Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia umuhimu wa wongofu wa shughuli za kichungaji, wongofu wa kiekolojia pamoja na wongofu wa kiutu! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia umuhimu wa wongofu wa shughuli za kichungaji, wongofu wa kiekolojia pamoja na wongofu wa kiutu! 

Papa Francisko: Wongofu Wa Kichungaji, Kiekolojia na Kiutu!

Wongofu wa kiekolojia ni mchakato unaowawezesha waamini kutambua dhamana na wajibu wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utunzaji bora wa mazingira uwe ni kielezo cha upendo na mshikamano ili kuondokana na dhambi ya unyonyaji, kama ilivyo hata katika mazingira kwa kutaka kupora rasilimali hii adhimu kwa ajili ya mafao binafsi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amekutana na kuzungumza na wataalam wa mazingira wanaoshirikiana kwa karibu zaidi na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, “Laudato si”. Baba Mtakatifu katika hotuba yake aliyowapatia kwa maandishi amedadavua mambo makuu matatu: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, unazungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ekolojia vinavyohusiana na watu; Ekolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ekolojia na maisha ya kiroho.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6 - 27 Oktoba, 2019 yaliongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kusikiliza na kuanza mchakato wa wongofu fungamani unaosikiliza na kujibu kwa makini kilio cha maskini wa Ukanda wa Amazonia pamoja na kilio cha Dunia Mama. Njia mpya za wongofu wa kichungaji zinalitaka Kanisa kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari kwa kutambua kwamba, linapaswa kuwa ni kielelezo cha Msamaria mwema, chombo cha huruma ya Mungu kinachokita maisha na utume wake katika mshikamano. Wongofu wa kichungaji unajielekeza zaidi katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Lengo ni kusikiliza na hatimaye, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya watu mahalia! Wongofu wa kiekolojia ni mchakato unaowawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutambua dhamana na wajibu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Utunzaji bora wa mazingira uwe ni kielezo cha upendo na mshikamano kwa jirani, ili kuondokana na dhambi ya kutaka kuwanyonya watu wengine, kama ilivyo pia hata katika mazingira kwa kutaka kupoka na kupora rasilimali hii adhimu kwa ajili ya mafao binafsi. Hapa kuna haja ya kufanya “metanoia” yaani “kutubu na kumwongokea Mungu” mintarafu ekolojia! Kwa maneno mafupi huu ndio wongofu wa kiekolojia. Baba Mtakatifu Francisko ametoa ufafanuzi huu makini kwa kuonesha chanzo cha dhana ya wongofu wa kiekolojia kuwa ni Maadhimisho ya Mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, uliofanyika huko Aparecida, nchini Brazil kunako mwaka 2006 na kunako mwaka 2015 Baba Mtakatifu akachapisha Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Kipindi chote hiki, kimekuwa ni hija ya toba na wongofu wa kiekolojia, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika wongofu wa kiekolojia

Huu ni mwaliko wa kutambua na kuthamini tunu msingi za maisha ya watu asilia pamoja na kuthamini vipaumbele vyao katika maisha, ili kuweka uwiano mzuri zaidi kati ya uhalisia wa maisha na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kutambua asili na mizizi ya tunu msingi za maisha ya jamii inayowazunguka na kamwe wasikubali kugenishwa na mambo mpito! Baba Mtakatifu anasema, hii ni changamoto mamboleo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kuna uwiano bora zaidi kati ya lugha ya kichwa ambayo inajikita katika kufikiri, lugha ya moyo inajielekeza zaidi katika kusikiliza na lugha ya mikono ni kutenda kwa ujasiri. Kila mtu aweze kusikia kile anachofikiri na kutenda kile anachosikia na kufikiri. Huu ni uwiano wa hekima na busara.

Huu ndio mwongozo wa wongofu wa kiekolojia, ili kufikiri na kutenda kiutu, kwa huruma na upendo; kwani mambo yote haya yanahusiana na kukamilishana. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wajifunze kuenzi, kuheshimu na kuthamini tamaduni zao. Hii ni changamoto muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya kupyaisha mizizi ya tamaduni zao, kama sehemu muhimu sana ya utambulisho wao. Vijana wa kizazi kipya wajenge na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi na wazee. Wazazi wajenge utamaduni wa kuzungumzana na watoto wao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazee wana ndoto za kinabii wakati vijana wana mwono wa maisha. Ushuhuda ni mahali ambapo waamini wanaweza kugundua mpango wa Mungu katika maisha yao na kwamba, hii ndiyo ekolojia ya kibinadamu!

papa ekolojia

 

07 September 2020, 15:14