Tafuta

Tarehe 17 Septemba 2020 Baba Mtakatifu ameungana na Wakleri wa Lombardia kuadhimisha Siku ya VI ya Mapadre Wagonjwa na Wazee kwa kuwatumia ujumbe wa imani, matumaini na mapendo! Tarehe 17 Septemba 2020 Baba Mtakatifu ameungana na Wakleri wa Lombardia kuadhimisha Siku ya VI ya Mapadre Wagonjwa na Wazee kwa kuwatumia ujumbe wa imani, matumaini na mapendo! 

Papa: Siku VI ya Mapadre Wagonjwa na Wazee Lombardia!

Papa Francisko, tarehe 17 Septemba 2020 ameungana na wakleri kutoka Lombardia, Kaskazini mwa Italia katika maadhimisho ya Siku ya VI ya Mapadre Wazee na Wagonjwa. Huu ni ushuhuda wa udugu. Ni siku ya upendo na mshikamano katika sala na udugu wa kikuhani kama njia ya kuwaenzi Mapadre wazee na wagonjwa ambao wamejisadaka sana kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Maadhimisho ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Baba Mtakatifu Francisko aliwaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kila kukicha! Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani, kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu. Licha ya mambo yote hayo, Baba Mtakatifu anasema, Mapadre wanaendelea kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu katika barua hii anapenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre, wote wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha na utume wao!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 17 Septemba 2020 ameungana na wakleri kutoka Lombardia, Kaskazini mwa Italia katika maadhimisho ya Siku ya Sita ya Mapadre Wazee na Wagonjwa Kutoka Lombardia. Huu ni ushuhuda wa udugu unaopata chimbuko lake katika Daraja takatifu ya Upadre. Ni siku ya upendo na mshikamano katika sala na udugu wa Kikuhani kama njia ya kuwaenzi Mapadre wazee na wagonjwa ambao wamejisadaka sana kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Askofu mkuu Mario Delpini wa Jimbo kuu la Milano, ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa “Caravaggio”. Hili ni tukio ambalo limeandaliwa na UNITALSI Lombardia. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amewakumbusha Mapadre wazee na wagonjwa kwamba, hata kama kimwili wanaonekana kuwa ni dhaifu, lakini bado wanatekeleza dhamana na utume wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa: sala na sadaka yao; kwa kusikiliza pamoja na majitoleo ya mateso na mahangaiko yao kimwili, kama sadaka safi na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu kwa ajili ya majimbo yao.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawapongeza Mapadre wazee na ambao kwa sasa uzee huu unaandamana na magonjwa. Huu ni ushuhuda wa upendo mwaminifu kwa Mungu na kwa Kanisa. Ni kielelezo cha kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai katika hali ya ukimya; kumbukumbu hai na msingi thabiti wa ujenzi wa Kanisa la Kristo Yesu kwa siku za mbeleni. Baba Mtakatifu anawashukuru watu wote wa Mungu na kwa namna ya pekee UNITALSI Lombardia, yaani Umoja wa Kitaifa wa Wasafirishaji wa wagonjwa Lourdes na kwenye Madhabahu ya Kimataifa. UNITALSI ni juhudi zilizoanzishwa na kunako mwaka 1903 na Giovanni Battista Tomassi, wakati alipokuwa anakaribia kukata tamaa ya maisha kutokana na kuandamwa mno na magonjwa, aliamua kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Lourdes, Ufaransa, hapo ndipo alipoonja matendo makuu ya Mungu katika maisha yake. Kwa maombezi ya Bikira Maria wa Lourdes akaongoka na hivyo kufanikiwa kuguswa na kweli za maisha ya Kikristo.

Aliporudi nchini Italia, akaandika Katiba ya UNITALSI na huo ndio ukawa ni mwanzo wa UNITALSI kuanza kuenea kwa kasi ya ajabu nchini Italia. Hiki ni kielelezo makini cha ushuhuda wa imani tendaji katika matendo ya huruma yanayojionesha katika Parokia na Majimbo mengi nchini Italia. Baba Mtakatifu amegusia pia kuhusu adha ya kuwekwa karantini na kutopata fursa ya kukutana na kuzungumza na wapendwa wao na kwamba, woga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 umewakumbusha kuhusu udhaifu wa binadamu katika ujumla wake. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, watu wanatumia vyema rasilimali muda waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kufurahia nafasi ya kukutana na jirani na hatimaye, kuweza kuganga na kuponya “kirusi” cha kudhani kwamba, mtu peke yake anaweza kujitegemea na kujitosheleza. Katika kimya kikuu, watu wengi wamenyanyua nyuso zao kuelekea mbinguni. Kwa neema ya Mungu hii inaweza kuwa ni fursa ya utakaso hata kwa Mapadre. Hakuna sababu ya kuogopa mateso, kwani Kristo Yesu anaubeba Msalaba pamoja nao!

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaweka Wakleri wote chini ya ulinzi na tunza Bikira Maria, Mama wa Mapadre wote. Anawakumbuka na kuwaombea Mapadre waliofariki dunia kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na wale wote wanaoendelea kupata tiba katika vituo mbalimbali vya afya. Wote hawa, amewapatia baraka zake za kitume!

Mapadre Wagonjwa
17 September 2020, 14:47