Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 30 Septemba 2020 amekazia mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika mchakato wa uponyaji wa ulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 30 Septemba 2020 amekazia mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika mchakato wa uponyaji wa ulimwengu. 

Papa Francisko: Uponyaji wa Ulimwengu: Mambo Ya Kuzingatia!

Baba Mtakatifu amekazia: Umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kama changamoto pevu ya kiimani. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakazia mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaoratibiwa na kanuni auni. Upendeleo kwa maskini ni sehemu ya Mapokeo thabiti ya Mama Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Heri za Mlimani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akitafakari kuhusu janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa kuangalia madhara yake, mintarafu magonjwa ya kijamii kwa kuongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu.”Tafakari hii makini, imekuwa ikiongozwa na Mwanga angavu wa Injili, Fadhila za Kimungu pamoja na Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hii imekuwa ni nafasi muafaka ya kutumia Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kuisaidia familia ya binadamu kuweza kuganga na kuponya ulimwengu huu unaoteseka kutokana na magonjwa makubwa na mazito! Yaani: mwono tenge wa mwanadamu, uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote; Ubinafsi na uchoyo. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kama changamoto pevu ya kiimani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakazia mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaoratibiwa na kanuni auni.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, upendeleo kwa ajili ya maskini ni sehemu ya Mapokeo thabiti ya Mama Kanisa yanayopata chimbuko lake kwenye Heri za Mlimani, Ufukara wa Kristo Yesu pamoja na huduma yake kwa maskini katika sura zake mbali mbali. Kristo Yesu mwenyewe alijilinganisha na maskini! Kumbe, Kanisa ni chombo cha faraja, utetezi na ukombozi kwa ajili ya maskini. Baba Mtakatifu anasema kanuni za kudumu kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa zinakita mizizi yake katika: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Mafao kwa wote, auni, na mshikamano. Mshikamano unatoa mwanga wa mafungamano ya maumbile ya kijamii kwa kukazia usawa, heshima, haki na watu kujisadaka katika ujenzi wa umoja unaofumbatwa katika kanuni maadili, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumtazama Kristo Yesu kwa jicho la imani, ili kuweza kuambata na kukumbatia Injili ya matumaini ya Ufalme wa Mungu ambao umeletwa na Kristo Yesu.

Huu ni Ufalme wa uponyaji na wokovu; haki na amani inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma na mapendo. Ni Injili ya imani, matumaini na mapendo. Haya ni mambo msingi katika mwanga angavu wa Injili yanayoweza kusaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo vya mabadiliko katika mchakato wa kuponya ulimwengu na hivyo kuunda ulimwengu mpya na bora zaidi. Huu ni muhtasari wa katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 30 Septemba 2020 kwenye Uwanja wa Jengo la Mtakatifu Damas lililoko mjini Vatican. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Katekesi hii haitakomea hapa bali itaendelea kufanyiwa kazi kwa kutembea kwa pamoja huku wakimtazama Kristo Yesu anayeokoa, anayeganga na kuuponya ulimwengu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake aliganga roho na miili ya watu, alisamehe dhambi, akawarudishia watu afya ya miili yao na kulitaka Kanisa liendeleze kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kazi yake ya uponyaji na ya wokovu.

Kristo Yesu alipyaisha na kuvipatanisha viumbe vyote, kiasi cha kuwakirimia wafuasi wake zawadi muhimu za kupenda, kuganga na kuponya kama alivyokuwa akitenda yeye mwenyewe, kwa kuwahudumia wote pasi na ubaguzi wa aina yoyote ile yaani: rangi, lugha au utaifa wa mtu. Ili haya yaweze kutendeka, Baba Mtakatifu Francisko anasema,  kuna haja ya kutafakari, kusifu na kuthamini haki msingi, utu na heshima ya binadamu pamoja na viumbe wengine wote, kwa sababu wote ni kielelezo cha upendo wa Mungu na kila kiumbe kinatoa mionzi ya hekima na wema wa Mungu usio na mipaka. Hii ni changamoto ya kuweza kuuona ukweli katika mwanga wa Fumbo la Utatu Mtakatifu sanjari na kutambua uhusiano wa umoja uliopo kati ya watu na viumbe vyote kwa kuvitunza na kuvihudumia kwa ukarimu. Mwelekeo huu wa kiimani unawasaidia waamini kutambua uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na waja wake, hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Huu ni mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama pamoja na Maskini, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa. Familia ya binadamu inapaswa kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa ufalme wa Mungu unaosimikwa katika misingi ya haki, ukweli, usawa pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama sehemu ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Hii ndiyo changamoto ambayo inapaswa kuvaliwa njuga ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa ulimwenguni. Katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watu wanapata mahitaji yao msingi; watu wanashirikishana katika kuzalisha na kugawana. Huu ni mshikamano wa upendo unaopata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia bila wema na huruma, hayataweza kufua dafu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Upendo wa Kristo Yesu, unawawajibisha waamini kuwakaribia jirani zao, kutembea nao kwa pamoja, kuwaganga, kuwaponya na kuwasaidia, mambo yanayohitaji sadaka ya pekee. Virusi vya Corona, COVID-19 vimeendelea kuanika udhaifu na mapungufu ya binadamu; vimeonesha ukosefu mkubwa wa usawa katika fursa na matumizi ya rasilimali za dunia hii. Leo hii kuna mamilioni ya watoto hawawezi kwenda shule wala kupata huduma makini ya tiba. Lakini kuna watu duniani wanakula, wanashiba na kusaza na hata wakati mwingine, kutupa chakula ambacho kingeweza kutumiwa na watu wanaopekenywa na baa la njaa duniani. Kuna haja ya kuganga na kuponya magonjwa si tu yale yanayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 bali hata magonjwa yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni magonjwa yanayokita athari zake katika masuala ya kiuchumi na kijamii. Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee na wala kamwe wasichukuliwe kama watu wanaosubiri hisani baada ya wafadhili, kula, kushiba na kusaza.

Huruma, upendo na mshikamano wa kidugu ni mambo msingi katika ujenzi wa umoja na nguvu dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwaweka waamini na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa afya njema, ili awaombee waweze kuwa na imani thabiti. Chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, watu wanaweza kufanya kazi kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, ulioanzishwa na Kristo Yesu kwa ujio wake hapa duniani. Huu ni ufalme wa mwanga dhidi ya giza; ni Ufalme haki katika maeneo ambayo hayana haki; ni Ufalme wa furaha kati ya watu wanaoteseka na ni Ufalme unaoganga na kuponya watu wanaoteseka na magonjwa pamoja na kuandamwa na kifo. Huu ni Ufalme wa upendo kati ya chuki na uhasama. Huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba, watu wanaeneza upendo wa Mungu na utandawazi wa matumaini katika mwanga wa imani.

Papa Katekesi

 

30 September 2020, 15:41