Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis, tarehe 10 Oktoba 2020 anatangazwa kuwa ni Mwenyeheri, mfano bora wa utakatifu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis, tarehe 10 Oktoba 2020 anatangazwa kuwa ni Mwenyeheri, mfano bora wa utakatifu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! 

Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis: Mfano Wa Utakatifu Wa Vijana

Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis,”Teenage Computer Genius” gwiji wa intenet, aliyeanzisha wavuti kwa ajili ya katekesi, mwenye upendo mkuu kwa Ibada ya Ekaristi Takatifu, Bikira Maria na Kanisa katika ujumla wake, anatarajiwa kutangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 10 Oktoba 2020. Itakumbukwa kwamba, alifariki dunia tarehe 12 Oktoba 2006, akiwa na umri wa miaka 15 tu!

Na Padre Gaston George Mkude na Pd. Richard Mjigwa, C.PP.S – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Baba Mtakatifu katika Sura ya tatu ya Wosia huu wa kitume anapenda kuwaambia vijana kwamba, wao ni leo ya Mungu inayofumbatwa katika matamanio halali ya vijana, madonda wanayokumbana nayo katika hija ya maisha yao pamoja tafiti endelevu ni sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya ujana. Baba Mtakatifu anagusia changamoto za ujana zinazoibuliwa katika ulimwengu wa kidigitali, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo pamoja na kuonesha mwanga unaoweza kuwaokoa vijana kutoka katika giza hili la maisha. Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis,”Teenage Computer Genius” gwiji wa intenet, aliyeanzisha wavuti kwa ajili ya katekesi, mwenye upendo mkuu kwa Ibada ya Ekaristi Takatifu, Bikira Maria na Kanisa katika ujumla wake, anatarajiwa kutangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 10 Oktoba 2020.

Itakumbukwa kwamba, alifariki dunia tarehe 12 Oktoba 2006, akiwa na umri wa miaka 15 tu! Lakini hata katika umri huu, ameonesha ukomavu mkubwa wa imani na matumaini, kiasi cha kuwa ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya, wanaoitwa “Millennials”. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kumweka Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika utakatifu wa maisha ya ujana. Mama Kanisa anamwomba, ili aweze kuwa ni msimamizi wa matumizi bora zaidi ya internet. Watakatifu wengine ambao ni wasimamizi wa vijana wa kizazi kipya ni Mtakatifu Domenico Savio na Wenyeheri ni Piergiorgio Frassati na Chiara Badano. Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis, kwa njia ya mitandao ya kijamii, akajipambanua kuwa ni katekista hodari miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kiasi hata cha kuweza kuzama zaidi katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika shida, changamoto na ugonjwa wake, daima aliutolea kuwa kama sadaka safi kwa Kristo Yesu, Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Askofu Domenico Sorrentino wa Jimbo Katoliki la Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino anasema, tukio hili la kumtangaza Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis kuwa Mwenyeheri katika kipindi hiki chenye changamoto kubwa kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni kielelezo cha mwanga wa matumaini. Ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni wa matumizi bora ya njia za mawasiliano ya jamii na hasa mitandao ya kijamii. Hii ni changamoto kwa watu wote wa Mungu kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Padre Gaston George Mkude wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania ameandika Kitabu kuhusu maisha ya Mwenyeheri Carlo Acutis. Utangulizi wa Kitabu umetolewa na Askofu Joseph R. Mlola, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma. Padre Gaston anapenda kutushirikisha kwa uchache yale mambo msingi kuhusiana na maisha ya Mwenyeheri Carlo Acutis.

Amani na Salama! ‘’MILLENNIALS’’, (Nikiri nimekosa neno la Kiswahili ila naomba mniruhusu nilitumie neno hili katika makala hii ya leo, ni neno la lugha ya Kiingereza likimaanisha kizazi cha wale waliozaliwa kati ya mwaka 1981 - 1996 hakika ndio kizazi cha leo na usasa, ni kizazi cha teknolojia, kizazi cha kidigitali tangu kuzaliwa kwao. Na ndio vijana wetu wa leo maana wamezaliwa na wanazaliwa katika mazingira tofauti kabisa na ulimwengu wetu wa zamani za miaka ya 70 na kurudi nyuma. Lugha yao na ulimwengu wao ndio ule wa teknolojia na udigitali. Leo tunakutana na mmoja wa ‘’millennials’’ naye si mwingine bali ni kijana mdogo kabisa aliyejulikana kama ‘’Carlo Acutis’’, ambaye leo ni Mtumishi wa Mungu na tarehe 10 Oktoba 2020atatangazwa kuwa Mwenyeheri katika mji wake wa Assisi nchini Italia.

Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis daima aliongozwa na msemo mmoja; ‘’Tutti nasciamo come degli original, ma molti muiono come fotocopie’’ (We are all born as originals, but many die as photocopies), ni msemo unaotafakarisha na kutukumbusha wajibu wetu wa kubaki wana wa Mungu na kiaminifu siku zote za maisha yetu, kuilinda hadhi ile tuliyoipokea siku ya ubatizo wetu, siku ile tulipozaliwa katika roho kwa kumiminiwa neema kutoka mbinguni.  Carlo Acutis ni mtoto wa kwanza wa wazazi Andrea Acutis na Antonia Salzano, alizaliwa jijini London, nchini Uingereza tarehe 3 Mei, 1991. Wazazi wake waliishi London kikazi lakini Mtumishi wa Mungu Carlos Acutis aliishi utoto wake nchini Italia katika jiji la Milano. Tayari akiwa na miaka 7 mtoto huyu alionesha imani kubwa hivyo kupata ruhusa maalumu kuweza kupokea Komunio ya kwanza. Mtoto Carlo alikuwa na desturi ya kufika parokiani kwake kila siku kwa ajili ya Ibada ya Misa Takatifu na zaidi sana alisali Sala ya Rozari kila siku ya maisha yake. Alikua na kuwa na upendo wa pekee sana kwa Yesu wa Ekaristi na hivyo kumpelekea kila siku kuchukua muda wa kukaa mbele ya Yesu wa Ekaristi na kumwabudu.

Mtoto Carlo alifariki dunia tarehe 12 Oktoba, 2006 na kifo chake kilitokana na ugonjwa wa Saratani ya damu (Leukemia) katika Hospitali ya Mtakatifu Gerardo, katika mji wa Monza, Italia. Mchakato wake wa kutangazwa mtakatifu ulipata kibali tarehe 13 Mei, 2013 kutoka Idara husika na kuanzia mchakato wake katika Jimbo kuu Katoliki la Milano, Italia. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Julai, 2018 alimtangaza kuwa Mtumishi wa Mungu, hatua ya awali kabisa kabla ya kutangazwa kuwa Mwenye Heri na mwishoni Mtakatifu. Tarehe 21 Februari, 2020 Baba Mtakatifu aliridhia mchakato wa kutangazwa kuwa Mwenye Heri. Baada ya Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu kupokea taarifa za muujiza wa uponyaji wa mtoto kutoka nchini Brazil aliyekuwa na shida ya kongosho hapo mwaka 2013.  Mtoto Carlo leo Mama Kanisa anaona fahari juu yake kwani akiwa bado mdogo alionesha ukomavu mkubwa katika imani, imani iliyogusa si tu wazazi wake bali hata rafiki zake na wale wote waliomfahamu.

Katika umri wake mdogo alikuwa na upendo mkubwa kwa Yesu wa Ekaristi na hata baadaye pia alikuwa na ibada kwa Mama yetu Bikira Maria. Mtoto Carlo alijaliwa pia uwezo mkubwa sana na wa kustaajabisha katika teknolojia ya Computer. Wazazi na hata rafiki zake walistaajabia uwezo huo mkubwa na wa kipekee kutokana na umri wake. Alitumia kipaji chake kuinjilisha, hivyo akaanza kuwa katekista sio kwa njia ya kawaida na labda tunayoifahamu wengi, daima alitoa mafunzo ya katekesi kwa njia ya kidigitali yaani kwa kutumia computer na internet. Na hata alikuwa na wavuti aliyoweka humo miujiza yote ya Ekaristi Takatifu. Na ndio leo tunaona mchakato wake umegusa watu wengi ulimwenguni lakini zaidi sana kwa ‘’millennials’’ na hasa kwa jinsi alivyotumia kipaji chake katika computer kwa kueneza imani yake.

