Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa faraja namatumaini kwa wale wote waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa faraja namatumaini kwa wale wote waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. 

Papa: Waamini Ni Mashuhuda wa Imani, Faraja Na Matumaini!

Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja na Injili ya matumaini kwa wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo. Wakiwa wamejawa na nguvu, karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, wajitahidi kujibu changamoto kwa njia ya mshikamano wa upendo. wale wote wanaokutana nao. Mshikamano ujenge uwezo wa kusikiliza kwa makini kilio cha Mama Dunia na maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake inayoongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 2 Septemba 2020, iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jengo la Mtakatifu Damas lililoko mjini Vatican, amejielekeza zaidi katika mshikamano unaoratibiwa na fadhila ya imani. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza mahujaji na wageni kutoka ndani na nje ya Italia waliohudhuria katekesi yake. Amesema, anamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amemwezesha tena kukutana mubashara na waamini, mahujaji na wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, binadamu ni kiumbe jamii, kumbe, mikutano ya namna hii ni muhimu sana katika ujenzi wa umoja na mafungamano ya kijamii, muhimu sana hata katika utulivu wa nyoyo zao. Baba Mtakatifu amewaalika kuendelea kusali ili janga hili la Virusi vya Corona, COVID-19 lisiwe ni sababu ya utengano na mipasuko ya kijamii, bali kikolezo cha umoja na mshikamano.

Baba Mtakatifu amewashauri kumkimbilia Roho Mtakatifu, ili aweze kuwakirimia nguvu na mapaji yake na hasa zaidi paji la ugunduzi, litakalowawezesha kutoka katika ubinafsi wao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja na Injili ya matumaini kwa wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo. Wakiwa wamejawa na nguvu, karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, wajitahidi kujibu changamoto mbalimbali kwa njia ya mshikamano wa upendo kwa wale wote wanaokutana nao na hasa zaidi wale wanaotegemea msaada wa kidugu kutoka kwao. Mshikamano wa upendo, ujenge uwezo wa kusikiliza kwa makini kilio cha Mama Dunia na maskini, ili kujenga na kudumisha: ukarimu, udugu na mshikamano.

Baba Mtakatifu amewaweka wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya chini ya ulinzi na maongozi ya Roho Mtakatifu, ili aweze kuwakirimia kadiri ya matamanio yao halali, yale yaliyofichika kwenye “sakafu ya mioyo yao”, daima wakiwa na imani thabiti, hata kama wakati mwingine, inawagharimu sana! Roho Mtakatifu ni mjenzi mkuu wa umoja na mshikamano ndani ya Kanisa na kati ya watu wote wenye mapenzi mema, ili kuweza kujenga ulimwengu unaosimikwa katika nguzo ya amani na mshikamano wa dhati. Baba Mtakatifu amewatakia wanafunzi wote wanaotarajia kuanza tena masomo tarehe 14 Septemba, 2020, maandalizi mema, heri na baraka. Amewatakia furaha na amani ya Kristo Yesu, iweze kuwashukia na kukaa juu yao!

Corona: Imani
02 September 2020, 13:53