Baba Mtakatifu Francisko amewatumia mahujaji wa hija ya 13 ya Familia Kitaifa nchini Italia, hija kwa ajili ya familia ujumbe wa imani, matumaini na mapendo kwa mwaka 2020. Baba Mtakatifu Francisko amewatumia mahujaji wa hija ya 13 ya Familia Kitaifa nchini Italia, hija kwa ajili ya familia ujumbe wa imani, matumaini na mapendo kwa mwaka 2020. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Mahujaji wa Hija ya 13 ya Familia

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini umuhumu wa matukio haya mawili, Kardinali Pietro Parolin kwa niaba yake, amewatumia mahujaji ujumbe wa matashi mema, huku akiwataka watimilike, wafarijike, wanie mamoja na wakae katika amani, kama kielelezo cha kauli mbiu ambayo imeongoza hija hii ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha madhara makubwa katika maisha ya ndoa na familia.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, Jumamosi tarehe 12 Septemba 2020 limeadhimisha hija ya 13 ya Familia Kitaifa, mahususi kwa ajili ya familia kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mtimilike, mfarijike, nieni mamoja na mkae katika amani.” Rej. 2 Kor. 13:11. Hija hii imewashirikisha mahujaji wachache na wengi wao wameshiriki kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Hii ni hija ambayo imeadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei na Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto. Hija hii imekuwa ni muda wa sala, tafakari, shuhuda pamoja na maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Mahujaji wamejikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa ajili ya familia pamoja na watoto wanaoanza tena masomo, Jumatatu tarehe 14 Septemba 2020 baada ya shule kufungwa kama sehemu ya utekelezaji wa itifaki ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-10.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini umuhumu wa matukio haya mawili, Kardinali Pietro Parolin kwa niaba yake, amewatumia mahujaji ujumbe wa matashi mema, huku akiwataka watimilike, wafarijike, wanie mamoa na wakae katika amani, kama kielelezo cha kauli mbiu ambayo imeongoza hija hii ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliojibidiisha kuandaa na hatimaye kutekeleza hija hii kwa ufanisi mkubwa, hasa zaidi katika kipindi hiki, ambacho familia nyingi bado zinaendelea kuonja madhara ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Kumbe, hija hii ni kielelezo cha ushuhuda wa imani na mshikamano unaopania kuwasaidia wanafamilia kujichotea nguvu katika sala sanjari na kujenga udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika matumaini ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mchakato wa wanafunzi kurejea tena shuleni, liwe ni tukio linalowawajibisha watu wote wa Mungu nchini Italia, ili kupyaisha tena dhamana na wajibu wa elimu inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa familia kama kitovu cha malezi na majiundo na wakati huo huo wanafunzi wenyewe wakiwa ni wadau wakuu katika mchakato mzima. Wanafunzi wanapaswa kupata malezi bora yatakayowawezesha kukuwa vyema na salama; kwa kufundwa tunu msingi za jamii, mambo msingi kwa ajili ustawi, maendeleo na mafao ya jamii nzima. Baba Mtakatifu Francisko ameungana na mahujaji wote kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili familia sehemu mbalimbali za dunia ziendelee kuwa ni chemchemi ya uhai, imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu katika ujumla wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume!

Mahujaji Italia
13 September 2020, 08:52