Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni ni kielelezo cha hatima ya maisha ya mwanadamu: Utu, heshima na haki zake msingi Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni ni kielelezo cha hatima ya maisha ya mwanadamu: Utu, heshima na haki zake msingi 

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili Na Roho! Utu!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Kupalizwa Bikira Mbinguni Mwili na Roho, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba neema ya unyenyekevu kama alivyokuwa Bikira Maria, Mtumishi wa Bwana. Lengo ni kumwezesha Mwenyezi Mungu kutenda matendo makuu katika maisha ya waja wake kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Utu wa mtu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 12 Agosti 2020, amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, tarehe 15 Agosti 2020, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, mwili na roho. Sherehe hii ni ufunuo wa utu na heshima ambayo binadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba neema ya unyenyekevu kama alivyokuwa Bikira Maria, Mtumishi wa Bwana. Lengo ni kumpa Mwenyezi Mungu nafasi ya kutenda matendo makuu katika maisha ya waja wake kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Katika Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, mwili na roho, anawafundisha watu wa Mungu kumwadhimisha Mungu kwa sababu amewatendea mambo makuu. Bikira Maria anawaalika watu kumwadhimisha Mungu kutokana na ukuu, uzuri na wema wake katika maisha yake. Waamini wanahamasishwa katika maisha, kuhakikisha kwamba, wanatafuta mambo makuu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha yao kwani Yeye peke yake ndiye aliye mkuu vinginevyo, wanaweza kujikuta wakiwa wanazama katika mambo madogo madogo ya maisha.

Haya ni mambo ambayo wakati mwingine hayana mvuto wala mashiko! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna watu wamezama hadi kutopea huko waliko kwa kuwa na mamuzi mbele, kinyongo, wivu, uadui na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, uchu wa mali na madaraka. Haya yote yanawaonesha watu waliovaa ngozi ya Kondoo, lakini ukweli wa mambo, watu hawa ni sawa na “mbwa mwitu wakali”. Huu ndio unafiki unaofichika katika maisha ya watu wengi. Katika Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuinua uso wao, tayari kuangalia “mambo makuu” ambayo Mwenyezi Mungu amemtendea katika maisha. Baba Mtakatifu katika tafakari yake anaendelea kufafanua kwamba, wakati huu Mama Kanisa ana mwadhimisha Mwenyezi Mungu kwa kumpaliza Bikira Maria mbinguni, mwili na roho. Mwenyezi Mungu ameutaza unyonge wa mjakazi wake na kumwezesha kuwa wa kwanza kutunukiwa utukufu. Bikira Maria, kiumbe kama viumbe wengine, anapalizwa mbinguni mwili na roho.

Huko mbinguni aliko, Bikira Maria, yuko kama Mama mzazi anayesubiri watoto wake warejee nyumbani kwao. Waamini wanakumbushwa kwamba, huku bondeni kwenye machozi, ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu, wako njiani kuelekea nyumbani kwa Baba milele. Kwa njia ya Bikira Maria, waamini wanaweza kuona hatima ya maisha yao. Hili ni tukio muhimu sana la imani kwani ndani mwake, waamini wanamwona Bikira Maria aliye palizwa mbinguni, mwili na roho. Huyu ndiye yule Mama aliyethubutu kushiriki katika Fumbo la Pasaka na sasa anashiriki pia utukufu wa Mwanaye mpendwa, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Bikira Maria, Mama wa Mkombozi, ndiye Eva mpya na Kristo Yesu ni Adamu Mpya; kielelezo makini cha faraja na matumaini kwa wasafiri ambao bado wako huku bondeni kwenye machozi. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kwa ajili ya watu wote wa Mungu, lakini zaidi ni faraja kwa wale wanaoteseka; watu wanaohuzunika kiasi cha kupondeka moyo na hawana tena nguvu ya kuweza kunyanyua uso wao kwa matumaini.

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuondoa wasi wasi na hofu nyoyoni mwao na wala tena hakuna umbali unaoweza kuwatenga kwani mbinguni kuna Mama Bikira Maria anayewasubiri kwa mikono miwili. Huyu ndiye Bikira Maria, Malkia wa mbingu na Mama wa wote. Kwa hakika anawapenda sana watoto wake, anataka kuwafurahisha na kuwaokoa kwa haraka, kwani anatawakia mema kama ilivyo kwa kila mama. Waamini watambue kwamba, wanayo thamani kubwa machoni pa Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya furaha, changamoto na mwaliko kwa waamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria; waendelee kuvutwa na uzuri wake na kamwe wasikubali kutiwa giza na mambo mpito, bali wawe tayari kuthubutu kuambata mambo makuu ya mbinguni. Bikira Maria ni Mlango wa mbingu, awasaidie, kuangalia kwa furaha na matumaini huko juu mbinguni, mahali ambapo kuna makazi yao halisi.

Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe, kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos”. Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho  kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae”.

Mwili wa Bikira Maria uliokuwa umekingwa na dhambi ya asili, ukapalizwa mbinguni. Hiki ni kielelezo makini cha imani ya watu wa Mungu kama alivyokiri Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997. Kwa mwanga na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, akiwa ameungana na Maaskofu wenzake, Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni sehemu ya Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki. Bikira Maria tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anatukumbusha kwamba, maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria yanakwenda sanjari na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Bikira Maria, Mama wa Mungu kwa upendeleo na neema ya Mungu akabahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na hivyo kushirikishwa kwa namna ya pekee kabisa katika Fumbo la Pasaka na utukufu wa Kristo Yesu.

Hili ni Fumbo linaloonesha historia ya ubinadamu, matumaini ya watu wa Mungu na Kanisa katika ujumla wake. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho, anaendelea kuliombea Kanisa ambalo bado liko safarini, ili liweze kupata neema ya uzima wa milele. Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama anaendelea kuwasindikiza watoto wa Kanisa ambao wako bondeni huku kwenye machozi, ili siku moja, waweze kufika mbinguni na kufurahia maisha na uzima wa milele. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni inakita mizizi yake katika imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha ushindi wa nguvu ya upendo wa Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni mwaliko kwa watoto wa Kanisa kulitafakari Fumbo hili la imani kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kumwokoa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kristo Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa, akafufuka amepaa na mwili wake wa utukufu, hatima ya maisha ya waamini wote. Kumbe hapa duniani, watu wajibidiishe kumtumikia Mungu: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni kutokana na nguvu za Kimungu zilizokuwa zikitenda kazi ndani mwake. Bikira Maria amepalizwa mbinguni kwa mastahili ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Mama Kanisa anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika watoto wake wote waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia kuimarisha imani yao kwa nguvu ya upendo wa Mungu pamoja na kutambua kwamba, miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Papa: Bikira Maria
12 August 2020, 14:26