Tafuta

Mkutano wa Urafiki kati ya watu nchini Italia huko Rimini kwa mwaka 2020 Unaongozwa na kauli mbiu: "Bila mshangao, tutabaki viziwi kwa mambo adhimu." Mkutano wa Urafiki kati ya watu nchini Italia huko Rimini kwa mwaka 2020 Unaongozwa na kauli mbiu: "Bila mshangao, tutabaki viziwi kwa mambo adhimu." 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Mkutano wa Rimini 2020: COVID-19

Mkutano wa Rimini 2020: Ujumbe: Ugonjwa wa COVID-19 na mshangao wake kwa watu wa Mataifa. Maana ya: maisha, mateso, kifo na uzuri wa Injili. Waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa imani inayokita mizizi yake katika uzuri wa Injili na uzuri wa Mwenyezi Mungu ambayo umefunuliwa kwa njia ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, yaani Kristo Yesu. Changamoto za COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini: “Meeting per l’amicizia fra i popoli” unaofanyika kila mwaka sasa umeingia katika awamu yake XLI, yaani Mwaka wa 41. Mkutano huu kuanzia tarehe 18 -23 Agosti 2020, unaongozwa na kauli mbiu: “Bila mshangao, tutabaki viziwi kwa mambo adhimu”. Huu ni mkutano unaopembua pamoja na mambo mengine, changamoto zinazoendelea kujitokeza baada ya janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kumbe, huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale watu waliovunjika na kupondeka moyo, kwa kubainisha sera na mikakati ya uchumi fungamani. Gonjwa la Corona, COVID-19 limesababisha utengano mkubwa, changamoto na mwaliko wa kuweza kujenga jamii inayosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Siasa inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu kitaifa na hata katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

Kwa kuzingatia itifaki dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 mkutano huu unafanyika kwa kutumia mitandao ya kijamii. Kati ya wawezeshaji wakuu kwenye mkutano wa Rimini ni Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Demokrasia na ushirikiano wa kimataifa; elimu, sanaa na fasihi simulizi sanjari na ushuhuda wa wadau mbali mbali ni mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha kwanza. Mkutano huu unafanyika wakati Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na changamoto kubwa za kijamii, kiuchumi na kiafya, ambazo zinaendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu na vipaumbele vyao ambavyo vimebadilika sana. Mageuzi ya sera na mikakati ya uchumi Barani Ulaya; umuhimu wa maisha ya kidini na kitamaduni kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, ili kuangalia ni wapi mahali pa kuanzia, ili kuwajengea watu Injili ya imani na matumaini, baada ya athari kubwa ambazo zimesababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Haya pia yanapewa umuhimu wa pekee katika kujenga na kudumisha mafungamano kati ya watu wa Mataifa.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Francesco Lambiasi wa Jimbo Katoliki la Rimini, Italia, kwa kuonesha uwepo wake wa karibu na sala anapenda kugusia yafuatayo: Ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 na mshangao wake kwa watu wa Mataifa. Maana ya: maisha, mateso, kifo na uzuri wa Injili. Waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa imani inayokita mizizi yake katika uzuri wa Injili na uzuri wa Mwenyezi Mungu ambayo umefunuliwa kwa njia ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, yaani Kristo Yesu.  Uzoefu na mang’amuzi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 umedhihirisha udhaifu wa mwanadamu sanjari na ukosefu wa uhakika wa usalama. Mwanadamu amejikuta yuko mbali kabisa na agenda, miradi, mazoea na vipaumbele vyake, kiasi hata cha kujikuta akiwa amesinzia. Kauli mbiu ya maadhimisho haya anasema Baba Mtakatifu Francisko “Bila mshangao, tutabaki viziwi kwa mambo adhimu” ina umuhimu wake katika kipindi hiki cha historia ya maisha ya mwanadamu, wakati wa kutafuta mafao ya wengi, si kwa kutegemea nguvu za mtu binafsi, bali kwa kumshangao mkubwa kama ilivyo kwa watoto wadogo, ni wakati wa kuangalia ukweli kwa macho ya mshangao kama ilivyo kwa mtoto mchanga.

