Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini katika Mwezi Oktoba maalum kwa Ibada kwa Bikira Maria, kudumisha Ibada ya Rozari Takatifu ndani ya familia! Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini katika Mwezi Oktoba maalum kwa Ibada kwa Bikira Maria, kudumisha Ibada ya Rozari Takatifu ndani ya familia! 

Papa Francisko Mwezi Oktoba: Rozari Takatifu Sala Ya Familia!

Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima yaani Francis, Yacinta na Lucia aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Waamini wasali Rozari kwenye familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anamwangalia Bikira Maria aliyemwilisha Heri za Mlimani kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake! Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake mwanana, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala, lakini zaidi kwa njia ya tafakari ya Rozari Takatifu. Baba Mtakatifu anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbali mbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu.

Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima yaani Francis, Yacinta na Lucia aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, Jumatano tarehe 30 Septemba 2020 amewakumbusha waamini kwamba, Mwezi Oktoba, umetengwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada ya Rozari Takatifu. Anawaalika waamini kuendelea kuwa waaminifu katika Mapokeo haya kwa kujitahidi kusali Rozari Takatifu, kama mtu binafsi, jumuiya, lakini inapendeza zaidi, ikiwa kama wanafamilia watasali na kutafakari kwa pamoja historia ya kazi ya ukombozi iliyotekelezwa kwa njia ya Kristo Yesu. Kwa njia ya Rozari Takatifu, waamini wanamshirikisha Bikira Maria furaha, machungu na matumaini yao. Baba Mtakatifu anawatakia waamini wote maadhimisho mema na baraka kwa mwezi Oktoba 2020.

Kwa njia ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kila mtu ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mchakato wa kuponya ulimwengu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumtaza Kristo Yesu aliyeanzisha Ufalme wa Mungu kwa ujasiri, kwa tafakuri na kwa njia ya ushuhuda wa maisha, ili kwa pamoja waweze kuujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani ili kukuza na kudumisha haki, furaha, uponyaji na wokovu kwa wale wote wanaoteseka kwa magonjwa na kifo. Ametumia fursa hii, kuwakaribisha Majandokasisi kutoka Marekani waliofika mjini Roma kuanza malezi na majiundo yao ya Kikasi katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Amerika ya Kusini. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awakirimie neema na baraka ili hatimaye, waweze kuwa ni watenda kazi waaminifu wa Injili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu amewatakia heri na faraja wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya. Kila mtu katika hali na nafasi yake, ajitahidi kuwa mkarimu, kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi. Wakubali kupokea kwa imani na matumaini majaribu ya maisha, matatizo na changamoto za maisha, huku wakishirikishana upendo kama sehemu ya ujenzi wa familia ya kweli inayosimikwa katika msingi wa amani na utulivu.

Mwezi wa Rozari 2020
01 October 2020, 14:33