Mama yake Antonia anakiri kuwa hakuwa mama wa mfano mintarafu imani ya mwanae, kwani alikuwa ni mkristo wa mazoea tu, ila kupitia mwanae na kwa ushauri wa rafiki yake akaweza kuanza kujifunza upya katekesi ili kuimarika zaidi katika imani. Labda wengi wetu tumepelekwa Kanisani na mama au wazazi wetu ila kwa Mtumishi wa Mungu Carlo hali ni tofauti ni yeye mtoto aliyempeleka mama yake katika imani. Mtumishi wa Mungu Carlo aliwashauri na kuwapeleka katika Misa sio tu mama yake bali hata na ndugu na rafiki zake. Ni mmoja aliyetambua kitu cha thamani kubwa na hivi moyo wake uliwaka mapendo ya kuwashirikisha wengine. Ni changamoto hata nasi kwetu leo juu ya kiu ya kuwashirikisha wengine mambo ya imani yetu, mambo yamuhusuyo Mungu. Hiki ndicho kiini cha uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Mama yake anashuhudia kuwa kabla ya mwanae Carlo kumpeleka Kanisani alishirikia Misa siku ya Komunyo ya Kwanza, Kipaimara na siku ya Ndoa yake ila sasa baada ya kusaidiwa na Mtumishi wa Mungu Carlo naye ameanza kushiriki Adhimisho la Misa Takatifu kila siku na kwa uchaji mkubwa. Kwake Mtumishi wa Mungu Carlo amekuwa kama mkombozi wake mdogo. Lakini pia Mtumishi wa Mungu kama watoto wengine wote wa umri na nyakati zake alikuwa mpenzi wa michezo ya Luninga. Pamoja na kupenda “Video games” alijitahidi na kujipa nidhamu ya kutenga saa moja kwa wiki kufurahia michezo hiyo, na alifanya hivyo kwa makusudi mazima ya kuepuka urahabu wa teknolojia. Tangu mapema anatambua na kuona hatari zinazoweza kutokana na utamaduni wa kidigitali.

Miaka minne baada ya kifo chake mama yake akajifungua watoto mapacha, na mama yake anashuhudia kusema ni muujiza uliotokana na maombezi ya Mtumishi wa Mungu Carlo, na wadogo zake mapacha ambao hawafahamu wamezaliwa siku ile ya kufariki kwake, siku ile alipozaliwa upya mbinguni. Hata wadogo zake hawa nao kwa kufuata mfano mwema wa kaka yao Mtumishi wa Mungu Carlo wanashiriki Adhimisho la Ekaristi Takatifu na kusali Rozari kila siku. Mama yake Antonia anakiri kuwa, Yesu Kristo Mfufuka kwa kupitia Mtumishi wa Mungu Carlo aliwaandaa na kuwaleta karibu na imani yao na hasa maisha ya Kisakramenti na hata kuweza kukipokea kifo cha Carlo, kwani wanajua bila imani lingelikuwa ni jambo zito na gumu, na hasa ukizingatia ni kifo cha mtoto mdogo wa miaka 15. Muujiza wa kwanza kwao ni mara baada ya kufariki kwa mtoto wao Carlo, kwanza siku ya mazishi umati mkubwa wa watu walioshiriki Misa ya maziko yake na pia watu kuona kuwa alikuwa sio mtoto wa kawaida tu bali ni mtoto mtakatifu na hivyo kuanza kusali kupitia maombezi yake.

Mama yake anakiri na kushuhudia kuwa baada ya mtoto wake kupokea Komunyo ya kwanza hakukosa kamwe kushiriki Ibada ya Misa Takatifu hata walipokuwa safarini likizoni daima waliona jinsi ya kumsaidia ili aweze kushiriki Ibada ya Misa Takatifu. Mtumishi wa Mungu Carlo alitambua katika udogo wake kuwa miili yetu inaweza kwenda likizo lakini hakuna likizo ya imani, mahusiano yetu na Mungu ni ya daima na katika hali na mazingira yoyote yale. Utakatifu wake ulijikita katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ni kwa kuunganika na Kristo anayejitoa sadaka kwa ajili yetu hapo tunajaliwa uzima wa milele. Pia alikaa na kusali mbele ya Yesu wa Ekaristi, imani katika uwepo halisi wa Yesu Kristo Mfufuka katika maumbo yale ya mkate na divai. Mtumishi wa Mungu Carlo anatukumbusha nasi leo juu ya kuwa na kiu na njaa ya kumpokea Yesu wa Ekaristi na pia kutenga muda kila siku kukaa mbele yake kuongea naye na kumwabudu.

