Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari: Stella Maris: Kongamano la 25 la Utume wa Bahari kuadhimishwa kuanzia tarehe 29 Sept. hadi tarehe 4 Oktoba 2021. Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari: Stella Maris: Kongamano la 25 la Utume wa Bahari kuadhimishwa kuanzia tarehe 29 Sept. hadi tarehe 4 Oktoba 2021. 

Miaka 100 Utume wa Bahari: Sept. 2021 Kongamano La 25 La Stella Maris

Kongamano la 25 la Utume wa Bahari limesogezwa mbele na kwa sasa litaanza kuadhimishwa mjini Glasgow, Scotland, tarehe 29 Septemba na kuhitimishwa tarehe 4 Oktoba 2021, Siku ambayo Utume wa Bahari ulianzishwa. Huu ni utume ambao umekuwa ni msaada mkubwa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia za katika masuala ya: maisha ya kiroho, kiuchumi na kisaikolojia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 17 Aprili 1922 Papa Pio XI alipoidhinisha Utume wa Bahari, “Apostolatus Maris” lakini unajulikana zaidi kama “Stella Maris”. Huu ni utume ulioanzishwa na waamini walei, ili kutaka kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko hapo tarehe 4 Oktoba 1920, kwa kuonesha na kushuhudia ukaribu wa Kanisa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Leo hii kuna umati mkubwa wa Mapadre wanaowahudumia mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Kuna jeshi kubwa la watu wanaojitolea zaidi kuwadumia mabaharia na wavuvi katika bandari 300 kwa kutembelea meli zisizopungua 70,000 kwa mwaka. Mama Kanisa anawashukuru kwa dhati Mitume hawa wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao.

Wadau wa Utume wa Bahari wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji, kwa kuwafunulia watu sura pendelevu ya Mama Kanisa kwa kuonesha ukaribu wake kwa watu wa Mungu na hivyo kuwahamasisha kujisikia kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Miaka 100 iliyopita, kimekuwa ni kipindi cha ujenzi wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika dini, tamaduni na mataifa mbalimbali. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 4 Oktoba 2020 sanjari na kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari, ametumia fursa hii, kuwatia shime wadau wote wa Utume wa Bahari, kuendelea kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili kwa uwepo wa Kanisa katika bandari na kati pamoja na mabaharia, wavuvi na familia zao.

Hili ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Kongamano la 25 la Utume wa Bahari limesogezwa mbele na kwa sasa litaanza kuadhimishwa mjini Gasgow, Scotland, tarehe 29 Septemba na kuhitimishwa tarehe 4 Oktoba 2021, Siku ambayo Utume wa Bahari ulianzishwa. Huu ni utume ambao umekuwa ni msaada mkubwa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao katika masuala ya: maisha ya kiroho, kiuchumi na kisaikolojia. Ndiyo maana Mama Kanisa anapenda kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Papa Pio XI alitamani sana kuona kwamba, Utume wa Bahari unaendelezwa kwenye Bahari na fukwe mbali mbali za dunia. Roho Mtakatifu na kwa maombezi ya Bikira Maria aendelee kupyaisha utume na huduma hii mintarafu mahitaji ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo.

Jubilei hii imekuwa ni fursa pia ya kubadili nembo ya Utume wa Bahari ambayo imetumika kwa takribani miaka 100, anasema Padre Bruno Ciceri, Mkurugenzi mkuu wa Utume wa Bahari Kimataifa. Mabadiliko haya yanapaswa kuanza kutekelezwa polepole, kwa kuzingatia kwamba, mabadiliko haya yanafanyika wakati ambapo bado Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuathirika kwa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Utume wa Bahari unamwangalia kwa namna ya pekee Bikira Maria, Nyota ya Bahari “Stella Maris” anayewaelekeza watu wa Mungu kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Tangu sasa na kuendelea Utume wa Bahari utakuwa unajulikana kama “Stella Maris”, ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na bila kufanya mkanganyiko wowote ule! Kuzuka kwa janga la Virusi vya Covid-19, kumepelekea mapadre wahudumu wa maisha ya kiroho kutumia zaidi njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii ili kuweza kuwafikia mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao.

Utume wa Bahari
06 October 2020, 14:57