Vatican News
Katika maadhimisho ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75 Katika maadhimisho ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75  (ANSA)

Papa Francisko Kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75 unaongozwa na kauli mbiu “Yale tunayoyataka kwa siku za mbeleni, Umoja wa Mataifa Tunaouhitaji: Kuendelea kuthibitisha Majitoleo Yetu ya Pamoja”. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko baada ya tarehe 22 Septemba 2020 anatarajia kutuma ujumbe kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75. Wajumbe wanausubiri

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Mataifa unaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake hapo tarehe 24 Oktoba 1945 mara tu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ukiwa na nchi wanachama 51. Leo hii, Umoja wa Mataifa unajumla ya nchi wanachama 193. Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa ulipania pamoja na mambo mengine kujizatiti katika kulinda na kudumisha amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Umoja wa Mataifa ulipania kuendeleza urafiki miongoni mwa mataifa kwa kujielekeza zaidi katika maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na kuboresha hali ya maisha ya watu duniani. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75, tarehe 15 Septemba 2020 limefungua mkutano wake wa 75 na unaotarajiwa kuhitimishwa rasmi hapo tarehe 30 Septemba 2020, huku Jumuiya ya Kimataifa ikiwa inakabiliwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Changamoto nyingine ni athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinazohitaji wongofu wa kiekolojia, matumizi bora na rafiki ya nishati katika sekta ya kilimo, viwanda, usafiri na katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu.

Ulinzi na usalama ni changamoto kubwa inayotokana na utengenezaji, ulimbikizaji na tishio la matumizi ya silaha za maangamizi duniani. Kuna vita sehemu mbalimbali za dunia, baa la njaa pamoja na mifumo ya ubaguzi inayotishia: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75 unaongozwa na kauli mbiu “Yale tunayoyataka kwa siku za mbeleni, Umoja wa Mataifa Tunaouhitaji: Kuendelea kuthibitisha Majitoleo Yetu ya Pamoja”. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko baada ya tarehe 22 Septemba 2020 anatarajia kutuma ujumbe kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 75. Hayo yamethibitishwa na Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican alipokuwa anajibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari mjini Vatican. Pamoja na mambo mengine, Mkutano huu unajadili kuhusu viumbe hai; Kumbukumbu ya Miaka 25 ya Mkutano wa Nne wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake, (FWCW) uliofanyika Beijing, China mwezi Septemba, 1995.

Kutakuwa pia na maadhimisho ya Juma la Hali ya Hewa. Huu ni muda muafaka wa kupokea taarifa rasmi kuhusu mwenendo wa mabadiliko ya tabianchi duniani. Mwishoni, kutakuwa na ajenda tete ya Siku ya maadhimisho ya Kufuta Matumizi ya Silaha za Nyuklia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumzia “dhana ya silaha za nyuklia”.

Papa: Umoja wa Mataifa

 

 

17 September 2020, 14:33