Akiwa katika kitanda cha umauti pia alionesha imani kubwa kinyume na umri wake. Daima alisema; ‘’Napenda kutolea sadaka maumivu yangu kwa Bwana, kwa ajili ya Papa na Kanisa zima. Nisingependa kukaa toharani, bali ningependa kwenda moja kwa moja mbinguni’’. Maneno haya kutoka kinywani mwa mtoto wa miaka 15 si tu yanatugusa leo bali tunaweza kuona ni kwa jinsi gani alikomaa katika imani na hasa tamaa ya kuunganika na Mungu mara baada ya kifo, ni imani yenye matumaini akionesha wazi kuwa kuna maisha na hasa ya heri zaidi mara baada ya kifo chetu, na ndio kwenda mbinguni.  Kanisa kwa sasa linamchukulia kuwa ni kielelezo kwa vijana wa kileo, kwa ‘’millennials’’, kwa wale wa kizazi cha kidigitali na hasa changamoto za kutumia teknolojia kuishi imani yetu, kutuweka karibu zaidi na Mungu na sio kuwa chanzo cha kutuweka mbali na Mungu. Mtoto Carlo anatumia kipaji chake kumtangaza Mungu, kumleta Mungu na kuinjilisha kwa njia za kisasa. Kanisa linafikiri pia kumtangaza kuwa Mtakatifu Msimamizi wa Internet.

Ulimwengu wa kidigitali leo sio tu ni ule wa ‘’Millennials’’ bali ni wetu sisi sote. Sote tunaishi na kuelea katika ulimwengu huo, na ndio unaoamua maisha ya siku kwa siku si tu katika jamii bali hata katika uwanda wa kiroho. Ulimwengu wa kidigitali sio tu kama njia za mawasiliano bali unaamua hata namna zetu za kufikiri, kutenda na kuishi. Ni utamaduni leo ambapo kuona yaani mawasiliano kwa njia ya kidigitali vimekuwa na nguvu zaidi kuliko ule wa kusikia na kusoma kwa njia tulizozoea.  Tumeshuhudia hata katikati ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, shule ziliendelea kuelimisha wanafunzi kwa njia ya kidigitali, wafanyakazi waliendelea kufanyakazi kutokea majumbani “Smart work” kwani njia hii iliwezesha, na hata Ibada za Misa na nyinginezo waamini waliweza kushiriki kwa njia hii ya kidigitali iwe kwa Luninga au kwa njia ya mitandao ya kijamii.

Pamoja na mazuri mengi tunayoweza kusema juu ya ulimwengu huu wa teknolojia na kidigitali bado tunaona upande hasi na wenye ukakasi. Mahusiano kati ya wanadamu leo yanazidi kupungua na kuzorota na hata kupelekea upweke hasi na maisha ya misongo ya mawazo. Mwanadamu ni zaidi ya tamaduni ya kidigitali na hasa inapofika suala la kimahusiano kati ya mtu na mtu. Na matumizi yaliyopindukia ya mitandao na vifaa vya kimawasiliano leo imepelekea hata urahabu, hivyo mmoja kujikuta kila mara na kila saa ametingwa katika ulimwengu wa mitandao. Leo mmoja kabla ya kulala anashika simu yake na labda hata asubuhi mara baada ya kuamka salamu ya kwanza ni katika simu ya kiganjani, simu leo imekuwa ni ugonjwa kwa wengi, akili na namna na maisha yetu sasa zinatawaliwa na simu na vyombo vya mawasiliano.

