Kanisa Katoliki nchini Brazil kuanzia tarehe 16-22 Agosti 2020 linaadhimisha Juma la Kwanza la Watawa Nchini Brazil. Kanisa Katoliki nchini Brazil kuanzia tarehe 16-22 Agosti 2020 linaadhimisha Juma la Kwanza la Watawa Nchini Brazil. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Juma La Kwanza la Watawa Brazil

Ikiwa kama Kristo Yesu ndiye mpendwa wao pekee katika maisha, watawa wataweza kukirimiwa nguvu ya kuwapenda watu wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao katika ukweli na huruma. Kwa sababu watakuwa wamejifunza kutoka kwa Yesu maana na jinsi ya kumwilisha upendo halisi katika maisha. Watawa wataweza kupenda kwa dhati, kwa sababu wanapendwa upeo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Agosti 2020, alitambua uwepo wa kundi kubwa la watawa kutoka nchini Brazil. Hawa ni watawa licha ya kuwa mbali na nchi yao anasema Baba Mtakatifu Francisko wanaendelea kuunganika na ndugu zao kiroho, wanapoadhimisha Juma la Kwanza la Maisha ya Kitawa Nchini Brazil kuanzia tarehe 16-22 Agosti 2020. Baba Mtakatifu katika barua aliyomwandikia Sr. Maria Ines Vieira Ribeiro, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Brazil kwa niaba ya watawa wote nchini Brazil, amewataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa sala. Baba Mtakatifu amekumbushia swali msingi alilowauliza watawa wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, ulioadhimisha kuanzia Mwaka 2014 hadi mwaka 2015.

Baba Mtakatifu anawahamasisha watawa kuendeleza maisha na utume wao kwa kujikita zaidi katika mchakato wa upyaishaji wa maisha na utume wa watawa nchini Brazil. Anawataka kwa mara nyingine tena, kujiuliza swali msingi, Je, Kristo Yesu ndiye mpendwa wao wa kwanza na wapekee katika maisha yao, kama walivyoahidi walipokuwa wanaweka nadhiri zao mbele ya watu wa Mungu? Ikiwa kama Kristo Yesu ndiye mpendwa wao pekee katika maisha, wataweza kukirimiwa nguvu ya kuwapenda watu wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao katika ukweli na huruma. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, watakuwa wamejifunza kutoka kwa Kristo Yesu maana na jinsi ya kumwilisha upendo halisi katika maisha. Watawa wataweza kupenda kwa dhati, kwa sababu ndani mwao wamekwisha kuonja upendo unaobubujika kutoka kwenye Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha watawa kwamba, kila wito una chanzo na asili yake, kwa kutambua na kung’amua kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda waja wake. Kwa upande mwingine, kuna changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Baba Mtakatifu anawataka watawa kuwa macho na makini, ili wasiteleze na hatimaye kutumbukia katika malimwengu, yatakayowaziba macho na hivyo kushindwa kuona neema ya Mungu, ambaye ndiye mhusika mkuu katika maisha na anaye waongoza kusimama kidete katika upendo wao bila “kupepesapepesa macho kutafuta upendo mbadala”. Msingi thabiti na imara katika maisha ya watawa, ili wasiyumbishwe kama “dala dala iliyokatika usukani” ni kutoa kipaumbele cha kwanza katika sala, licha ya shughuli na utume mbali mbali wanaopaswa kuutekeleza. Wawe na ujasiri wa kumtaza Kristo Yesu, ili waweze kujifunza kuishi na kuhudumia kwa kutambua kwamba, wao wanayo thamani kubwa machoni pa Mwenyezi Mungu anayewapenda upeo!

Watawa Brazil
18 August 2020, 13:12