Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katekesi tarehe 16 Septemba 2020: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote, Mtazamo wa tafakuri Papa Francisko katekesi tarehe 16 Septemba 2020: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote, Mtazamo wa tafakuri  (Vatican Media)

Papa Francisko: Uponyaji wa Ulimwengu: Mazingira na Tafakuri

Papa Francisko amejielekeza zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, mtazamo wa tafakuri! Katekesi hii imeongozwa na tafakari ya Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Mwanzo Sura 2: 8-9. 15. Hili ni simulizi kuhusu asili ya binadamu na uzuri wa bustani ya Edeni na mwishoni, Mwenyezi Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujiunga pamoja naye, ili kutafakari kuhusu janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa kuangalia madhara yake, mintarafu magonjwa ya kijamii. Katekesi hii ya kina, inaongozwa na Mwanga angavu wa Injili, Fadhila za Kimungu pamoja na Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hii ni nafasi muafaka ya kutumia Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kuisaidia familia ya binadamu kuganga na kuponya ulimwengu huu unaoteseka kutokana na magonjwa makubwa na mazito! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwa pamoja, wataweza kushiriki katekesi hii kama wafuasi wa Kristo Yesu anayeganga na kuponya, ili kujenga ulimwengu bora zaidi unaosimikwa katika matumaini kwa ajili ya kizazi cha sasa na vile vijavyo. Baba Mtakatifu katika mzunguko mpya wa katekesi unaongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 16 Septemba 2020, kwenye Uwanja wa Jengo la Mtakatifu Damas lililoko mjini Vatican, katekesi iliyofanyika mubashara kwa ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbalimbali za dunia, amejielekeza zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, mtazamo wa tafakuri!

Katekesi hii imeongozwa na tafakari ya Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Mwanzo Sura 2: 8-9. 15. Hili ni simulizi  kuhusu asili ya binadamu na uzuri wa bustani ya Edeni na mwishoni, Mwenyezi Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ili mwanadamu aweze kuondoka katika janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 hana budi kujiganga mwenyewe pamoja na kuwaganga jirani zake. Huu ni mwaliko wa kuwaunga mkono wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini, wanyonge, wagonjwa na wazee, kwa sababu hawa ni watu wanaohitaji huduma ya pekee katika jamii ya leo, hata kama kwa bahati mbaya hawatambuliwi na kupewa huduma wanayostahili. Huu ni ushuhuda wa imani kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Matunzo halisi ya maisha ya binadamu, mahusiano na mafungamano na maumbile, kamwe hayatengani na udugu wa kibinadamu, haki na uaminifu kwa jirani. Hii ni amana na utajiri wa kibinadamu na kikristo!

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, hauna budi pia kuelekezwa katika matumizi bora ya ardhi pamoja na huduma kwa kila kiumbe. Hii inatokana na ukweli kwamba, kila kitu kinahusiana na kingine na kwamba, changamoto mamboleo zinapaswa kufanyiwa kazi kwani Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kutunza kazi ya uumbaji. Uharibifu wa kazi ya uumbaji katika kiwango chochote kile ni dhambi dhidi ya binadamu na dhidi ya Mwenyezi Mungu hali inayojionesha katika madhara ya vita, vurugu na dhuluma mbalimbali. Matumizi bora ya mazingira nyumba ya wote, ni mwaliko wa kusimama na kutafakari. Mtu asipojifunza kuthamini kitu vizuri, watu wasishangae wanapokichukulia kila kitu kama kifaa cha kutumiwa ovyo bila hata aibu. Kila kiumbe kina mionzi ya hekima na wema wa Mungu usiokuwa na mipaka. Kumbe kazi ya uumbaji inapaswa kuheshimiwa kwa kuepukana na matumizi yasiyofaa ambayo yangemdharau Mwenyezi Mungu, Muumbaji. Tafakuri ya kina inaganga na kuponya roho!

