma makini inayotolewa kwa wageni, mahujaji na watalii wanaofika mjini Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Hii ni kazi inayohitaji kwa namna ya pekee kabisa kuheshimu: sheria, taratibu na kanuni zinazotolewa, mambo ambayo yanatekelezwa kwa uvumilivu na kwa kuwaheshimu wageni na mahujaji wanaofika. Vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican vinatekeleza dhamana na wito wake kwa kuzingatia weledi na uwajibikaji makini; kwa kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Vikosi hivi vinawajibika kimaadili na kiutu, kutoa kipaumbele cha pekee kwa watu dhaifu, maskini, wazee na wagonjwa. Yote haya yanawezekana kwa wanajeshi hawa kukita huduma yao katika ustawi na maendeleo ya wengi, daraja makini linalounganisha Jeshi la Polisi na wananchi katika ujumla wao.

Watu wana imani na kutumainia msaada unaotolewa na Askari Polisi wanapokutana nao, ushuhuda unaotolewa kila siku na Askari Polisi. Hata kama wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama hawayaoni na kuyatambua yote haya, lakini Askari Polisi watambue kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu anayaona na kamwe hatayasahau kabisa! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 17 Oktoba 2020 alipokutana na kuzungumza na Kikosi cha Jeshi la Polisi cha “San Pietro”, ili kutoa shukrani zake za dhati kwa kazi kubwa na ushuhuda wanaoendelea kuutoa wanapotekeleza dhamana na wajibu wao wa kila siku. Baba Mtakatifu amewaambia Askari Polisi kwamba, wananchi wana imani nao! Lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, daima wako tayari kusaidia na kwamba, ni watu wenye hekima na busara wanaoongozwa na moyo wa sadaka na uwajibikaji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anawataka Askari Polisi kuragibisha uraia wenye kuwajibika; kwa kulinda na kudumisha haki ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; mambo yanayofumbatwa kwa namna ya pekee katika dhamana ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Katika utekelezaji wa dhama na majukumu yao, Askari Polisi watambue kwamba, kila mtu anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu kwa sababu ameumbwa kwa sura na mfano wake, hivyo anahitaji kuheshimiwa. Baba Mtakatifu amewaombea neema na baraka Askari Polisi ili kwamba, waendelee kuishi na kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa umakini na majitoleo. Anawashukuru kwa sadaka na majitoleo yao katika mchakato wa ulinzi na usalama na kwamba, hana cha kuwalipa, bali Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo awakirimie Mwenyewe kadiri ya mahitaji yao! Imani, mapokeo ya uaminifu na ukarimu, amana, utajiri na urithi mkubwa wa Jeshi la Polisi nchini Italia; viwe ni sababu ya utimilifu wa maisha yao. Kila mtu awe na mang’amuzi chanya kuhusu maisha ya taaluma yake kama mtu binafsi na kama familia.

Baba Mtakatifu amewaombea neema, baraka na mapaji ya Roho Mtakatifu pamoja na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama mwaminifu, “Virgo fidelis” hasa wakati wa uchovu, matatizo na changamoto za maisha, watambue kwamba, Bikira Maria ataweza kuwaombea mbele ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia mahitaji na matamanio yao halali.

Papa: Polisi

 

 

17 October 2020, 15:10