Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kinyama na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa huko nchini Nigeria. Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kinyama na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa huko nchini Nigeria. 

Papa Francisko Asikitishwa Na Vitendo Vya Kigaidi Nchini Nigeria

Baba Mtakatifu Francisko anawaombea wananchi wanaoshambuliwa na magaidi huko Kaskazini Mashariki wa Nigeria. Mashambulizi na vitendo vya kigaidi, vinatishia usalama, amani, ustawi, maendeleo, mafungamano na umoja wa Kitaifa. Hivi karibuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilisikitishwa sana na mauaji ya kinyama yaliyofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, Jumamosi tarehe 15 Agosti 2020, amejielekeza huko nchini Nigeria, ili kuweza kuwaombea, watu wanaoendelea kushambuliwa na magaidi huko Kaskazini Mashariki wa Nigeria. Mashambulizi na vitendo vya kigaidi, vinatishia usalama, amani, ustawi, maendeleo, mafungamano na umoja wa Kitaifa. Hivi karibuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilisikitishwa sana na mauaji ya kinyama yaliyofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, na kuitaka Serikali ya Nigeria, kuhakikisha kwamba, inawatia “pingu” wahusika na hatimaye, kuwafikisha kwenye vyombo vya haki, ili kujibu tuhuma zinazowakabili. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakiri kwamba, vitendo vya kigaidi katika mifumo yake mbali mbali ni hatari sana kwa amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, magaidi, wanaoratibu pamoja na kufadhili vitendo hivi vya kinyama wanashughulikiwa kikamilifu mintarafu sheria za kitaifa na kimataifa.

Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa Serikali mbali mbali kushirikiana na kushikamana ili hatimaye, vitendo vya kigaidi viweze kutoweka katika uso wa dunia, na kutoa nafasi kwa watu kuendelea na shughuli zao mbali mbali. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, CBCN, limeitisha Siku 40 za: Kusali na Kufunga kwa ajili ya kuombea haki na amani nchini Nigeria. Familia ya Mungu nchini Nigeria kuanzia tarehe 22 Agosti 2020, Kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia wa Amani hadi tarehe 30 Septemba 2020 katika mkesha wa Sherehe ya Uhuru wa wananchi wa Nigeria itakuwa inaombea haki na amani nchini mwao. Itakumbukwa kwamba, Nigeria ilijipatia uhuru wake tarehe 1 Oktoba 1960. Maaskofu Katoliki nchini Nigeria, wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumlilia Bikira Maria, Malkia wa Amani, ili aweze kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, aweze kusitisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, wanaoendelea kupoteza maisha yao kila kukicha kwa sababu ya mashambulizi yanayofanywa na kikundi cha Boko Haram.

Amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu, mahali ambapo hakuna amani, si rahisi sana watu kuweza kupata maendeleo ya kiroho na kimwili. Misimamo mikali ya kidini na kiitikadi ni hatari sana kwa umoja na mafungamano ya kitaifa na kimataifa. Ni wajibu msingi kwa wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Inasikitika kuona kwamba, kuna baadhi ya wanasiasa wanataka kujinufaisha wenyewe kutokana na machafuko ya kidini na kijamii nchini Nigeria. Rushwa na ufisadi; uchoyo na ubinafsi; uchu wa mali na madaraka ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuchochea uwepo wa vikundi vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Rushwa na ufisadi vikikomeshwa, sera na mikakati ya maendeleo ikapangwa vyema, vijana wakapata fursa za ajira, kwa hakika, vitendo vya kigaidi vitapungua kama sio kutokomea kabisa.

Wananchi wa Nigeria wanahitaji kuona maboresho makubwa katika huduma ya elimu, afya, ustawi wa jamii pamoja na kuwa na nishati ya umeme wa kuaminika. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linapenda kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa: haki, amani, maridhiano na upatanisho wa kitaifa, ili kuwawezesha watu wa Mungu nchini Nigeria kujikita zaidi katika njia ya haki na amani. Askofu mkuu Augustine Obiora Akubeze, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, CBCN anasema, wananchi wamechoka sana na mashambulizi ya kigaidi dhidi yao! Watu wa Mungu wanasubiri kwa hamu kusikia kwamba, mashambulizi ya kigaidi yamekoma na wahusika wamefikishwa mbele ya mkono wa sheria, ili kujibu mashtaka yao. Haki, na amani ni tunu msingi na kikolezo cha maendeleo fungamani ya binadamu.

Papa: Nigeria

 

 

15 August 2020, 14:31