Papa Francisko analitaka Kanisa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ili kuwafunda vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Papa Francisko analitaka Kanisa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ili kuwafunda vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu. 

Papa Francisko: Wafundeni Vijana Wawe Vyombo Vya Amani Duniani!

Papa Francisko: Kanisa halina budi kushirikiana na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu, ili kusaidia kuwafunda vijana wa kizazi kipya watakaosimama kidete kulinda na kutunza Injili ya Uhai, amani na maridhiano. Kuna haja ya kuwa na vijana ambao wako imara katika utunzaji bora wa mazingira; watu ambao wako tayarii kulinda, kutetea na kudumisha haki, utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Idara ya Uchapaji ya Vatican, LEV., imeandika kitabu kijulikanacho kama "Per un sapere della pace" yaani “Kwa ajili ya ujuzi wa amani” na kuhaririwa na Bwana Gilfredo Marengo na dibaji yake kuandikwa na Baba Mtakatifu Francisko. Hiki ni kitabu chenye kurasa 124 na kinauzwa kwa bei ya Euro 14. Lengo la kitabu hiki ni kusaidia majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya mintarafu amani. Ni wajibu na dhamana ya Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anashirikiana kwa dhati kabisa na taasisi za elimu na vyuo vikuu sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya kuwafunda vijana wa kizazi kipya, ili wawe ni vyombo na wajenzi wa amani. Ni katika muktadha huu, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, kimeanzisha kozi maalum kuhusu ujenzi wa amani duniani. Kimsingi, Kitabu hiki kinapembua kwa kina na mapana kuhusu umuhimu wa kujenga agano, majadiliano katika ukweli na uwazi; utambulisho wa vijana, uhalisia wa maisha, upendo pamoja na wachangiaji wa mada katika kitabu hiki. Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” ulioachapishwa kunako tarehe 11 Aprili 1963 anakazia: ukweli, haki, upendo na uhuru wa watu wa Mungu.

Changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo kiasi cha kutishia mchakato wa: haki, amani na maridhiano kati ya watu ni pamoja na: vitendo vya kigaidi, ukosefu wa haki msingi za binadamu; uhuru wa kuabudu, uhalifu pamoja na misimamo mikali ya kidini inayopandikiza: chuki, hofu na utamaduni wa kifo! Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, leo hii kuna Vita ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande kutokana na utandawazi, kiasi kwamba, dunia leo hii imegeuka na kuwa kama kijiji, lakini watu wanaogopana kiasi kwamba, tofauti msingi kati ya watu, zimekuwa ni chanzo cha kudhaniana vibaya, chuki, uhasama, mipasuko ya kijamii na hatimaye kusababisha vita. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa halina budi kushirikiana kwa dhati kabisa na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu, ili kusaidia kuwafunda vijana wa kizazi kipya watakaosimama kidete kulinda na kutunza Injili ya Uhai, amani na maridhiano.

Kuna haja ya kuwa na vijana ambao wako imara katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; watu ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Haya ni mambo yanayopaswa kuendelea kupyaishwa na kuboreshwa zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kina kati ya falsafa, taalimungu, sheria na historia kwa kufanya tafiti za kina, huku tafiti hizi zikisaidiwa na mchango wa sayansi ya binadamu. Lengo ni kusaidia mchakato wa kukuza ujuzi, ufahamu na utambuzi wa amani duniani, ili hatimaye kuwafunda vijana wa kizazi kipya watakaojizatiti kama wajenzi wa amani katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu. Vijana kama wajenzi wa amani duniani wanapaswa kuwa na mwono mpana wa historia na mapendekezo yanayoweza kunafsishwa katika uhalisia wa maisha ya watu ili kudumisha amani.

Huu ni mwelekeo wa kijamii unaoambata na kufumbata hali halisi ya maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa vijana wanaojiandaa kuwa ni wanasayansi wa amani duniani, wanapaswa kujifunza kusoma alama za nyakati; kwa kuendelea kujizatiti katika tafiti makini za kisayansi, huku wakiwa na moyo wazi, tayari kushirikishana na jirani zake: furaha ya Injili, mateso na machungu ya walimwengu, tayari kufanya mang’amuzi ya Kiinjili. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wajenzi wa amani wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo. Wanafunzi wasaidiwe kutambua wito na dhamana yao kama waamini walei, ili waweze kuwa tayari kumwilisha Injili ya upendo katika maisha ya ndoa na familia; wasimame kidete kutangaza na kushuhudia upendo jamii na hata katika masuala ya kisiasa. Huu ni wajibu na dhamana inayobubujika moja kwa moja kutoka katika msingi wa imani, ili hatimaye, kujenga jamii mpya.

Kimsingi, kitabu hiki ni matunda ya kongamano lililoadhimishwa kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, hapo tarehe 28 Februari 2019. Kati ya wawezeshaji walioshiriki katika kongamano hili ni pamoja na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, Padre Giulio Cesareo, Mkurugenzi wa Idara ya Uchapaji ya Vatican, LEV pamoja na Kardinali Renato Raffaele Martino, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani.

Papa: Amani
15 September 2020, 15:43