Kristo Yesu, anawataka wafuasi wake wajifunze fadhila ya unyenyekevu kwa kuendelea kujikita katika kipaji cha kushangaa, kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo daima inampatia mwamini nafasi ya kuanza tena katika mazingira mbali mbali. Maisha bila mshangao yanageuka kuwa ni mambo ya kawaida. Hata imani bila mshangao inakuwa ni jambo la kawaida tu! Mama Kanisa pia anapaswa kupyaishwa, ili aendelee kuwa ni makazi ya Mungu aliye hai, Mchumba wa Kristo, na Mama anayezaa watoto. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika miezi ya hivi karibuni, watu wengi wameshikwa na mshangao ambayo umefumbatwa katika huruma kutokana na uwepo wa mateso makubwa ambayo yameonesha udhaifu wa binadamu. Huruma hii imewasukuma madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya kujitoa bila ya kujibakiza ili kuweza kukabiliana na changamoto kubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni changamoto hii, iliyowawezesha waalimu na wanafunzi kujisadaka ili kuhakikisha kwamba, masomo yanaendelea kwa njia ya mitandao ya kijamii na hatimaye, wanafunzi wakaweza kumaliza mwaka wa masomo salama salimini. Kuna baadhi ya watu wamefanikiwa kuona nyuso za ndugu na jamaa zao, kiasi cha kupata ari na mwamko mpya wa kuendelea kukabiliana na changamoto ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, kauli mbiu “Bila mshangao, tutabaki viziwi kwa mambo adhimu” ni changamoto na mwaliko wa watu kuzama katika undani wa maisha yao, ili hatimaye, kumgundua Mwenyezi Mungu anayewapenda kwa dhati na huu ndio msingi mambo yote kabisa. Zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu ni kipaji cha kushangaa, ambacho kina uwezo wa kutambua mambo. Hisia zinapita, na mshangao peke yake ndio unaobaki. Mshangao ni kipaji kinachopaswa kuendelezwa, ili hatimaye, mtu kuweza kugundua maana halisi ya maisha, mateso na kifo. Bila uelewa huu sahihi, maisha yasingelikuwa na maana yoyote. Kuna mamilioni ya watu ambao wamejitaabisha sana kutafuta maana ya maisha. Watu wengi wakajikuta wakiwa wamewekwa karantini, kiasi cha kushindwa kushangaa tena. Kipindi hiki cha watu kuwekwa karantini, wengi wakagundua ndani mwao tena maana na umuhimu wa maisha na hivyo kuchanua tena kama maua ya kondeni! Bila kipaji cha kushangaa, wengi wangeli baki wakiwa viziwi. Wasanii wamewawezesha watu kugundua maana ya uzuri na kwamba, bila uzuri wa Injili ni vigumu sana kuweza kufahamu ukweli wenye mvuto na unaotaka kufikia ukamilifu wake.

Mbele ya uzuri mwanadamu anabaki akiwa amepigwa bumbuwazi na kwamba, ubaya tena hauna mvuto kwake. Bila ya kung’amua uzuri, ukweli uko mashakani. Hii ni changamoto pevu kwa Wakristo ili kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika nguvu ya uzuri wake; mvuto kutoka kwa Yesu, kama ambavyo alizoea kusema, Mtumishi wa Mungu Luigi Giussani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kila muundo wa katekesi ungefanya vyema kushughulikia “njia ya uzuri” (via pulchritudinis). Kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kunaonesha kwamba kumwamini na kumfuata siyo tu jambo sahihi na la kweli, bali pia ni jambo zuri, lenye uwezo wa kuyajaza maisha kwa mwangaza mpya na furaha kuu, hata katikati ya matatizo. Kwa hiyo kila namna ya kudhihirisha uzuri wa kweli inaweza kutambuliwa kama njia inayoelekea kwenye kukutana na Kristo Yesu. Kama asemavyo Mtakatifu Augostino Mwana mwilika, kama ufunuo wa uzuri usiopimika, anapendeka kabisa na anawavuta kwake kwa viunganishi vya upendo. Kwa hiyo malezi katika “njia ya uzuri” (via pulchritudinis) yanapaswa kuwa ni sehemu ya juhudi ya waamini kurithisha imani kwa wengine. Rej. Eg. Namba 167.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kushirikiana na kushikamana na Kristo Yesu ili kutangaza na kushuhudia uzuri wa Mwenyezi Mungu, aliyefanyika Mwili na kukaa kati ya waja wake, ili macho ya waamini yaweze kuiona Sura yake na macho yaweze kushangaa kuhusu uwezo wa kuishi. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, ni afadhali kuwa binadamu kwa sababu Kristo Yesu amekuwa ni binadamu. Utu na heshima ya binadamu ndio ugunduzi mkubwa ambao Wakristo wanaweza kuwashirikisha jirani zao kama kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya matumaini. Huu ni mwaliko wa kuwa wakweli na wa wazi mbele ya uzuri, ambao umewabadilishia maisha na kuwashuhudia upendo wa Mungu unao okoa, hasa zaidi kwa watu wanaoteseka. Huu ndio ujumbe ambao Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwashirikisha wajumbe kwenye Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini: “Meeting per l’amicizia fra i popoli” unaofanyika kila mwaka sasa umeingia katika awamu yake XLI, yaani Mwaka wa 41. Kuanzia tarehe 18 -23 Agosti 2020, unaongozwa na kauli mbiu: “Bila mshangao, tutabaki viziwi kwa mambo adhimu”.

Papa: Rimini 2020

 

 

 

18 August 2020, 13:40