Don Roberto Malgesini: Shuhuda wa Huruma na Upendo wa Mungu kwa Maskini Duniani, aliyeuwawa kikatili tarehe 15 Septemba 2020 na kuzikwa tarehe 19 Septemba 2020. Don Roberto Malgesini: Shuhuda wa Huruma na Upendo wa Mungu kwa Maskini Duniani, aliyeuwawa kikatili tarehe 15 Septemba 2020 na kuzikwa tarehe 19 Septemba 2020. 

Don R. Malgesini: Shuhuda wa Huruma ya Mungu Kwa Maskini!

Mara baada ya Misa Takatifu, Kardinali Konrad Krajewski amewasilisha salam za rambirambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye tangu aliposikia habari za mauaji haya ya kikatili amekuwa pamoja nao katika sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu anasema, kwa macho ya binadamu Don Roberto Malgesini amefariki dunia, lakini kamwe upendo, sadaka na majitoleo yake hayawezi kufutika .

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Don Roberto Malgesini alizaliwa kunako mwaka 1969 huko Morbegno, Kaskazini mwa Italia. Alipadrishwa kunako mwaka 1998. Alikuwa anafanya utume wake miongoni mwa maskini, wakimbizi na wahamiaji, Jimbo Katoliki la Como. Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Bikira Maria, Mama wa mateso, Jumanne tarehe 15 Septemba 2020 majira ya asubuhi alichomwa kisu na kufariki hapo hapo na mtu ambaye amejulikana kwa jina Ridha Mahmoudi mwenye umri wa miaka 53, aliyeingia nchini Italia kunako mwaka 1993 akitokea nchini Tunisia. Don Roberto Malgesini amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 51 tangu alipozaliwa. Watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Como wanamwita Don Roberto Malgesini “Martire della misericordia” yaani “Shuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini”.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 16 Septemba 2020 alimkumbuka na kumwombea, akisema kwamba, Don Roberto Malgesini ameuwawa na mgonjwa wa afya ya akili aliyekuwa anamhudumia. Baba Mtakatifu alitumia fursa hii kuungana na watu wa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Como kwa ajili ya kuomboleza msiba huu mzito. Kwa upande wake, Askofu Oscar Cantoni, katika utenzi wake wa maombolezo anasema, anamshukuru na kumrudishia Mwenyezi Mungu sifa na utukufu kwa ushuhuda wa kifodini cha Don Roberto Malgesini. Kwa hakika amekuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii. Ni Padre aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wala hakutamani kuwa na Parokia ya kuhudumia, bali kuwa kati pamoja na maskini, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu.

Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa, Jumamosi tarehe 19 Septemba 2020, amemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ibada ya mazishi ya Don Roberto Malgesini, iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Como na kuendeshwa na Askofu Oscar Cantoni. Ibada hii imefuatiliwa na maelfu ya maskini, wakimbizi na wahamiaji, walionja huruma na upendo wa Don Roberto Malgesini enzi ya uhai wake. Mara baada ya Misa Takatifu, Kardinali Konrad Krajewski amewasilisha salam za rambirambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye tangu aliposikia habari za mauaji haya ya kikatili amekuwa pamoja nao katika sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu anasema, kwa macho ya binadamu Don Roberto Malgesini amefariki dunia, lakini kamwe upendo, sadaka na majitoleo yake hayawezi kufutika hata kidogo.

Huu ni ukurasa wa Injili unaosema, “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” Yn. 15:13. Sehemu hii ya Injili inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wafuasi wa Kristo Yesu. Katika maisha na utume wake, Don Roberto Malgesini, alinafsisha ile Sala kuu ya Baba Yetu Uliye mbinguni, kwa kujitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, ili kulitukuza Jina la Mungu na Ufalme wake, uje hapa duniani. Hii ni changamoto na mwaliko kwa Mapadre kuhakikisha kwamba, wanaiishi Injili kikamilifu, kama wanavyohimiza Mwenyeheri Kardinali Newman na Mama Theresa wa Calcutta. Waliwahimiza watu wa Mungu kueneza ukuu wa Kristo Yesu kwa njia ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli maisha yao, yaweze kuwa ni mng’ao angavu wa Kristo Yesu, ili hatimaye, watu waonje uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yao, ili wanapoinua nyuso zao, wamwone Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko unaowasukuma kutoa ushuhuda kwa njia ya mifano halisi ya maisha yao, ili kweli watu wa Mungu waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Damu na ushuhuda wa Don Roberto Malgesini ni chachu ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa maskini!

Mauaji ya Padre
19 September 2020, 16:02