Papa Francisko: Toba na wongofu wa ndani ni neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Papa Francisko: Toba na wongofu wa ndani ni neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. 

Papa Francisko: Toba Na Wongofu wa Ndani Ni Neema ya Mungu

Papa Francisko: Watoza ushuru na makahaba ni watu ambao walipokea upendeleo wa pekee wa neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani toba na wongofu wa ndani ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama ilivyokuwa kwa Mathayo, mtoza ushuru. Mwana wa kwanza alimwambia baba yake kwamba, “Hataki”, lakini akatubu na kuongoka kutoka katika undani wa maisha yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Mathayo aliyekuwa ni mtoza ushuru na mbele ya watu akaonekana kuwa ni msaliti wa nchi yake katika Injili ya Jumapili ya 26 ya Mwaka A wa Kanisa, anaweka mbele ya macho ya wasomaji wake, Kristo Yesu anayefundisha umuhimu wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaomwilishwa katika maisha ya watu. Anakazia umuhimu wa kuunda dhamiri nyofu inayomwezesha mwamini kuchagua jema na kuachana na jambo baya katika maisha. Kristo Yesu anafafanua wazo hili kwa kutoa mifano wa mtu mmoja aliye kuwa na wana wawili, akamwambia yule wa kwanza nenda kafanye kazi shambani akamjibu naenda, lakini hakwenda. Akamwendea yule wa pili, akamwambia vilevile naye akajibu kwa kusema “Sitaki”, baadaye akatubu, akaenda shambani. Rej. Mt. 21:28-32. Hapa utii unafumbatwa kwa namna ya pekee katika kufikiri na kutenda kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu; kwa njia ya ushuhuda unaowawezesha watu kutenda mema zaidi.

Mafundisho ya Kristo Yesu yanapania kuwaelimisha wafuasi wake kuondokana na mambo yanayoonekana kwa nje zaidi na ambayo yanatendwa kwa njia ya mazoea. Huu ni mwelekeo wa dini ambayo haizamishi mizizi yake katika undani wa maisha ya mwamini, bali inabaki inaelea juu juu katika ibada zisizomgusa mtu katika undani wake. Na huu ndio uliokuwa mwelekeo wa wakuu wa makuhani na wazee wa watu wa kutaka kujionesha mbele ya watu. Lakini Kristo Yesu akawaonya na kuwaambia wasipokuwa makini watoza ushuru na makahaba watatangulia mbele yao kuingia katika Ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohane mbatizaji alikuja kwao kwa njia ya haki, hawakumwamini, lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, wakatubu na kumwongokea Mungu. Rej. Mt. 21:32. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 27 Septemba 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, watoza ushuru na makahaba si mfano bora wa maisha na baadhi ya watu waliokengeuka na kutopea katika mmong’onyoko wa kimaadili kudhani kwamba, hata wale wanaohudhuria Ibada ya Misa kila siku ni wadhambi tena kuliko wao. Watoza ushuru na makahaba ni watu ambao walipokea upendeleo wa pekee wa neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani toba na wongofu wa ndani ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama ilivyokuwa kwa Mathayo, mtoza ushuru. Mwana wa kwanza alimwambia baba yake kwamba, “Hataki”, lakini akatubu na kuongoka kutoka katika undani wa maisha yake. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, ni mvumilivu na anayewasubiri waja wake kutubu na kumwongokea. Mwenyezi Mungu daima yuko kandoni mwa wale wote wanaohitaji huruma na msaada wake, lakini anaheshimu uhuru wa kila mtu!

Daima amefungua mikono yake, ili kuwakaribisha na kuwapokea wanaotubu na kumwongokea ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Imani kwa Mwenyezi Mungu inamtaka mwamini kupyaisha dhamiri yake kwa kuchagua mema na kuachana na uovu; kwa kuchagua ukweli badala ya uwongo; kwa kukumbatia upendo kwa ajili ya Mungu na jirani na hivyo kuukataa ubinafsi. Kwa mtu yeyote anayeongokea katika mwelekeo huu wa maisha, baada ya kuonja adha ya dhambi na mateso yake, atakirimiwa nafasi ya kwanza katika Ufalme wa Mungu, mahali ambapo kuna furaha mbele ya Malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye. Rej. Lk 15: 7. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, toba na wongofu wa ndani ni mchakato unaowataka waamini kuachana na mambo yanayokwenda kinyume na kanuni maadili na utu wema. Njia ya toba na wongofu wa ndani ina machungu yake, kwa sababu huu ni mwaliko wa kujikana mwenyewe na kielelezo cha mapambano ya maisha ya kiroho.

Huu ni mchakato wa mapambano bila kutumbukia kwenye vishawishi, kwa kutekeleza yote kadiri wanavyowezeshwa na Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, waweze kuishi katika amani na furaha ya Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Injili ya Jumapili ya XXVI ya Mwaka A wa Kanisa ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuishi kama Wakristo, si katika ndoto na mambo ya kufikirika; bali imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu, daima wakiwa wazi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao; kwa kumpenda Mungu na jirani. Yote haya yanahitaji baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha tena kwamba, wongofu wa ndani ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe, waamini wanapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia daima neema hii. Bikira Maria awasaidie waamini kuwa wapole na wasikivu kwa Roho Mtakatifu kwani anawasaidia waamini kulainisha nyoyo zao, tayari kwa toba na wongofu wa ndani, ili hatimaye kupata maisha na uzima wa milele, ahadi kutoka kwa Kristo Yesu.

Neema ya Wongofu

 

27 September 2020, 16:13