Shirikisho la Vyama Huru Vya Wafanyakazi Nchini Poland "Solidarnosc linaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 40 tangu kuazishwa kwake mwaka 1980. Shirikisho la Vyama Huru Vya Wafanyakazi Nchini Poland "Solidarnosc linaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 40 tangu kuazishwa kwake mwaka 1980. 

Miaka 40 Ya Shirikisho la Vyama Huru Vya Wafanyakazi Poland

Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarność". Hili ni Shirikisho ambalo limeleta mabadiliko makubwa ya kihistoria nchini Poland na Ulaya ya Kati katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko amekazia zaidi umuhimu wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika mapambano dhidi ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarność" yaani “Mshikamano” hivi karibuni limeadhimisha kumbukumbu ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1980. Shirikisho hili limekuwa ni moto wa kuotea mbali katika mchakato wa kuleta mabadiliko ya kisiasa na kijamii ndani na nje ya Poland kiasi hata cha kushuhudia utawala wa Kikomunisti, ukikunja vilago na kutoweka nchini Poland. Ni Shirikisho ambalo linajipambanua kwa kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wafanyakazi nchini Poland kwa kuwaunganisha wale wote waliokuwa wananyanyaswa, ili waweze kuwa ni kitu kimoja. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, Jumatano tarehe 2 Septemba 2020 amewakumbusha watu wa Mungu kutoka Poland kuhusu Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarność".

Hili ni Shirikisho ambalo limeleta mabadiliko makubwa ya kihistoria nchini Poland na Ulaya ya Kati katika ujumla wake. Katika muktadha wa mshikamano kwa mwaka 2020, Baba Mtakatifu Francisko amekazia zaidi mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika mapambano dhidi ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kwamba, hakuna mshikamano wa kweli pasi na upendo. Wala hakuna furaha ya kweli kwa binadamu na taifa katika ujumla wake, ikiwa kama hakuna upendo wa dhati. Injili ya upendo katika muktadha huu ni huduma makini inayonafsishwa katika upendo kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kutoa kwa ukarimu. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa waaminifu kwenye mshikamano unaofumbatwa katika upendo wa dhati, ambao ni huduma makini kwa Mungu na jirani!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Desemba 2019 alikutana na viongozi wakuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarność" mjini Vatican. Aliwaambia kwamba,  changamoto kubwa kwa wakati huu ni ile ya kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu kati ya waja wake. Uwepo wa Mungu hufuatana na juhudi za dhati za mtu mmoja mmoja na za makundi ya watu kutafuta ari na maana katika maisha yao. Mwenyezi Mungu hukaa miongoni mwao, akihamasisha mshikamano, udugu, ustawi, ukweli na haki. Takribani miaka 40 iliyopita, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahimiza watu wa Mungu nchini Poland kutambua uwepo endelevu wa Mungu na hivyo kumwomba nguvu ya Roho Mtakatifu, ili aweze kushuka na hivyo kupyaisha uso wa dunia. Mshikamano wa upendo na wale wote wanaotafuta haki zao msingi unaomwilishwa katika maeneo ya kazi, elimu, mafungamano ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimataifa ni kielelezo makini cha waamini kujiweka wazi mbele ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko alisikitika kusema kwamba, neno “Mshikamano” limechakachuliwa kiasi cha kueleweka vibaya, lakini linataja kitu ambacho ni zaidi ya matendo machache ya ukarimu. Ikumbukwe kwamba, mshikamano kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mwitikio huria wanao utoa wale wanaotambua kwamba kazi ya kijamii ya mali na lengo lake la jumla la bidhaa ni mambo ya kiuhakika yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya mali binafsi. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea watu ambao wamepokwa: utu, heshima na haki zao msingi. Hawa ndio wale wanaofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, bila ya kupata ujira wa haki unaokidhi mahitaji yao msingi kwa ajili ya kuzitegemeza familia zao au kupata huduma bora ya afya au mapumziko. Katika majadiliano kati ya Dola pamoja na jamii, Kanisa halina suluisho kwa kila suala maalum. Lakini kwa kushirikishana na wadau mbali mbali katika jamii linaweza kupata majibu msingi ili kutetea utu wa binadamu, ustawi na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu aliwakumbusbha wajumbe hawa kwamba, kubadilisha miundo bila kujenga hoja na mitazamo mipya kutahakikisha tu kwamba mara moja au baadaye, miundo hiyo hiyo haitaweza kufua tena dafu na hata wakati mwingine kusababisha madhara makubwa zaidi. Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwaombea karama na mapaji ya Roho Mtakatifu viwasaidie wao kama watendaji wakuu pamoja na wafanyakazi wote Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarność", ili ari na mwamko huu uweze kupata chimbuko lake katika tunu msingi na kanuni za Injili yaani kuchukuliana mizigo na kuitimiza hiyo sheria ya Kristo. Na hatimaye, akawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Mari Mama wa Mungu na Malkia wa Poland, ili waendelee kudumu katika utekelezaji wa shughuli na utume wao.

Wafanyakazi Poland 2020
02 September 2020, 14:10