Maadhimisho ya Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiajki Duniani Kwa mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu "Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia" Kuwakaribisha, Kuwalinda na Kuwaendeleza. Maadhimisho ya Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiajki Duniani Kwa mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu "Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia" Kuwakaribisha, Kuwalinda na Kuwaendeleza. 

Ujumbe wa Papa Francisko: Siku ya 106: Wakimbizi Na Wahamiaji 2020

Maadhimisho ya Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia”. Kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha watu wasiokuwa na makazi maalum. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa wakati huu linagumishwa zaidi kutokana na changamoto mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chimbuko la Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni mahangaiko pamoja na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu. Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Tangu wakati huo, Siku hii imekuwa ikiadhimishwa Jumapili baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana. Kunako mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko kutokana na sababu za kichungaji akaamua Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Dunaini iadhimishwe Jumapili ya Pili ya Mwezi Septemba.

Lakini, baada ya kusikiliza maoni, sasa ameridhia maombi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia akaamua kwamba, Siku hii iadhimishwe Jumapili ya mwisho ya Mwezi Septemba na kwa mwaka huu inaadhimishwa tarehe 27 Septemba 2020. Maadhimisho ya Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia”. Kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu Francisko anasema wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa wakati huu linagumishwa zaidi kutokana na changamoto mamboleo yaani: vita na dharura mbali mbali ambazo zimesababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kiasi cha kuzalisha wimbi kubwa la wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi zao wenyewe. Ni watu wanaoteseka kutokana na umaskini na kwamba, nchi nyingi duniani hazina miundombinu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji.

Baba Mtakatifu anasema, hivi karibuni Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu limechapisha Mwongozo Wa Shughuli za Kichungaji kwa Watu Wasiokuwa na Makazi Maalum. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Mwaka 2020 anapenda kujikita zaidi na changamoto ya watu wasiokuwa na makazi maalum; watu ambao wamesahaulika katika agenda za kitaifa na kimataifa. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 lisiifanye Jumuiya ya Kimataifa kusahau mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwaangalia kwa jicho la huruma wale wote walioathirika kutokana na ukosefu wa fursa za ajira, waliotelekezwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na hata wakati mwingine kukataliwa kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Kristo Yesu alilazimika kukimbilia Misri pamoja na wazazi wake na hivyo kuonja hofu na mashaka kuhusu hatima ya maisha yao. Leo hii, kuna mamilioni ya watu wanaohisi na kuonja hali kama hiyo.

Kuna watu wanaokimbia nchi na makazi yao kwa sababu ya baa la njaa, vita, hatari mbali mbali za maisha na hivyo wanatafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kristo Yesu yuko kati pamoja na watu wote hawa kama hata ilivyo kwa wale wote wanaoteseka kwa baa la njaa, kiu, uchi, wagonjwa, wafungwa na wageni. Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanauona Uso wa Kristo Yesu anateseka kati pamoja na watu wote hawa. Waoneshe ujasiri wa kuwaendea ili kukutana nao, kuwapenda na kuwahudumia kwa niaba ya Kristo Yesu. Watu wasiokuwa na makazi maalum ni fursa nyingine tena ya kukutana na Kristo Yesu, tayari kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha katika maisha ya jumuiya inayowapatia ukarimu. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau waliweza kumtambua Kristo Yesu kwa kumega mkate, janga la Virusi vya Corona, COVID-19 liwasaidie waamini kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo watu wasiokuwa na makazi maalum. Jambo la msingi ni kuwa karibu nao, ili kuwahudumia kwa huruma na mapendo kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema.

Na kwa njia hii, wataweza kujenga ujirani mwema. Waamini wajenge utamaduni wa huduma ya upendo kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, wakati wa Karamu ya mwisho, Kristo Yesu alipowaosha Mitume wake miguu. Ili kupatana kuna haja ya kuwasikiliza kwa makini wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Sanaa ya kusikiliza kilikuwa ni kigezo muhimu sana kwa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo na hatimaye, wakaweza kushirikishana amana na utajiri wao, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, kuweza kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Watu wajihusishe kikamilifu ili kuwaendeleza jirani zao kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu na yule mwanamke Msamaria. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19, limeonesha umuhimu wa kushirikiana na kushikamana, ili watu waweze kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na huo ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa ukarimu, udugu wa kibinadamu na mshikamano wa kweli. Kuna haja ya kushirikiana ili kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Hakuna sababu ya kuwa na: kinzani, mipasuko na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko. Hakuna tena muda wa ubinafsi wala ubaguzi. Ili kuweza kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na ushirikiano na mshikamano wa kimataifa na hata kwa watu mahalia bila kumtenga awaye yote. Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2020 yanayoongozwa na kauli mbiu “Kama Kristo Yesu, wanalazimishwa kukimbia”. Kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha watu wasiokuwa na makazi maalum, anapenda kuwakabidhi watu wote wasio kuwa na makazi maalum, chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, Mlinzi mwaminifu wa Familia Takatifu ya Nazareti. Mtakatifu Yosefu awafariji na kuwalinda wale wote wanaotumbukizwa katika vita, umaskini pamoja na kuyakimbia makazi na nchi zao. Mtakatifu Yosefu awaombee nguvu ya kuweza kudumu, awafariji katika mateso na mahangaiko yao, awape ujasiri katika majaribu wanayokumbana nayo. Mtakatifu Yosefu, awaombee wale wasiokuwa na ajira, ili waweze kupata ajira na makazi salama.

wahamiaqji siku 106

 

 

 

24 September 2020, 16:15