Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Jukwaa la Uchumi la Ambrosseti amekazia: Masuala ya uchumi, Mang'amuzi, Kanuni Maadili na Utu wema, Wongofu wa Kiekolojia Ugunduzi na Miji kwa siku za usoni. Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Jukwaa la Uchumi la Ambrosseti amekazia: Masuala ya uchumi, Mang'amuzi, Kanuni Maadili na Utu wema, Wongofu wa Kiekolojia Ugunduzi na Miji kwa siku za usoni. 

Papa Francisko: Uchumi: Wongofu Wa Kiekolojia na Kanuni Maadili

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kwa kwa Jukwaa la Uchumi la Ambrosetti amejikita katika masuala ya kiuchumi yanayoitawala dunia nyumba ya wote; Umuhimu wa kufanya mang’amuzi yanayosimamiwa na kanuni maadili na utu wema, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; Wongofu wa kiekolojia; Kipaji cha ugunduzi na hatimaye, mwelekeo wa miji kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wajumbe wa Jukwaa la “The Forum of the European House-Ambrosseti” kuanzia tarehe 4 hadi 5 Septemba 2020 wanaadhimisha mkutano wao huko mjini Cernobbio, Kaskazini mwa Italia unaojadili masuala tete yanayogusa undani wa jamii, uchumi pamoja uvumbuzi. Haya ni masuala mtambuko yanayohitaji nguvu ya pekee ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zilizoibuliwa na hali tete ya huduma ya afya, kuchechemea kwa uchumi sanjari na dharura ya masuala ya kijamii. Janga la homa kali ya mapafu, COVID-19 linaonesha umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kama njia ya kupambana na janga hili ambalo bado ni tishio kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wanapaswa kujisikia kuwa wao ni sehemu ya familia kubwa ya binadamu na kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana katika ulimwengu huu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Watu wote wanatambua kwamba wote wanaishi katika dunia nyumba ya pamoja, kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, ili kuweza kutumia vyema amana, utajiri na mali za dunia, kwani binadamu amejifunza vizuri zaidi kushikamana wakati wa “shida na patashika nguo kuchanika.”. Janga hili limesaidia Jumuiya ya Kimataifa kutambua na kuthamani juhudi za wanasayansi katika kukabiliana na changamoto mbali mbali pamoja na ukomo wa uwezo wao. Watu wamejifunza kupanga vipaumbele na tunu msingi za maisha ya kijamii. Changamoto ya watu kukaa karantini, imewafanya kujifunza maana halisi ya furaha na mafungamano ya kijamii, kiasi hata cha kutoa kipaumbele cha pekee kwa mambo msingi katika maisha. Baadhi ya nguzo zilizokuwa zinatumika kubeba mifumo mbali mbali ya kiuchumi imeporomoka.

Leo na kesho ya binadamu inaonekana kuwa mashakani kutokana na changamoto pevu zinazoendelea kuibuliwa hususan katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya mang’amuzi ya kina, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa mambo msingi yatakayosaidia kuchochea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 4 Septemba 2020 ametuma ujumbe kwa Wajumbe wa Jukwaa la “The Forum of the European House-Ambrosseti.” Katika ujumbe wake, Baba Mtakatifu amejikita katika masuala ya kiuchumi yanayoitawala dunia nyumba ya wote; Umuhimu wa kufanya mang’amuzi yanayosimamiwa na kanuni maadili na utu wema, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; Wongofu wa kiekolojia; Kipaji cha ugunduzi na hatimaye, mwelekeo wa miji kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, uchumi katika maana yake ya ndani ni utawala thabiti wa dunia kama nyumba ya wote, kwa sababu ya mwingiliano na mafungamano yake katika maisha na mahusiano ya watu. Uchumi halisi unasimikwa katika misingi inayowashirikisha watu kwa lengo la kutaka kuinua na kuboresha maisha; kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu badala ya kuabudu na kuthamini fedha. Lengo ni kuondokana na vurugu na ukosefu wa usawa. Rasilimali fedha iwe ni kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mungu. Faida ya kweli iwe ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limebainisha kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia peke yake hayawezi kufua dafu, bali upendo, mshikamano, ukarimu na ujasiri ni mambo msingi katika kukabiliana na changamoto mamboleo. Uelewa sahihi wa mazingira unasaidia kuzuia maumbile yasigeuzwe kuwa ni chombo cha kujipatia faida kubwa tu na kuendeleza unyonyaji.

