Tafuta

Papa Francisko: Msalaba ni Kitabu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Papa Francisko: Msalaba ni Kitabu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! 

Papa Francisko: Msalaba: Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu!

Sikukuu ya Kutuka kwa Msalaba, Papa Francisko anasema, huu ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu unaweza kuonekana kana kwamba ni upuuzi mtupu! Kila mara mwamini anapoutaza Msalaba, anagundua upendo na huruma ya Mungu iliyotundikwa Msalabani. Msalaba ni Kitabu kikuu kinachosimulia huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wa nyakati zote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba iwasaidie waamini kutambua na kuthamini ukuu wa Msalaba, madhara ya dhambi na thamani ya mateso ya Kristo Yesu Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa watu wote. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na kifo. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya kimya kikuu! Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba, anaadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba “Exaltatio Sanctae Crucis” kwa lugha ya Kilatini. Hii ni Sikukuu ambayo inapata chimbuko lake kunako mwaka 335 Mfalme Costantino alipojenga Makanisa makuu mawili na kwa mara ya kwanza akawaonesha watu Masalia ya Msalaba Mtakatifu. Hata hivyo, hii ni Sikukuu yenye ukuu na maana yake kwani inadhihirisha kuwa Msalaba wa Kristo ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu; ni siku ambayo Msalaba wa Kristo unang’ara duniani!

Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii wakati Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutuka kwa Msalaba, anasema kwamba, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu unaweza kuonekana kana kwamba ni upuuzi mtupu! Kila mara mwamini anapoutaza Msalaba, anagundua upendo na huruma ya Mungu iliyotundikwa Msalabani. Msalaba ni Kitabu kikuu kinachosimulia huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wa nyakati zote. Ni katika muktadha wa maadhimisho haya Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi, wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, Jumamosi, tarehe 12 Septemba 2020 kwenye Kituo cha Hija Pugu, ameadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba. Ibada hii ya Misa takatifu ilitanguliwa na Ibada ya Kitubio na kufuatiwa na Njia ya Msalaba.

Askofu mkuu Ruwa'ichi, ametoa mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuuheshimu Msalaba na kuupatia hadhi yake, ili hatimaye, kama waamini waweze kuishi kama viumbe wapya. Kila mtu ajitahidi kuupokea na kuubeba Msalaba wake, kama njia ya kumshuhudia na kumtangaza Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya maisha yaliyotukuka. Kamwe waamini wasiuonee aibu Msalaba wa Kristo Yesu kwa sababu una hadhi, una nguvu na ni chemchemi ya nguvu na usalama wa waamini kwani juu la Msalaba ametundikwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Askofu mkuu Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anazitaka familia kutambua kwamba, Msalaba ni chombo cha wokovu, chimbuko la baraka, kielelezo cha imani, matumaini na mapendo. Msalaba ni chimbuko la maisha mapya. Waamini mbele ya Msalaba waoneshe heshima na kuusujudia kwani juu yake ametundikwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi wa ulimwengu. Katika kipindi hiki cha mchakato wa uchagu mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 28 Oktoba 2020, watanzania, wamtazame Kristo Yesu Mwokozi wa ulimwengu, wamwombe ili Tanzania iweze kusimikwa katika misingi ya haki, amani na usalama kwa raia wote.

Papa Msalaba
14 September 2020, 14:16