Mchango wa Vatican katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa. Mchango wa Vatican katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa. 

Mchango Wa Vatican Katika Maadhimisho ya Miaka 75 ya UN

Papa: Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati katika mapambano dhidi Virusi vya Corona, COVID-19. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, chanjo dhidi ya COVID-19 inapatikana kwa ajili ya matumizi ya wote na upendeleo wa pekee, uwe ni kwa maskini kwa kuwa hawana nguvu ya kiuchumi wala rasilimali fedha ya kuweza kukabiliana na janga hili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75, tarehe 15 Septemba 2020 limefungua mkutano wake wa 75 unaongozwa na kauli mbiu “Yale tunayoyataka kwa siku za mbeleni, Umoja wa Mataifa Tunaouhitaji: Kuendelea kuthibitisha Majitoleo Yetu ya Pamoja”. Mkutano huu pia umekuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa hapo tarehe 24 Oktoba 1945 mara tu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ukiwa na nchi wanachama 51. Leo hii, Umoja wa Mataifa una jumla ya nchi wanachama 193. Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Changamoto nyingine ni athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinazohitaji wongofu wa kiekolojia, matumizi bora na rafiki ya nishati katika sekta ya kilimo, viwanda, usafiri na katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mkutano umeadhimishwa kwa njia ya mitandao ya kijamii, kwa kutoa fursa kwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kushirikisha mawazo yao.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75 pamoja na mambo mengine amekazia zaidi kuhusu: Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati katika mapambano dhidi ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 inapatikana kwa ajili ya matumizi ya wote na upendeleo wa pekee, uwe ni kwa maskini zaidi kwa kuwa hawana nguvu ya za kiuchumi wala rasilimali fedha na vifaa tiba vya kuweza kukabiliana na janga hili. Pili ni kuhusu ukosefu wa ajira kutokana na janga la Virusi vya Corona-COVID-19 sanjari na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kiasi cha Jumuiya ya Kimataifa kuanza kutumia akili bandia “Artificial intelligence, AI. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ni jambo muhimu na la kujivunia, ikiwa kama watu watafanya kazi katika mazingira bora zaidi, yenye usalama kwa kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wahalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu wanapaswa kushughulikiwa kisheria, ili kuwajengea watu leo na kesho yenye matumaini.

Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kushughulikia changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa sehemu mbalimbali za dunia, ili kujenga na kudumisha dunia inayosimikwa katika umoja na udugu wa kibinadamu. Kuhusu sera na mikakati ya uchumi, Baba Mtakatifu anasema, mfumo wa uchumi duniani unapaswa kuwa ni fungamani unaongozwa na kanuni auni, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na kuangalia uwezekano kwa Nchi tajiri zaidi duniani kufuta deni la nje kwa nchi maskini duniani. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga ili kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajikita katika sera na mikakati ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa elimu bora kwa watoto na vijana wa kizazi kipya, kwa sababu hii ni sehemu ya haki zao msingi na kwamba, watoto wana haki ya kuwa na wazazi wa pande mbili, yaani: Baba na Mama na wala si vinginevyo! Utu, heshima na haki msingi za wanawake zinapaswa kulindwa na kudumishwa, hasa wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha kumbukumbu ya miaka 25 ya Mkutano wa Nne wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake, (FWCW) uliofanyika Beijing, China mwezi Septemba, 1995. Jumuiya ya Kimataifa haitaweza kuwa na amani na usalama ikiwa kama bado kuna mashindano makubwa ya utengenezaji,ulimbikizaji na biashara haramu ya silaha duniani.

Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amesema, katika kipindi cha Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, nchi wanachama wamekuwa wakiukimbilia kama chemchemi ya matumaini kwa ajili ya amani, usalama, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Umoja wa Mataifa ni mahali ambapo nchi wanachama wamekita matumaini yao katika mapambano dhidi ya umaskini, njaa na magonjwa, tayari kujenga na kudumisha hakijamii. Katika miaka hii yote 75, Vatican imekuwa ni “kisima cha kanuni maadili” ili kukuza moyo wa umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Umoja wa mataifa umekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea: haki msingi za binadamu kwa kudumisha amani na usalama. Lakini, bado kuna haja ya kufanya marekebisho makubwa kwenye Umoja wa Mataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kwa kuziunganisha nchi wanachama, katika majadiliano kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres katika hotuba yake elekezi kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75 amegusia mambo makuu manne ambayo bado yanaendelea kuwa ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu: Vita na kinzani; athari za mabadiliko ya tabianchi; hali ya Mataifa kutoaminiana pamoja athari za ulimwengu wa kidigitali: kwa sasa kuna changamoto ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kiasi kwamba, idadi ya maskini duniani inaendelea kuongezeka maradufu, kiasi cha kutishia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030.

Changamoto zote hizi zinahitaji umoja na mshikamano, ili kuhakikisha kwamba, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanapatikana. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendelea kujielekeza zaidi katika mchakato wa maboresho ya sera za kiuchumi na kijamii, kwa kujenga uchumi fungamani na jamii shirikishi, kwa kuheshimu na kuzingatia haki msingi za binadamu. Katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inapunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa angani. Itengeneze fursa za ajira zinazoheshimu na kuendeleza mazingira nyumba ya wote sanjari na kudhibiti ongezeko la nyuzi joto duniani hadi kufikia nyuzi joto 1.5.C., kama njia ya kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015.

Kuna haja ya kuwa na nisharti rafiki kwa mazingira sanjari na kuhakikisha kwamba sera na mikakati ya ya kiuchumi inalenga kupambana pia na athari za mabadiliko ya nchi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuzingatia miundombinu sanjari na kujikita katika kanuni maadili na utu wema ili kupambana na ukosefu wa haki msingi za kijamii. Kuna haja ya kukuza utandawazi wa umoja na mshikamano; kwa kujenga na kudumisha Jumuiya shirikishi.

UN Miaka 75
01 October 2020, 15:21