Papohapo, maumbile yasitawaliwe kiasi cha kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Pale ambapo kuna mazingira na watu wengi wanashirikishwa, hapo kuna haja ya kuwa na mtazamo na fikra mpya mintarafu teknolojia kwa ajili ya kuhudumia mifumo mbalimbali ya maendeleo ili iweze kuwa na afya bora zaidi, kwa kujikita katika utu wema kwa kumwangalia binadamu katika ukamilifu wake.Baba Mtakatifu anasema, kuna umuhimu wa kufanya mang’amuzi yanayosimamiwa na kanuni maadili na utu wema ili kuleta mabadiliko yanayotamaniwa na wengi. Mang’amuzi yaisaidie Jumuiya ya Kimataifa kusoma alama za nyakati kwa kujikita katika Maandiko Matakatifu na Mafundisho makuu ya Kristo Yesu yanayohitaji kimsingi wongofu wa ndani na kipaji cha ugunduzi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika wongofu wa kiekolojia ili kupunguza kasi ya uzalishaji na ulaji wa kupindukia, ili kutumia fursa hii kwa kutafakari juu ya maumbile, tayari kuunganishwa tena na ulimwengu unaowazunguka. Huu ni muda muafaka wa kuondokana na tabia potofu ya “kukwangua” rasilimali za dunia, hali inayohatarisha uchumi.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na matumizi ya: muda, rasilimali pamoja na nguvu yasiwapeleke watu mchakachaka, bali yasaidie kujenga uzoefu wa mafungamano ya kibinadamu. Huu ni mwaliko wa watu kuwa wabunifu na wajenzi watakaojikita zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuibua sera na mikakati ikayosaidia kuleta maendeleo fungamani. Huu ni ugunduzi wa upendo unaotoa maana ya maisha ya sasa na kujielekeza zaidi katika maboresho ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Wongofu wa kiekolojia na ubunifu ni mambo msingi ambayo wanapaswa kurithishwa vijana wa kizazi kipya. Hawa ni wachumi na wajasiriamali vijana. Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni tukio ambalo linatarajiwa kuwakusanya wachumi na wajasiriamali wachumi vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kuanzia tarehe 19-21 Novemba, 2020 huko Assisi, nchini Italia. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, unaotekelezwa kwa namna ya pekee, na Baba Mtakatifu Francisko.

Mtakatifu Francisko wa Assisi alimchagua Mwenyezi Mungu kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake! Akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maamuzi yake magumu ya kuambata na kukumbatia ufukara, ulikuwa ni mwanzo wa mwono mpya wa uchumi, ambao bado ni mfano bora wa kuigwa. Kuna haja ya kuwekeza miongoni mwa vijana wa kizazi kipya watakaokuwa wadau wa uchumi kwa siku za usoni. Ni muhimu sana kuwaandaa vijana watakaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya zao sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; vijana wanaothamini utu na udugu wa kibinadamu na kwamba, rasilimali fedha ni matokeo ya mambo hayo makuu. Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU, hapo tarehe 9 Mei 2020 imeadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Robert Schuman, Waziri Mkuu wa Ufaransa lilipotolewa kunako tarehe 9 Mei 1950. Tamko hili ni chimbuko la Umoja wa Ulaya, EU baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.  Tamko lilipania kuhakikisha kwamba, Bara la Ulaya linasitisha chuki, uhasama na kinzani na hivyo kuanza kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani, umoja, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Ulaya.

Amani Duniani itaweza kulindwa na kudumishwa kwa kujikita katika umoja na mshikamano, kwa kukusanya nguvu na rasilimali kwa ajili ya kupambana na mambo yale ambayo yanatishia: utulivu, amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Umoja wa Ulaya unahitaji kuonesha uongozi ambao unakita mizizi yake katika ubunifu unaonafsishwa katika masuala ya kisiasa na kiuchumi, kama kielelezo cha mshikamano, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Binadamu anapaswa kuwa ni kiini cha sera na mikakati ya huduma ya elimu, afya na uchumi. Watu wanapaswa kukaribishwa, kulindwa, kusindikizwa na kushirikishwa katika maisha ya jamii inayowakirimia, mara wanapobisha hodi, wakitafuta hifadhi, usalama na maisha ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa miji ijayo itakayopata utimilifu wake katika Yerusalemu ya mbinguni, mji wa amani, uliojengwa kwa ajili ya watu, wenye mazingira ya kuvutia na humo watu wanapata utimilifu wa maisha. Baba Mtakatifu anawasihi waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujielekeza zaidi katika ujenzi mpya wa uchumi na maendeleo yatakayopambana na mifumo yote inayowasukumizia watu pembezoni mwa jamii; kwa kutoa mwelekeo wa mfumo mpya wa maisha sanjari na kutoa sauti kwa wale wasiokuwa na sauti.

Papa: Uchumi

 

04 September 2020, 15:29