Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema mchango wa mshikamano na Nchi Takatifu ni kielelezo cha matumaini, mshikamano na ujirani mwema. Papa Francisko asema mchango wa mshikamano na Nchi Takatifu ni kielelezo cha matumaini, mshikamano na ujirani mwema. 

Mchango wa Mshikamano na Nchi Takatifu: Matumaini na Ujirani

Papa Francisko: Mchango wa mshikamano kwa ajili ya Nchi Takatifu ni kielelezo cha matumaini, mshikamano na ujirani mwema na watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu. Hapa ni mahali ambapo Neno wa Mungu alitwaa mwili na kukaa kati ya waja wake, akatangaza na kushuhudia uwepo wa ufalme wa Mungu, akateswa, akafa, akazikwa na kufufuka siku ya tatu kadiri ya Biblia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa miaka mingi, watu wa Mungu katika Nchi Takatifu wamekuwa wakifurahia ukarimu kutoka kwa waamini wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa njia ya mchango wa upendo wa mshikamano, waliweza kuendelea na maisha yao ya kila siku kama kielelezo cha uwepo na ushuhuda wao wa Kiinjili katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii, ili kujenga mazingira ya amani na utulivu. Lakini mambo yamekwenda mrama sana kwa maadhimisho ya Juma Kuu kwa Mwaka 2020 kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko kwa kusoma alama za nyakati, akaridhia ombi lililowasilishwa kwake na Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki na kuamua kwamba, mchango wa mshikamano na upendo wa kidugu ufanyike Jumapili, tarehe 13 Septemba 2020 katika makesha ya kuadhimisha Sherehe ya Kutukuka kwa Fumbo la Msalaba, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba.

Hii ni Siku ambayo Masalia ya Msalaba Mtakatifu yaligunduliwa huko Yerusalemu na huo ukawa mwanzo wa ujenzi wa Kanisa kuu la Kaburi Takatifu na Ibada ya hadhara. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 13 Septemba 2020, amesema kwamba, mchango wa mshikamano kwa ajili ya Nchi Takatifu ni kielelezo cha matumaini, mshikamano na ujirani mwema na watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu. Hapa ni mahali ambapo Neno wa Mungu alitwaa mwili na kukaa kati ya waja wake, akatangaza na kushuhudia uwepo wa ufalme wa Mungu, akateswa, akafa, akazikwa na kufufuka siku ya tatu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Yerusalemu, kwa kufanya matendo ya huruma, ili kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Papa Nchi Takatifu 2020
13 September 2020, 15:03