Ili kutambua mionzi hii ya hekima na wema wa Mungu, kuna haja ya kutunza ukimya, kusikiliza na kutafakari. Bila tafakari makini kuna hatari ya kutopea katika ubinafsi kwa mwanadamu kujiangalia peke yake pasi na uwiano bora pamoja na kuonesha jeuri na kiburi kinachomfanya binadamu kudhani kwamba, ni mtawala wa viumbe vyote. Tafsiri potofu ya Maandiko Matakatifu imepelekea matumizi mabaya ya kazi ya uumbaji. Mwanadamu “amejimwambafai” na kudhani kwamba, ni Mungu na kwa mwelekeo huu, ameharibu mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Ni kweli kabisa, mwanadamu anapaswa kuitumia ardhi kwa ajili ya maisha na maendeleo yake, lakini, anapaswa kukumbuka kwamba, utume wake ni kuhakikisha kuwa anailima na kuitunza; anaitumia na kuilinda. Mwanadamu hataweza kupata maendeleo ya kweli, bila kujizatiti katika kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote inayotoa hifadhi kwa viumbe vyote. Maskini na wanyonge zaidi pamoja na Mama Dunia wanao wasi wasi mkubwa kuhusu uharibifu ambao umefanywa na binadamu na wanadai mchakato wa wongofu wa kiekolojia.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa na mtazamo wa tafakuri, ili kutambua na kung’amua matumizi sahihi ya kazi ya uumbaji kama zawadi inayoonesha mionzi ya hekima na wema wa Mungu, kama wanavyofafanua Mababa wa maisha ya kiroho. Huu ni mwaliko wa tafakuri na hatima yake ni upendo, kielelezo cha furaha na upendo unaooneshwa na Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake. Ni nafasi ya kutambua uwepo wa Mungu katika viumbe vyake, kwa uhuru kamili na neema; kwa kuvipenda na kuvilinda. Tafakuri hii inawawezesha waamini na watu wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa kujizatiti kutunza mazingira, kwa kutambua kwamba, hata binadamu ni sehemu fungamani ya uzuri wa kazi ya uumbaji. Ni katika muktadha huu, binadamu anahisi ndani mwake wito wa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Asiyejua kutafakari hana pia uwezo wa kutafakari amana na utajiri wa binadamu. Matumizi mabaya ya kazi ya uumbaji yanapelekea pia unyonyaji unaowageuza watu wengine kuwa watumwa. Ikumbukwe kwamba, wote ni ndugu wamoja!

Kwa mtu mwenye tafakuri ya kina, ana uwezo wa kujizatiti ili kubadili yale mambo yanayosababisha uchafuzi wa mazingira pamoja na madhara yake katika afya ya binadamu. Atajizatiti katika elimu itakayosaidia kuleta mwelekeo mpya wa tabia ya uzalishaji na ulaji, ili kuchangia katika mfumo mpya wa uchumi unaoheshimu na kuthamini utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Tafakuri inayomwilishwa katika matendo, ina mwelekeo wa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, kwa kuunganisha mapokeo na tamaduni kutoka kwa wahenga pamoja na njia mpya za maendeleo ya teknolojia, ili mtindo wa maisha ya binadamu uweze kuwa ni fungamani. Mwenyezi Mungu anasamehe daima, lakini uharibifu wa mazingira hauna msamaha hata kidogo. Uchafuzi wa mazingira umepelekea ongezeko la joto duniani, hali inayotishia kuyeyuka kwa barafu na hivyo kuwepo na ongezeko la kina cha bahari na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kumbe, kuna haja ya kujenga mahusiano na mafungamano ya kidugu kati ya binadamu na kazi ya uumbaji, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; pamoja na kuendelea kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai na chemchemi ya matumaini dhidi ya utamaduni wa kifo.

Tafakuri na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mwelekeo unaopaswa kuvaliwa njuga, kwani unaonesha uhusiano kati ya mwanadamu pamoja na kazi ya uumbaji. Kwa kufuata na kutekeleza njia hii, waamini wanakuwa ni walinzi wa nyumba ya wote, watunzaji wa zawadi ya uhai na matumaini. Watu wanapaswa kuwajibika barabara kulinda na kutunza amana na utajiri ambao Mwenyezi Mungu amewakabidhi kwa ajili ya matumizi ya kizazi cha sasa na kile kijacho! Binadamu anapaswa kuwa na mwelekeo mpana zaidi kwa kutambua amana na urithi anaotaka kukiachia kizazi cha sasa na kile kijacho. Mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya utunzaji wa Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu anapenda kuyaelekeza mawazo yake kwa watu mahalia, ambao kimsingi, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwatambua, kutubu na kuongoka kutokana na ubaya waliowatendea na hatimaye, kuwalipa fidia. Anawafikiria pia wanaharakati, vyama vya kitume pamoja na makundi mbalimbali yanayoendelea kujipambanua kwa ajili ya kulinda maeneo, tunu msingi za maisha pamoja na tamaduni zao. Kwa bahati mbaya sana, ukweli huu wa kijamii, hauungwi mkono sana na wakati mwingine umeonekana kuwa kama ni kikwazo. Lakini, ni ukweli unaosaidia kuchangia mapinduzi ya amani, mapinduzi ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya binadamu wote. Kwa kuwa ni watunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, wanawezeshwa kumtukuza Mungu, kutafakari na kulinda kazi ya uumbaji.

Papa Mazingira 2020

 

 

16 September 2020, 15:21