Tafuta

PAPA FRANCISKO PAPA FRANCISKO 

Papa Francisko:Masengenyo dhidi ya wengine ni mdudu hatari zaidi ya covid!

Ndugu yako akikosa enenda ukamwonye,wewe na yeye peke yenu yaani usiweke dhambi zake mbele ya kadamnasi.Ina maana ya kwenda kwa ndugu yako kwa umakini bila kumhukumu,bali kwa ajili ya kumsaidia ili aweze kutambua alichofanya japokuwa siyo rahisi kama anavyoeleza Yesu katika Injili ya Siku.Na kusengenya wengine ni mdudu hatari zaidi ya covid.Ni tafakari ya Papa Dominika tarehe 6 Septemba 2020.

Na Sr. Angla Rwezaula – Vatican

Injili ya Dominika hii kutoka Mt 18,15-20 inahusu hotuba ya nne za Yesu katika simulizi ya Matayo ijulikanayo kama hotuba ya kijumuiya au ya Kikanisa. Sehemu ya leo hii inazungumzia masahihisho kidugu na kutualika kujitafakari juu ya mambo makuu mawili ya maisha ya kikristo. Masahihisho haya ni yale ya kijumuiya ambayo yanatakiwa kulinda muungano yaani umoja wa Kanisa na yale  ya kibinafsi ambayo yanahitaji umakini na heshima kwa kila dhamiri binafsi. Ndivyo Papa Francisko ameanza tafakari yake siku ya Dominika, tarehe 6 Septemba 2020 kabla ya sala ya Malaika wa Bwana akiwaelekea waamini na mahujaji waliounganika katika uwanja wa Mtakatifu Petro kusali sala ya Malaika wa Bwana. Papa Francisko akiendelea na tafakari hiyo amesema “ili kuweza kumsahihisha ndugu aliyekosa, Yesu anashauri njia ya kumrudisha.  Daima njia ya Yesu ni njia ya kuweza kujirudi. “Yeye daima anatafuta ili kuweza kumfanya mtu ajirudi na kuokoa na ndiyo kwa hakika njia ya kujirudi. Njia hii imegawanyika katika hatua tatu. Ya kwanza Yesu  anasema:“enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu” (Mt 18, 15), Papa Francisko anaongeza kufafanua kuwa “ usiweke dhambi zake mbele ya kadamnasi. Hii ina maana ya kwenda kwa ndugu yako ukiwa na umakini bila kumhukumu, kwa ajili ya kumsaidia aweze kutambua alichofanya”. “Ni mara ngapi sisi tumefanya uzoefu huu anauliza Papa. Na mwingine anaweza kuja na kusema “sikiliza katika hili umekosea. Unatakiwa kubadilisha kidogo kwa hilo”. Labda kwa mara ya kwanza utakarisika, lakini baadaye unamshukuru, kwa sababu ni ishara ya udugu, ya muungano, ya msaada na ya kujirudi”, Papa amesisitiza.

Kukosolewa na ndugu mara nyingi siyo rahisi

Njia hii, Papa Francisko anabainisha ya kwamba siyo rahisi kuiweka  katika matendo ya mafundisho ya Yesu kwa sababu nyingi. Awali ya yote ipo hofu ya kwamba kaka au dada anaweza kuichukulia vibaya; na mara nyingi inakosekana imani ya kutosha kwa kaka na dada… na sababu nyinginezo. Lakini mara nyingi hata sisi tumefanya hivyo, tumehisi kuwa ilikuwa ndiyo njia ya Bwana, Papa Francisko amebainisha. Pamoja na hayo yote inawezekana  kujitokeza kwamba licha ya nia njema, jaribio la kwanza likashindikana. Katika kisa hicho ni vizuri using’ang’anie, au kusema kuwa shauri lake, mimi ninanawa mikono, hapana, kwani siyo tabia ya kikristo usiache bali ukimbilie msaada wa kaka mwingine au dada. Yesu anasema: “lakini kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike” (Mt 18, 16).  Huu ulikuwa ni utaratibu wa sheria ya Musa (Kum 19,15).