Leo tunashuhudia hata unyanyasaji wa kimtandao, kitu kinachopelekea watu kupoteza hata hadhi na utu na heshima zao. Utamaduni wa kidigitali leo unapelekea pia usambazaji wa picha za ngono na hata za aibu kuwa rahisi zaidi na hata tunashuhudia watu wakiishia katika urahabu wa kuangalia picha hizo za ngono na utupu. Leo kuliko kabla watu wanadhalilishwa kwa njia ya mitandao hiyo, kifupi mitandao pia imepelekea kupoteza kwa kiasi kikubwa maisha binafsi na ya siri ya mwanadamu. Hata katika uwanda wa kiuchumi, utamaduni wa kidigitali leo unatawala na kuamua hata juu ya dhamira za watu na juu ya dhana nzima ya demokrasia. Kwa njia ya mitandao leo si tu tunapata habari za kweli na maana bali habari nyingi za uongo na zenye kujeruhi na kuumiza na kuvunja mahusiano ya upendo kati ya watu. Mitandao inatumika hata kwa kueneza chuki na uongo na mifarakano. Ukweli leo unajikuta njia panda kwani ni mara ngapi tunakutana na habari au taarifa mitandaoni na kutuacha katika wakati mgumu ya kuwa na hakika kuwa ni kweli au la, na hata mara nyingine tunaamini ni kweli kuwa ni taarifa na habari za kupikwa tu.

Leo duniani tunashuhudia kitu tunachoweza kukiita kama ‘’digital migration’’ (Uhamiaji wa kidigitali), ndio kusema, kuzama katika ulimwengu wa kidigitali na hivyo kujitenga au kujiweka mbali na familia zetu, tamaduni na hata kweli zetu za kiimani na kidini. Ni kuzama katika upweke wa hali ya juu na mwisho kujikuta unapoteza mguso na ulimwengu halisi. Mama mzazi wa Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis anashuhudia na kusema kuwa kijana wake pamoja na kuwa na kipaji cha hali ya juu ya Computer, hakutumia kipaji chake kwa namna za kujitenga na ulimwengu halisi na Muumba wake, badala yake alitumia kipaji chake kumweka karibu zaidi na Mungu na wenzake. Kama Katekista kwa njia ya kidigitali aliweza kuwafikia watu sio tu wa umri wake bali hata wenye umri mkubwa tena wa kada mbalimbali iwe ni walei na hata makleri kwa njia ya wavuti wake.

Mtumishi wa Mungu Carlo aliona haja na hitaji ya kuwashirikisha wengine imani yake ya uwepo wa Yesu Kristo Mzima katika Sakramenti ya Altare yaani Ekaristi Takatifu. Kwake alikuwa anaongozwa na msemo wake mwingine maarufu;’’L’Eucaristia è la mia autostrada per il cielo’’ yaani ‘’Ekaristi ni njia yangu ya kwenda mbinguni’’, kwa kweli anatumia neno ‘’autostrada’’ kwa maana ya barabara kuu na ya haraka au ‘’High way’’, hivyo ni njia ya haraka kwenda mbinguni kama ilivyokuwa tamaa yake akiwa katika kitanda cha umauti, alionesha hamu yake ya kwenda mbinguni kuunganika na Mungu bila ya kupitia toharani. Baba Mtakatifu Francisko anapenda Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis awe kielelezo kwa ‘’millennials’’ na hasa katika utamaduni wetu wa leo wa kidigitali kwani si tu watu wa kizazi cha leo bali sote tunaelea na kuishi katika ulimwengu huo. Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis anatualika kutafakari msemo wake usemao; ‘’La tristezza è lo sguardo rivolto verso sé stessi, la felicità è lo sguardo rivolto verso Dio’’, yaani, huzuni ni pale unapojikazia macho na kujiangalia wewe mwenyewe, furaha ni pale tunapomkazia macho na kumwangalia Mungu.

Ni maneno yenye kututaka kuachana na ubinafsi na umimi wetu. Kwa kuwa Mtumishi wa Mungu Carlo atatangazwa Mwenye Heri tarehe 10 Oktoba 2020 nimeona nitenge japo dakika chache kuandika simuliza lake na hasa lenye lengo la kuwagusa ‘’Millennials’’ wenye kuishi katika ulimwengu wa utamaduni wa kidigitali, kutambua kama Mtumishi wa Mungu Carlo nasi tunaalikwa kuutakatifuza ulimwengu na kuwa mashahidi wa Injili na imani yetu kwa kutumia vema njia za kileo za kiteknolojia na kidigitali. Ni matarajio ya Papa Francisko kuwa tukio la kutangazwa Mtumishi wa Mungu Carlo kuwa Mwenye Heri litawakutanisha vijana wengi kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu hata kama hawataweza kufika kimwili, bali kwa njia ya mitandao ya kijamii na hasa zaidi kwa njia ya sala.

Carlo Acutis
08 October 2020, 09:51