Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na wanamichezo wa mshikamano kwa ajili ya kusaidia kuchangia fedha kwa ajili ya waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko amekutana na wanamichezo wa mshikamano kwa ajili ya kusaidia kuchangia fedha kwa ajili ya waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. 

Papa Francisko Akutana na Wanamichezo Wa Mshikamano

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwanza amewashukuru kwa kujisadaka kwa ajili ya kuchangia huduma kwa wagonjwa wa Virus vya Corona, COVID-19. Amewakumbusha wanamichezo hao kwamba, wao ni chemchemi ya furaha na amani ya ndani kwa watu wengi wanaokutana nao katika hija ya maisha yao. Michezo inapaswa kuchangia: ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di se”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbali mbali, ili kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu, furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Michezo katika nafasi  mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu; ni njia ya mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, ili waweze kutambua umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu wa kibinadamu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuandika ukurasa mpya wa michezo katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita zaidi katika mchakato wa: Ushirikishwaji; ukweli, uwazi na uaminifu pamoja kuwa na upendeleo kwa maskini.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 5 Septemba 2020 amekutana na kuzungumza na Kikundi cha wanamichezo walemavu waliokuwa wameongozana na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni.  Hili ni kundi la wanamichezo wa mshikamano “Tunakimbia kwa pamoja” “We run together, Simul Currebant”. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwanza amewashukuru kwa kujisadaka kwa ajili ya kuchangia huduma kwa wagonjwa wa Virus vya Corona, COVID-19. Amewakumbusha wanamichezo hao kwamba, wao ni chemchemi ya furaha na amani ya ndani kwa watu wengi wanaokutana nao katika hija ya maisha yao. Michezo inapaswa kuchangia: ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao kama ambavyo walivyofanya kwa kukusanya fedha zitakazopelekwa kwenye Hospitali ya “Papa Giovanni XXIII” iliyoko huko Bergamo, Kaskazini mwa Italia na kiasi kingine, kitatumwa kwenye Mfuko wa Hospitali Brescia, maeneo ambayo hivi karibuni, yalikumbwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wanamichezo mbalimbali kutoka ndani na nje ya Italia, ambao kwa njia ya miradi ya michezo wamechangia kwenye mfuko wa mshikamano na baadhi ya wanamichezo wamefungua malango ya nyumba zao kwa kuwakaribisha maskini, kielelezo cha upendo na ukarimu, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wanamichezo wenye ulemavu wanayo nafasi na heshima kubwa katika ulimwengu wa michezo. Hii ndiyo dhana ya michezo shirikishi inayojenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; ikiwa na uwezo hata wa kuganga na kuponya madonda; kwa kujenga na kudumisha madaraja urafiki wa kijamii yanayowakutanisha watu. Huu ni ujumbe maalum sana kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanamichezo kutoka Vatican: “Athletica Vaticana” au “Vatican Athletics” wanaoendeleza mchakato wa kuishi michezo katika uhalisia wa maisha.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, ule mkutano uliokuwa umepangwa na baadaye ukahailishwa kutokana na kuibuka kwa janga la Virusi vya Corona, COVID-19 utaweza kufanyika mapema iwezekanavyo. Huu ni mkutano unaokishirikisha Kikosi cha Jeshi la Polisi kinachoshughulikia Uchumi na Fedha, Kikundi cha Majadiliano ya Kitamaduni “Cortile de Gentili” pamoja na Shirikisho la Wanamichezo Kutoka Mkoa wa Lazio “Fidal Lazio”. Baba Mtakatifu amesema kwamba, hivi karibuni, Kitengo cha Uchapaji cha Vatican, Libreria Editrice Vaticana, LEV, kimechapisha kitabu kinachokusanya mawazo yake kuhusu michezo. Baba Mtakatifu amewapongeza wote kwa sadaka na majitoleo yao na kwamba, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu wataweza kukimbia kwa pamoja: “We run together, Simul Currebant” kwa ajili udugu, utu na heshima ya binadamu.

Itakumbukwa kwamba, hapo awali, michezo hii ilikuwa imeandaliwa na Kardinali Gianfranco Ravasi Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni akishirikiana na wadau mbali mbali wa michezo nchini Italia. Lengo ni kuhamasisha utamaduni wa amani, upendo na mshikamano unaomwilishwa katika michezo. Na kwa njia ya michezo, wadau mbali mbali waweze kuimarisha utamaduni wa watu kukutana, kushirikiana na kushikamana kama sehemu ya mchakato wa majadiliano katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Fedha hii itawasaidia madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya ambao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa ni mashujaa walioko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, kiasi hata cha kuhatarisha usalama na maisha yao katika ujumla wake. Kristo Yesu alisema hakuna upendo mkubwa zaidi kuliko wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Makada katika sekta ya afya wamekuwa ni mashuhuda wa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yao, ambayo wanaendelea kuyafanya kwa weledi, uadilifu mkubwa na uwajibikaji katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Papa: Michezo 2020

 

 

05 September 2020, 15:07