Mashuhuda wanawekwa kwa ajili ya kusaidia na siyo kuhukumu

Pamoja na kwamba yawezekana kuona mashuhuda ni dhidi ya mshtakiwa lakini kiukweli itasaidia kulinda mashuhuda dhidi ya uongo. Pamoja na hayo yote  Yesu anakwenda mbali zaidi, kwani mashahuda walioombwa siyo kwa ajili ya kumshtaki na kuhukumu, baadala yake ni  kusaidia.  Hii lakini Papa anaongeza inatakiwa tukubaliane, mimi na wewe, twende tuzungumze na yeye anayekosea, ambaye yupo anaaibisha na muhimu twenda kwa ndugu huyo na kuzungumza naye!  Hii ndiyo njia ya kuweza kumrudisha na ambayo Yesu anatutaka kwetu sisi”. Kwa hakika Yesu anajua wazi kuwa hata njia hii na mashahuda pia inaweza kutofaulu, kinyume na sheria ya Musa, ambayo mashuhuda wawili au watatu walikuwa wanatosha kuhukumu.

Yapo mambo ambayo hayawezi kuachwa na sintofahamu

Kwa hakika hata upendo wa wawili au ndugu watatu unaweza usiwe wa kutosha kwa huyo na yule wenye vichwa vigumu. Katika kesi kama hiyo, Yesu anaongeza kusema “Na asipowasikiliza wao, liambie Kanisa” (Mt 18,17). Katika hali nyingine jumuiya nzima inajumuishwa. Kuna mambo mengine ambayo hayawezi kuachwa na sintofahamu kwa ndugu wengine. Lakini wakati mwingine inawezekana hata hiyo  isitoshe. Yesu anasema: “na asipolisikiliza kanisa pia, nawe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru”. Maneno haya, yanaonekana kuwa ya dharau japokuwa kiuhalisia yanamwalika ndugu ajiweke mikononi mwa Mungu.  Ni Baba peke yake anayeweza kuonesha upendo mkubwa zaidi ya ule wa ndugu wote waliojiweka pamoja.

PAPA SALA YA MALAIKA

Masengenyo ni mdudu wa hatari sana zaidi ya covid, bora kukaa kimya

Mafundisho haya ya Yesu yanatusaidia sana kwa sababu tufikirie mfano tunapotazama makosa, tabia mbaya, kuteleza kwa kaka au dada, kawaida tukifanyacho ni kwenda kuwasimulia wengine na kusengenyaMasengenyo ufunga mioyo ya Jumuiya, ufunga umoja wa Kanisa. Msengenyaji mkubwa ni ibilisi ambaye daima anakwenda na kusema mambo mabaya sana ya watu, kwa kuwa Yeye ni muongo na anatafuta kutenganisha Kanisa, kuwafanya ndugu waende mbali na wasifanye umoja na jumuiya.  Papa Francisko ametoa onyo: “Tafadhali kaka na dada tujitahidi tusifanye masengenyo. Masengenyo ni mdudu mbaya sana zaidi ya covid! Tujitahidi tusifanye  masengenyo”!  Ni upendo wa Yesu ambao ulimkaribisha mtoza ushuru na mpagani, kashfa kwa watu wenye kufikiria haki wa wakati huo. Hii siyo hukumu kwa maana ya kuwa bila rufaa, bali ni utambuzi ambao wakati mwingine kwa kujaribu kibinadamu inawezekana kushindwa na kwamba kujikuta yuko peke yake mbele ya Mungu inaweza kumpelekea ndugu huyo mbele ya dhamiri yake mwenyewe na uwajibikaji wa matendo yake. “Ikiwa jambo fulani haliendi basi ni kufanya kimya na kusali kwa ajili ya kaka na dada wanaokosea, lakini bora kutofanya masengenyo” Papa Francisko ameonya. Bikira Maria atusaidie kusahihishana kidugu, ambayo ni tabia njema ili katika jumuiya zetu tuweze kutengeneza kwa upya na daima mahusiano mapya kidugu, yanayosimika mizizi juu ya msamaha wa pamoja, na kwa nguvu isiyoshindwa ya huruma ya Mungu, Papa Francisko amehitimisha.

06 September 2020, 15:30