Bikira Maria Aliyepalizwa mbinguni mwili na roho ni faraja na matumaini ya watu wa Mungu, huku bondeni kwenye machozi. Bikira Maria Aliyepalizwa mbinguni mwili na roho ni faraja na matumaini ya watu wa Mungu, huku bondeni kwenye machozi. 

Bikira Maria Aliyepalizwa Mbinguni: Faraja na Matumaini ya Watu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 15 Agosti 2020, Mama Kanisa ameadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, hatua kubwa sana katika maisha ya mwanadamu. Bikira Maria ameingia mbinguni mwili na roho. Hatua hii ndogo iliyopigwa na Bikira Maria, lakini kwa sasa imekuwa ni kielelezo cha mafanikio makubwa katika maisha ya mwanadamu! Matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 20 Julai 1969, Apollo 11, ikiwa imewabeba wanasayansi wa anga za juu akina Neil Armstrong na Edwin Aldrin, walipokanyaga mwezini kwa mara ya kwanza na tukio hili likatafsiriwa kuwa ni “hatua ndogo lakini yenye mafanikio makubwa kwa binadamu”. Kwa hakika kabisa, binadamu alikuwa amepiga hatua kubwa sana ya maendeleo kihistoria. Lakini, tarehe 15 Agosti 2020, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, hatua kubwa sana katika maisha ya mwanadamu. Bikira Maria ameingia mbinguni mwili na roho. Hatua hii ndogo iliyopigwa na Bikira Maria kwa sasa imekuwa ni kielelezo cha mafanikio makubwa katika maisha ya mwanadamu. Halijalishi hata kidogo kwamba, binadamu anaweza kujimwambafai na kwenda hadi mwezini, ikiwa kama hapa duniani, watu wanashindwa kuishi kama jirani wema, huku wakipendana na kushikamana kama ndugu wamoja. Kupalizwa kwa Bikira Maria Mbinguni mwili na roho ni chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu kwamba, baada ya kifo, kuna ufufuko na maisha ya uzima wa milele.

Hii ni sehemu ya tafakari ya kina iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 15 Agosti 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa hakika, Mwenyezi Mungu hataiacha miili ya waja wake ione uharibifu. Kwa njia ya Bikira Maria, lengo la maisha ya mwanadamu limeweza kufikiwa na kwamba, waamini wanayo kila sababu ya kujizatiti kikamilifu katika hija ya maisha yao, huku wakiwa “wametia nia ya kwenda mbinguni” si kwa ajili ya kupata ushindi kwa mambo ya kidunia, bali maisha ya uzima wa milele. Bikira Maria ni nyota angavu inayowaongoza waamini kwenda mbinguni. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Bikira Maria, Mama wa Yesu, akiwa amekwisha tukuzwa mbinguni mwili na roho, ni sura ya mwanzo wa Kanisa ambalo litapata utimilifu wake katika ulimwengu ujao. Kadhalika anang’aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na ya faraja kwa taifa la Mungu lililo safarini, mpaka siku ya Bwana itakapokuja. Rej. LG. 68.

Mwinjili Luka, anamweka Bikira Maria mbele ya macho ya waamini, akiwa anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani “Magnificat” kwa kusema, “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana na roho yangu imemfurahia Mungu mwokozi wangu”. Maana yake ni kwamba, Mwenyezi Mungu amemkuza mja wake, licha ya matatizo, fursa na changamoto mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu aliweza kumkirimia katika maisha. Hii ni changamoto kwa waamini kutojikatia tamaa hata kidogo wanapokumbana na matatizo pamoja na changamoto za maisha. Mwenyezi Mungu apewe sifa na ukuu wake, kwa sababu Mungu ndiye chemchemi ya furaha ya kweli kutokana na uwepo wake wake wa daima. Mwenyezi Mungu yuko karibu na daima yuko tayari kuwashika mkono na kuwasaidia waja wake, kwa sababu udhaifu wa Mungu unajionesha kwa namna ya pekee katika upendo wake wa dhati. Mwenyezi Mungu anawaangalia waja wake na anawapenda wadogo na wanyenyekevu wa moyo kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Mwenyezi Mungu alimtendea makuu Bikira Maria kwa kumjalia zawadi ya maisha, Neno wa Mungu aliyetungwa mimba tumboni mwake.

Yeye ambaye ni bikira, anapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kama ilivyokuwa hata kwa binadamu yake Elizabeth katika uzee wake, yeye aliyeitwa tasa, Mwenyezi Mungu amemtendea mambo makuu kwa kupata mimba na alikuwa anasubiri mtoto wake aweze kuzaliwa! Hawa ni watu ambao hawakuyaamini macho yao, lakini wakathubutu kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi katika maisha yao. Naye akawaonesha upendo na huruma yake ya daima. Ndiyo maana Bikira Maria anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na utukufu! Baba Mtakatifu anawauliza waamini ikiwa kama katika maisha yao, wamejenga utamaduni wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya uhai, msamaha na upendo? Waamini wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kujijengea utamaduni wa kushukuru kama chemchemi ya furaha ya ndani kwa kusema, Asante Mungu wangu!

Itakumbukwa kwamba, Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe, kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos”. Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho  kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae”.

Mwili wa Bikira Maria uliokuwa umekingwa na dhambi ya asili, ukapalizwa mbinguni. Hiki ni kielelezo makini cha imani ya watu wa Mungu kama alivyokiri Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997. Kwa mwanga na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, akiwa ameungana na Maaskofu wenzake, Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni sehemu ya Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki. Bikira Maria tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anatukumbusha kwamba, maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria yanakwenda sanjari na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Bikira Maria, Mama wa Mungu kwa upendeleo na neema ya Mungu akabahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na hivyo kushirikishwa kwa namna ya pekee kabisa katika Fumbo la Pasaka na utukufu wa Kristo Yesu.

Hili ni Fumbo linaloonesha historia ya ubinadamu, matumaini ya watu wa Mungu na Kanisa katika ujumla wake. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho, anaendelea kuliombea Kanisa ambalo bado liko safarini, ili liweze kupata neema ya uzima wa milele. Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama anaendelea kuwasindikiza watoto wa Kanisa ambao wako bondeni huku kwenye machozi, ili siku moja, waweze kufika mbinguni na kufurahia maisha na uzima wa milele. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni inakita mizizi yake katika imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha ushindi wa nguvu ya upendo wa Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni mwaliko kwa watoto wa Kanisa kulitafakari Fumbo hili la imani kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kumwokoa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kristo Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa, akafufuka amepaa na mwili wake wa utukufu, hatima ya maisha ya waamini wote. Kumbe hapa duniani, watu wajibidiishe kumtumikia Mungu: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni kutokana na nguvu za Kimungu zilizokuwa zikitenda kazi ndani mwake. Bikira Maria amepalizwa mbinguni kwa mastahili ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Mama Kanisa anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika watoto wake wote waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia kuimarisha imani yao kwa nguvu ya upendo wa Mungu pamoja na kutambua kwamba, miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Papa: Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni

 

15 August 2020, 14:49