Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa tangu mwaka 2003 ifikapo tarehe 10 Septemba inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Vitendo vya Kujinyonga. Mwaka 2020 kuna ujumbe wa matumaini kutoka kwa Papa Francisko. Jumuiya ya Kimataifa tangu mwaka 2003 ifikapo tarehe 10 Septemba inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Vitendo vya Kujinyonga. Mwaka 2020 kuna ujumbe wa matumaini kutoka kwa Papa Francisko.  (AFP or licensors)

Ujumbe wa Papa Francisko: Siku ya Kuzuia Vitendo vya Kujinyonga!

Kila mwaka ifikapo tarehe 10 Septemba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya kuzuia vitendo vya kujinyonga iliyoanzishwa na UN kunako mwaka 2003. Hii ni siku inayoratibiwa na Shirika la Afya Duniani, WHO, pamoja na Shirikisho la Afya ya Akili Kimataifa, IASP. Maadhimisho ya Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Kufanya Kazi kwa Pamoja ili Kuzuia Kujinyonga”:

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Kimataifa ya Kuzia Vitendo vya Kujinyonga “World Suicide Prevention Day”, (WSPD): inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 10 Septemba, ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2003. Hii ni siku inayoratibiwa na Shirika la Afya Duniani, WHO, pamoja na Shirikisho la Afya ya Akili Kimataifa, IASP. Maadhimisho ya Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Kufanya Kazi kwa Pamoja ili Kuzuia Kujinyonga”: "Working Together to Prevent Suicide.” Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya 800, 000 wamejinyonga na wengine zaidi ya milioni 20 wamejaribu kutaka kujinyonga. Nchi ambazo kwa sasa zinaongoza kwa wananchi wake kujinyonga ni China, Vietnam, Iran, Brazil na Afrika ya Kusini. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema njia kuu zinazotumiwa na watu kujinyonga, kwa wanaume ni kutumia silaha za moto, ambazo ufanisi wake ni asilimia 99%. Wanawake hutumia zaidi sumu. Njia ya pili ni pombe pamoja, dawa na sumu. Njia ya tatu ni kujirusha kutoka juu ya ghorofa, daraja au mwamba. Njia zingine maarufu ni kujinyonga na kujitoboa eneo lenye mrija mkubwa wa damu, Njia ningine zinazotumika kwa kiasi ni kujinyima hewa kwa kujifunga husoni mfuko wa plastiki, kuvuta hewa ya Carbon monoxide, au Nitrogen Dioxide, au Helium nk. Hata hivyo, njia hizo za kujiua hutegemea na mtu, kazi au elimu, jinsia na tamaduni.

Nchi ambazo zina idadi ndogo sana ya wananchi wake wanaojaribu kutaka kujinyonga ni Estonia na Sweden. Jamii inahamasishwa kushikamana kwa dhati ili kuzuia na hatimaye kuokoa maisha ya watu wanaotaka kujinyonga kutokana na sababu mbalimbali katika maisha. Huu ni mwaliko wa kuwasikiliza, kuwajali na kuwasaidia watu ambao wanajikuta wakiwa wanashambuliwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa Sonona. Hii ni shida inayowakumba watu wenye umri mbalimbali na kwamba, tatizo hili linazidi kuongezeka kila kukicha sehemu mbalimbali za dunia. Maboresho ya hali ya maisha ni kati ya mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa kuzuia watu kutumbukia katika utamaduni wa kifo kwa kuamua kujinyonga. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anazungumzia kuhusu changamoto ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Hili ni gonjwa ambalo limeonesha wazi ukosefu wa uhakika na usalama katika sekta ya afya. Matumaini ya watu wengine yametoweka kama “ndoto ya mchana”, watu wengi wanajisikia kuachwa pweke na hivyo nyoyo zao kuelemewa sana na majonzi pamoja na machungu ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia hifadhi, tunza na usalama kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kristo Yesu, mwenyewe anataka waja wake wawe na ujasiri, kwa kufungua nyoyo zao kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kuonja huruma na upendo wake wa daima! Kwa njia hii, wataweza kuonja faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayeendelea kuwatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

