Tarehe 15 Septemba, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Mateso. Tarehe 15 Septemba, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Mateso. 

Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Mateso, 15 Septemba

Papa Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, Bikira Maria alilia kwa uchungu mkubwa na moyo wake kujeruhiwa vibaya kutokana na mateso na kifo cha Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Leo hii, Bikira Maria anawaonesha huruma wote wanaoendelea kuteseka kutokana na umaskini sanjari na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na wakuu wa ulimwengu huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Septemba, siku moja baada ya kuadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba, linaadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria, Mama wa Mateso. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, Bikira Maria alilia kwa uchungu mkubwa na moyo wake kujeruhiwa vibaya kutokana na mateso na kifo cha Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Leo hii, Bikira Maria anawaonesha huruma wale wote wanaoendelea kuteseka kutokana na umaskini sanjari na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na wakuu wa ulimwengu huu. Bikira Maria Mama wa Mateso awe ni faraja kwa wale wanaoteseka; matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo na awe ni chemchemi ya huruma na mapendo kwa wenye huzuni na mahangaiko makubwa! Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Mateso anasema Mtakatifu Paulo VI katika Wosia wake wa Kitume “Marialis cultus” yaani “Ibada kwa Bikira Maria”, huu ni mwaliko kwa waamini kutafakari kile kipindi maalum katika historia ya ukombozi wa mwanadamu na hivyo kumheshimu Bikira Maria aliyeshiriki kwa namna ya pekee katika mateso ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, kiasi hata cha kudiriki kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya Mwanaye! Rej. Yn. 19: 25-27.

Umama wa Bikira Maria unachukua nafasi ya pekee pale Mlimani Kalvari, chini ya Msalaba. Itakumbukwa kwamba, Ibada ya Kumbukumbu kwa heshima ya Bikira Maria Mama wa Mateso iliandikwa kwenye Kalenda ya Kanisa Katoliki kunako mwaka 1814. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, waamini katika Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mateso wanayakumbuka mateso ambayo Bikira Maria aliyapitia katika maisha na utume wake. Kristo Yesu alipotolewa Hekaluni, Mzee Simeoni alitabiri kwamba, upanga utaingia moyoni mwa Bikira Maria, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi! Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu pamoja na Mtoto Yesu, walilazimika kukimbilia ugenini, huko Misri ili kusalimisha maisha ya Mtoto Yesu. Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu waliingiwa na wasi wasi na hofu kubwa, wakaanza kumtafuta Mtoto Yesu kwa muda wa siku tatu bila mafanikio na hatimaye, wakamkuta Yesu akiwa Hekaluni. Katika Njia ya Msalaba, Bikira Maria alikutana na Yesu, akamsindikiza hadi pale Mlimani Kalvari, chini ya Msalaba akashuhudia kifo chake! Wakamteremsha kutoka Msalabani na kumkabidhi Bikira Maria. Baada ya yote haya, Yesu akazikwa kaburini.

Kwa karne nyingi, waamini wamejenga na kukuza Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mateso. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Sala ya Malaika wa Bwana, daima anamkumbuka Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Huyu ni Mama aliyejisadaka na kujitoa kwa ajili ya wengine kama ilivyokuwa kwenye arusi ya Kana ya Galilaya, akakubali kuwa ni Mama wa wote. Bikira Maria katika maisha na utume wake, akawa ni mwanafunzi mwaminifu wa Kristo Yesu, akajifunza kutoka kwake, na kumsindikiza katika maisha na utume wake. Akawasindikiza wanawake wachamungu waliovutwa na huduma ya Kristo Yesu katika maisha yao! Kuna wakati, Bikira Maria na ndugu zake, walidhani kwamba, “Yesu alikuwa amechanganyikiwa” wakaenda kumwona, lakini hawakupata nafasi! Bikira Maria akamfuata Mwanae wa pekee, hadi kudiriki kusimama chini ya Msalaba na kushuhudia jinsi ambavyo walimnyanyasa na kumdharirisha Yesu! Lakini, akaendelea kuwa jasiri kama Mama na hatimaye, Kristo Yesu akiwa chini ya Msalaba, akamkabidhi kwa yule Mwanafunzi aliyempenda na tangu wakati huo, akawa ni Mama wa waamini wote. Ni Mama aliyeshirikiana na kushikamana na Mitume wa Yesu katika kusali!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria, aliendelea kuwa ni Mama na mwanafunzi hodari wa Kristo Yesu; mwaliko kwa waamini kumtafuta, ili kukimbilia ulinzi na tunza yake ya kimama. Maria ni Mama na Bikira, mfano hai wa utimilifu wa Kanisa. Hata Kanisa, kwa kuutazama utakatifu wa Bikira Maria, kwa kuiga upendo wake na kutimiza mapenzi ya Mungu, linakuwa pia ni Mama. Kwani kwa njia ya mahubiri na Sakramenti ya Ubatizo linazaa watoto waliotungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na hivyo kuzaliwa kwa Mungu, kwa uzima mpya usiokufa! Kanisa ni Mama wa wote, watakatifu na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu. Kumbu kumbu ya Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mateso iwe ni fursa kwa waamini kutafakari Fumbo la mateso katika maisha yao! Waguswe na mateso ya Bikira Maria katika maisha na utume wake, ili hatimaye, waweze kumtolea sifa na heshima kwa kukubali kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa.

Bikira Maria Mateso
15 September 2020, 15:05