Tafuta

Vatican News
Tarehe 8 Septemba, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa Tarehe 8 Septemba, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa  (Vatican Media)

Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria, 8 Septemba: Nyota Angavu!

Mt. Paulo VI tarehe 8 Septemba 1964 Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria ni nyota angavu inayotangulia Jua la Haki, Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Ni Sikukuu ya kifamilia, ili kuadhimisha zawadi ya uhai inayojikita katika Injili ya uhai. Ni fursa ya kukuza Ibada kwa Bikira Maria Mfariji, changamoto na mwaliko kwa wasichana kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sikukuu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa inaadhimishwa na Kanisa tarehe 8 Septemba ya kila mwaka. Siku kuu hii inapata chimbuko na msingi wake katika Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, kwa kumpatia upendeleo wa pekee Mama yake, Bikira Maria. Sikukuu hii ilianzishwa na Papa Sergio wa kwanza kunako karne VII kadiri ya Mapokeo ya Makanisa ya Mashariki ambayo yanaipatia Sikukuu hii heshima ya hali ya juu kabisa. Kuzaliwa kwa Bikira Maria kuna uhusiano wa pekee kabisa na kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Huu ni utimilifu wa ahadi za Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Sikukuu hii ni sehemu ya maandalizi ya “Tabernakulo” itakayomtunzwa Mwana wa Baba wa milele. Kumbe, kuzaliwa kwa Bikira Maria ni matunda ya kazi ya ukombozi. Ni katika muktadha huu, Bikira Maria anakuwa ni mwanga angavu wa Jua la haki, anayeutangazia ulimwengu furaha ya Mkombozi wa ulimwengu. Mtakatifu Paulo VI tarehe 8 Septemba 1964, alisema, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu hii kwa kuzingatia mambo makuu matatu: Bikira Maria ni nyota angavu inayotangulia Jua la Haki, Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Hii ni Sikukuu ya kifamilia, ili kuadhimisha zawadi ya uhai inayojikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ni fursa ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mfariji, changamoto na mwaliko kwa wasichana kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao. Mtakatifu Paulo VI anasema, Bikira Maria ni kielelezo cha upendeleo wa Mungu unaonafsishwa katika utenzi wa Bikira Maria “Magnificat”. Bikira Maria akakingiwa na kila doa la dhambi ya asili, Mwenyezi Mungu akamkirimia baraka zote za rohoni katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo Yesu. Akachaguliwa ili awe mtakatifu na bila hatia mbele zake katika pendo ili aweze kushiriki kikamilifu katika Fumbo la Umwilisho, tukio muhimu sana katika kazi ya Ukombozi. Kuzaliwa kwa Bikira Maria ni Sikukuu ya kifamilia inayounganisha mwanga wa Ibada, Sala na Imani kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Waamini wanamtolea Mwenyezi Mungu sifa na shukrani kwa kuzaliwa kwa Bikira Maria, Mama wa Kristo Yesu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Waamini wanataka kuungana na Bikira Maria katika maisha na utume wake, huku wakijitahidi kufuata nyayo zake katika Njia ya Msalaba wa Mwanaye Kristo Yesu hadi pale Mlimani Kalvari huku wakisali na kusema: “Salamu Malkia, Mama mwenye huruma, uzima, tulizo na matumaini yetu salam. Tunakusihi hapa ugenini sisi wana wa Eva, tunakulilia tukilalamika na kuhuzunika bondeni kwenye machozi. Haya basi mwombezi wetu, utuangalie kwa macho yako yenye huruma na mwisho wa ugeni huu, utuoneshe Yesu mzao mbarikiwa wa tumbo lako, Ee mpole, Ee mwema, Ee mpendelevu Bikira Maria.” Mtakatifu Paulo wa VI anafafanua kwamba, waamini ni sehemu muhimu sana ya umoja wa Fumbo wa Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kumbe, wanapaswa kuwa na mwono mpana zaidi kuhusu kazi ya Ukombozi na mchakato wa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha; kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu.

Sikukuu hii ipyaishe upendo kwa Bikira Maria na Kanisa; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa utu, heshima na haki msingi za wanawake. Wanawake watambue wajibu na haki zao katika maisha na utume wa Kanisa kwa kusimama kidete katika kanuni maadili na utu wema, kwa kukumbatia na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Sikukuu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria ni fursa ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mfariji, changamoto na mwaliko kwa wasichana, kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao. Mtakatifu Paulo VI anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu, ili Kanisa liweze kuwapata wasichana watakaojitosa kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia maisha ya kuwekwa wakfu, huku wakijitahidi kufuata nyayo za Bikira Maria Mama wa Mungu aliyethubutu kusema "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema” na kwa lugha ya Kilatini inasomeka kama ifuatavyo: “Fiat mihi secundum Verbum tuum”.

Mtakatifu Paulo VI alisema, miito ya kitawa leo hii inahitaji ari, moyo wa sadaka na majitoleo zaidi, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, pengine kuliko hata ilivyokuwa kwa miaka kadhaa iliyopita ambapo, maisha ya kitawa yalionekana kuwa kama “kimbilio la wakosefu”. Kwa kufuata nadhiri ya: Ufukara, Utii na Usafi kamili, watawa waweze kupata ile furaha na amani ya ndani kwa kujisadaka kwa ajili ya Mungu na huduma ya upendo kwa waja wake!

Bikira Maria: Kuzaliwa

 

 

 

07 September 2020, 15:51