Tafuta

Papa Francisko anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa msamaha wa upendo. Papa Francisko anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa msamaha wa upendo. 

Papa: Jengeni Utamaduni wa Msamaha Wenye Huruma!

Papa Francisko anasema, Kristo Yesu anawahamasisha waja wake, kuwa na nguvu na ujasiri wa kusamehe kwa sababu katika maisha si kila kitu kinaweza kupewa ufumbuzi kwa njia ya haki. Kuna haja ya kujenga na kumwilisha utamaduni wa upendo wa msamaha kama jibu muafaka kwa swali la Mtakatifu Petro kwa Kristo Yesu. “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya XXIV ya Mwaka A wa Kanisa unajikita katika haki na huruma ya Mungu kama unavyosimuliwa na Mwinjili Mathayo 18: 21-35. “Nivumilie nami nitakulipa yote” ni maneno ya mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta elfu kumi na Mfalme. Maneno haya yanasikika kwa mara nyingine tena yakitamkwa na mtumwa mwingine wa Mfalme kwa kusema, “nivumilie, nami nitakulipa yote pia”. Maneno haya anaambiwa yule mtumwa aliyesamehewa deni kubwa na Mfalme wake, lakini akashindwa kumsamehe mtumwa mwenzake, lile deni dogo alilokuwa anamdai! Mfalme anaonesha huruma kwa mtumwa aliyekuwa anadaiwa deni kubwa na Mwinjili Mathayo anakaza kwa kusema, Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Kiasi hiki cha fedha, leo hii kingekuwa ni kikubwa sana.

Deni lilikuwa ni kubwa na msamaha wake pia ulionekana kuwa ni mkubwa zaidi. Lakini yule mtumwa alionekana kukosa huruma, kwani yule mtumwa, akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia sawa na mshahara wa mtu kwa juma moja; akamkamata, akamshika koo akitaka alipwe deni yake. Basi yule mjoli akamsihi amvumilie, lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Bwana wake alipomsikia, akagadhabika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Katika Injili hii, kuna mielekeo miwili, ule wa Mfalme unaonesha kwamba, huruma ya Mungu inavuka mipaka ya haki na mwelekeo wa pili ule wa kibinadamu unagota zaidi katika haki. Mwenyezi Mungu daima yuko tayari kusamahe na kusahau!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 13 Septemba 2020. Kristo Yesu anawahamasisha waja wake, kuwa na nguvu na ujasiri wa kusamehe kwa sababu katika maisha si kila kitu kinaweza kupewa ufumbuzi kwa njia ya haki. Kuna haja ya kujenga na kumwilisha utamaduni wa upendo wa msamaha kama jibu muafaka kwa swali la Mtakatifu Petro kwa Kristo Yesu. “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Lakini, Kristo Yesu anamjibu kwa kusema “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.” Rej. Mt. 18: 21-22. Baba Mtakatifu anasema hii ni lugha ya picha katika Maandiko Matakatifu inayomaanisha kwamba, watu wa Mungu wanahimizwa kusamehe daima pasi na ukomo!

Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Francisko ikiwa kama huruma na upendo vingekuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu, leo hii kusingelikuwepo na vita, kinzani wala mipasuko ya kijamii. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, upendo wenye huruma unanafsishwa kwenye mahusiano na mafungamano ya kibinadamu; kati ya watu wa ndoa, kati ya wazazi na watoto wao; ndani ya jumuiya, katika jamii na hata katika masuala ya kisiasa. Inasikitisha kuona kwamba, hata leo hii bado kuna ndugu ambao wamewekeana kinyongo na wanataka kulipizana kisasi. Baba Mtakatifu anasema, ameguswa na maneno haya: “Kumbuka mwisho wako, uuache uadui; kumbuka uozi na mauti, ujiepushe na kutenda dhambi”. Haya ni maneno kutoka katika Somo la kwanza anakaza kusema, waamini wajenge utamaduni wa kusamehe, ili hata wao waweze kupata msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mfano wa Injili hii, ni mwaliko wa kutambua maana ya maneno yaliyoko kwenye Sala ya Baba Yetu “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.” Mt. 6:12. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inabeba ukweli wenye maamuzi mazito. Mwanadamu asitegemee kupata msamaha kama yeye mwenyewe hawezi kutoa msamaha kwa jirani zake. Huu ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kusamahe na kupenda, ili hata wao waweze kusamehewa na kupendwa zaidi. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kwa maombezi ya Bikira Maria, awasaidie kutambua jinsi ambavyo wanadaiwa mbele ya Mwenyezi Mungu, ili daima, waweze kuwa na mioyo wazi kwa ajili ya wema na huruma.

Papa: Msamaha
13 September 2020, 15:25