Kwa upande wake, Dr.Tedros Adhanom Ghebreyesus Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, anasikitika kusema kwamba, kila kifo ni janga kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki. Tatizo la watu kujinyonga linaweza kuzuilika kwa kuwekeza katika sera na mikakati endelevu ya elimu na afya ya umma. Vijana wengi wako hatarini kujinyonga hasa katika Nchi zile ambazo zina kipato cha juu zaidi. Sababu zinazopelekea watu kujinyonga ni pamoja na: kuteteleka kwa afya ya akili, umaskini na hali ngumu ya maisha, magonjwa ya muda mrefu, upweke hasi, msongo wa mawazo pamoja na kulegalega kwa mahusiano kati ya wapendanao. Kuna hali ya kukata tamaa ya maisha kunakowapelekea watu hata kuona maisha hayana maana na hakuna sababu ya kuendelea kuishi na hatimaye, kupelekea kujinyonga. Kukata tamaa kunaanzia katika mtazamo wa mtu ambao ni kujaza mtazamo hasi katika akili yake katika kila jambo analofanya na kujaza mambo moyoni na kusababisha mtu kuanza kudhoofika kiakili na hatimaye kimwili.

Hakuna kitu kibaya kama kuwa na mtazamo hasi katika maisha yako, hali inayoweza kumsababishia mtu kukata tamaa. Watu wanashauriwa kutoweka mambo makubwa mioyoni mwao na badala yake wayatoe na kuwashirikisha jirani zao ili waweze kuwasaidia kwa ushauri nasaha na tiba muafaka. Kuwa na mtazamo wa kuhisi kutengwa na ndugu, jamaa na marafiki nayo inachangia mtu kukata tamaa na kutotimiza ndoto ya maisha yake. Wakati jukumu la maisha yako ni wewe mwenye na hupaswi kukata tamaa ya maisha. Watu wanapaswa kuishi kadiri ya hali na mazingira yao na kamwe wasitake kujifananisha na watu wengine, kwani watachanganyikiwa na hatimaye kukumbwa na ugonjwa wa Sonona. Dr. Deogratius Kessy katika makala yake kuhusu mada hii, anawashauri watu kuambatana na watu wenye mwelekeo chanya wa maisha. Epuka kuzungukwa na watu wenye mtazamo hasi, watu hawapaswi kukata tamaa kabisa kwani ni dhambi, waendelee kuweka juhudi na maarifa na kupambana hadi ushindi upatikane.

Hali ya mtu kukosa tumaini la maisha inamsababishia kukata tamaa kutokana na kusemwa vibaya, kukosolewa, kukosa upendo, furaha, amani na utulivu wa ndani. Kukosa mahitaji ya msingi katika maisha humpelekea mtu kukata tamaa, matatizo ya kiuchumi, kifamilia, kimapenzi nakadhalika husababisha mtu kukata tamaa ya maisha kutokana na kukosa matumaini katika baadhi ya mambo fulani katika maisha yake. Wimbi la watu mtaani waliokata tamaa ni kubwa sana wengine wanaamua hata kujiingiza katika ulevi, uvutaji sigara, bangi, na utumiaji haramu wa dawa za kulevya na hatimaye wanakuwa ni waathirika wa utumwa mamboleo. Vijana wajitahidi kuwa wabunifu, wenye kuthubutu kufanya maamuzi magumu ya maisha ili kuokoa vipaji na ndoto zao. Mafanikio ya mtu ni sehemu ya mchakato wa maisha na wala hakuna njia ya mkato, kumbe, hakuna sababu msingi ya kujikatia tamaa, kwani kuna nafasi ya kuboresha hali ya maisha hatua kwa hatua.

Kuzuia Kujinyonga 2020
10 September 2020, 14:20