Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje huko Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 1-6 Agosti 2020 Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje huko Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 1-6 Agosti 2020 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya Vijana Kimataifa 2020

Baba Mtakatifu anakazia: Umuhimu wa vijana kukutana na Kristo Yesu katika Neno, Ibada na Sakramenti za Kanisa. Wasiogope kwa sababu Kristo Yesu anaishi na anawataka hata vijana nao kuishi. Wajenge utamaduni wa sala na tafakari katika maisha yao na Bikira Maria, awe ni mfano bora wa kuigwa. Ujumbe huu unachota utajiri wa Wosia wake wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe Mosi, Agosti hadi tarehe 6 Agosti 2020, Sherehe ya Kung’ara Bwana, yanapambwa na kauli mbiu “Njoni, nanyi mtaona.” Yoh. 1:39. Maadhimisho haya yanatajirishwa kwa Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi pamoja na maadhimisho ya Misa Takatifu zinazoongozwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa. Sakramenti ya Upatanisho, ni mahali muafaka pa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani. Kuna katekesi makini kama sehemu ya majiundo endelevu ya vijana wa kizazi kipya, utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi kuhusu utume wa vijana. Hiki ni kipindi cha shuhuda mbali mbali za maisha na utume wa vijana katika kukabiliana na changamoto mamboleo kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa vijana kukutana, tayari kuandamana kwa pamoja, ili kukutana na Kristo Yesu anayewaalika, kushinda pamoja naye kama ilivyokuwa kwa wale Mitume wa kwanza, waliotikia wito wake alipowaambia “Njoni, nanyi mtaona.” Yoh. 1:39.

Maadhimisho haya yamezinduliwa na Askofu mkuu Luigi Pezzuto, Balozi wa Vatican nchini Bosnia na Herzegovina aliyewakabidhi vijana ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Mwaka 2020. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa vijana kukutana na Kristo Yesu katika Neno, Ibada na Sakramenti za Kanisa. Wasiogope kwa sababu Kristo Yesu anaishi na anawataka hata vijana nao kuishi. Wajenge utamaduni wa sala na tafakari katika maisha yao na Bikira Maria, awe ni mfano na kiongozi wao wa maisha katika kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Ujumbe wa Baba Mtakatifu unachota utajiri wake kutoka kwenye Wosia wake wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi.” Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Mitume wa kwanza waliokubali na kuitikia wito wake, walikwenda wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile.

Uzoefu na mang’amuzi yao kama Mitume, uliacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo zao kiasi hata cha kukumbuka muda ule: “Nayo ilikuwa yapata saa kumi” Yoh. 1:39. Wale Mitume wa kwanza, wakashirikishana Habari Njema, kiasi kwamba, Andrea nduguye Simon Petro akampeleka kwa Yesu. Naye Kristo Yesu akamtazama na kumpatia jina jipya akisema, “Wewe u Simon, mwana wa Yohane; nawe utaitwa Kefa maana yake Petro au Jiwe na tangu siku hiyo, Simon akajulikana kama Petro. Baba Mtakatifu Francisko anawaambia vijana kwamba, kwa kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao, wanabadilika na kuwa watu wapya zaidi, kwa kupewa utume wanaopaswa kuwashirikisha majirani zao, daima wakimwangalia Kristo Yesu kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao. Huu ni mwaliko wa kuacha yote na kuanza kumfuata Yesu katika maisha, tayari kushiriki maisha ya Yesu, huku wakiwa wamejazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Vijana lazima wajizatiti kukutana na kuishi na Kristo Yesu katika maisha yao, kwa njia ya sala, pamoja na kujiaminisha kwake, kwa sababu anautambua moyo wa binadamu. 

“Njoni, nanyi mtaona.” Yoh. 1:39 anasema Baba Mtakatifu ni ujumbe hata kwa vijana wa kizazi kipya, kwani Kristo Yesu anataka kugusa undani wa maisha yao ya kiroho na hivyo kuwawezesha vijana kutambua maana ya maisha. Vijana wawe tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, aliyekubali mpango wa Mungu kwa kusema “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Lk. 1:38. Hata vijana katika uhuru wao kamili wanapaswa kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Bikira Maria ni mlinzi na mwanga wa matumaini kwa watoto. Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, mwanga wa matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kamwe hautaweza kuzimika, ikiwa kama vijana watajiaminisha katika ulinzi na tunza yake ya kimama. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kuweza kutambua mateso na mahangaiko ya jirani zao. Wawe tayari kuongozwa na Roho Mtakatifu, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Maadhimisho ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina yaliasisiwa na Padre Slavko Barbaric aliyewakusanya vijana ili kuwafundisha katekesi kuhusu Ibada na Tasaufi ya Bikira Maria; kwa namna ya pekee akikazia umuhimu wa upyaisho wa maisha ya Kikristo, ili kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika utu mpya katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Ili kuweza kufikia hatua hii ya maisha, vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kutakasa dhamiri zao, ili waweze kuwa tayari kupokea ujumbe wa Kristo Yesu katika maisha yao; ujumbe wa Injili, kimsingi unahitaji kutua nanga katika akili na moyo uliotulia, tayari kusubiri kwa ari na moyo mkuu siku ile Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Kristo Yesu ni: Njia, Ukweli na Uzima. Kardinali Vinko Puljić, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vrhbosna ndiye aliyepewa dhamana ya kufunga Siku ya 31 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina.

Vijana 2020
04 August 2020, 13:53