Tafuta

Tarehe 5 Septemba, Jumuiya ya Kimataifa Inaadhimisha Siku ya Upendo Kimataifa iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa tarehe 17 Desemba 2012 ili kuenzi mchango wa Mama Theresa wa Calcutta katika huduma ya upendo. Tarehe 5 Septemba, Jumuiya ya Kimataifa Inaadhimisha Siku ya Upendo Kimataifa iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa tarehe 17 Desemba 2012 ili kuenzi mchango wa Mama Theresa wa Calcutta katika huduma ya upendo. 

Siku ya Kimataifa ya Upendo 5 Sept. Mama Theresa wa Calcutta

Umoja wa Mataifa tarehe 17 Desemba 2012 ukatangaza kwamba, tarehe 5 Septemba ya kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Upendo ili kumuenzi Mama Theresa wa Calcutta aliyejisadaka bila ya kujibakiza ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai, huruma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Injili ya Uhai!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii  anamwomba Mama Theresa wa Calcutta, mhudumu wa upendo, kuwaombea waamini na watu wote wenye mapenzi mema, ili kipimo cha matendo yao, kiwe daima ni upendo wa bure unaotolewa kwa watu wote bila ubaguzi wa lugha, tamaduni, jamaa au dini. Mtakatifu Mama Theresa wa Calcuta, lakini jina lake hasa ni “Anjezë Gonxhe Bojaxhiu” alizaliwa tarehe 26 Agosti 1910 huko Skopje, Macedonia ya Kaskazini. Tarehe 5 Septemba 1997 akafariki dunia na kutangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 4 Septemba 2016 na Baba Mtakatifu Francisko. Umoja wa Mataifa tarehe 17 Desemba 2012 ukatangaza kwamba, tarehe 5 Septemba ya kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Upendo ili kumuenzi Mama Theresa wa Calcutta aliyejisadaka bila ya kujibakiza ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai, huruma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu anasema, Mama Theresa wa Calcutta ni Msimamizi wa Caritas Internationalis, ambaye kunako mwaka 1950 alianzisha Shirika la Wamisionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta ambao wanajulikana kama mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini. Mama Theresa wa Calcutta awe ni mfano bora wa kuigwa katika mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa kusambana “Virusi vya upendo na mshikamano” ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 liaamshe ndani ya watu wa Mungu fadhila ya huruma na upendo!

Itakumbukwa kwamba, Mama Theresa wa Calcutta ni kielelezo na shuhuda wa huruma ya upendo wa Mungu unaomwilishwa kwa wagonjwa, maskini na wote wanaosukumwa pembezoni mwa jamii kwani upendo kwa jirani ndicho kipimo ambacho Yesu atakitumia siku ya mwisho kuwahukumu wazima na wafu! Maskini ni kundi lisilopendwa na wengi, kumbe, hili ndilo kundi ambalo Mama Theresa wa Calcutta anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo wao kwao. Huu ni muhtasari wa kitabu ambacho kimeandikwa kwa heshima ya Mama Theresa wa Calcutta “Tuwapende wasiopendeka” na Baba Mtakatifu Francisko kukiandikia dibaji yake! “Amiamo chi non è amato. Testi inediti di Madre Teresa di Calcutta (Editrice Missionaria Italiana) Mama Theresa wa Calcutta anasema Ukoma na Kifua kikuu ni magonjwa ambayo hayawezi kufua dafu kwa upweke hasi unaoweza kumfanya mwanadamu kuchungulia na hata wakati mwingine kuonja kaburi! Upweke ni chanzo cha mipasuko ya kijamii, ukosefu wa amani, vita na majanga yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji ya kitabu hiki anakazia mambo mafuatayo: Sala, upendo, huruma, familia na vijana. Anakumbusha kwamba, Kanisa katika maisha na utume wake linaendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu na kwamba, kuna maskini wanaohitaji kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mama Theresa wa Calcutta anawahamasisha waamini kujichotea nguvu ya huruma na upendo wa Mungu kutoka katika kisima cha: Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuweza kumwilisha sala katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Sala iwawezeshe waamini kukutana na kuzungumzana na Kristo Yesu; kuomba rehema na neema ili kuwa kweli ni watu wanaoweza kuthubutu kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao; kwa kuwaangalia wote kwa jicho la upendo linalopyaisha maisha ya watu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, upendo ni fadhila inayomwezesha mwamini kuwa kweli ni Msamaria mwema kwa jirani yake anayeogelea katika shida na magumu ya maisha: kiroho na kimwili.

Upendo uwawezeshe waamini kuwa ni mashuhuda wa huruma inayoganga na kuponya madonda na majeraha ya maisha ya mwanadamu; ni ushuhuda wa faraja ya Mungu kwa madonda ya binadamu! Yote haya yanawezekana ikiwa kama mwamini amefungamanisha maisha yake na Kristo Yesu, tayari kushuhudia uwepo na ukaribu wa Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Mama Theresa wa Calcutta aliyaandika matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha na utume wake, yakawa ni chachu ya utakatifu wa maisha, kumbe, ni jambo linalowezekana hata kwa waamini wengine kuiga mfano huu bora! Mama Theresa alionesha karama na utajiri wa kimama, akawapokea na kuwahudumia watu wote pasi na ubaguzi. Alikuwa na jicho la pekee hasa kwa vijana waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi baada ya familia zao kusambaratika kutokana na sababu mbali mbali. Bikira Maria ni mfano wa Umama unaoguswa na mahangaiko ya wengine, tayari kuyajibu kwa njia ya huduma makini! Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya faraja ya Mungu kwa familia zao kwa njia ya sala. Familia inahitaji kusimikwa katika upendo, umoja na kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa! Kwa kutekeleza yote haya, familia zinakuwa ni zawadi kubwa inayoweza kutolewa kwa Kanisa!

Mama Theresa wa Calcutta anawataka vijana kwa namna ya pekee kujenga maisha na uwepo wao kwa kumzunguka Kristo Yesu, ufunuo wa Huruma ya Mungu; mwamba thabiti na mwaminifu katika ahadi zake hata kama mwanadamu atakengeuka na kuasi. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kukita maisha yao katika matumaini na kamwe wasithubutu kutoa nafasi kwa wajanja wachache kupoka matumaini yao, bali waendelee kushikamana na kumpenda Mungu; huku wakijenga madaraja yanayowaunganisha watu, kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Vijana wawe na ujasiri wa kupambana na changamoto za maisha, daima wakiwa na malengo ya juu pamoja na kuwashirikisha vijana wenzao fursa na mafanikio ya maisha. Vijana wa kizazi kipya warutubishe maisha yao kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Sala ili kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha.

Mama Theresa wa Calcutta 2020

 

05 September 2020, 15:22