Baba Mtakatifu Francisko anaadhimisha kumbukumbu ya Mwaka mmpja tangu alipotembelea Msumbiji, Madagascar na Mauritius Septemba 2019. Baba Mtakatifu Francisko anaadhimisha kumbukumbu ya Mwaka mmpja tangu alipotembelea Msumbiji, Madagascar na Mauritius Septemba 2019. 

Kumbukumbu ya Mwaka Mmoja wa Hija ya Kitume Nchini Msumbiji

Hija kitume ya Papa Francisko nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 iliongozwa na kauli mbiu “Matumaini, amani na upatanisho." Papa alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano na familia ya Mungu nchini Msumbiji. Alikazia umuhimu wa kujenga amani na upatanisho wa kidugu; mchakato wa maendeleo sanjari na utunzaji bora wa mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu iliyongoza hija kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 ilikuwa ni: matumaini, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu katika hotuba yake alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano na familia ya Mungu nchini Msumbiji kutokana na majanga asilia. Alikazia umuhimu wa kujenga amani na upatanisho wa kidugu; mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Baba Mtakatifu aliwashukuru watu wa Mungu nchini Msumbiji kwa mapokezi na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake nchini Msumbiji. Aliwapongeza kwa utajiri wa tamaduni, uoto wa asili, furaha na matumaini ya watu wa Mungu nchini Msumbiji. Aliwashakuru wadau wote waliojisadaka ili kupyaisha tena mchakato wa amani na upatanisho nchini Msumbiji. Baba Mtakatifu aliipongeza na kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imesimama kidete ili kuhakikisha kwamba mchakato wa amani na upatanisho wa kitaifa, licha ya matatizo na changamoto zake, unarejea tena na matokeo yake ni kutiwa sahihi kwa Mkataba wa Amani huko Serra da Gorongosa kati ya Chama cha FRELIMO na RENAMO.

Mkataba huu unafutilia mbali uhasama kati ya ndugu wamoja nchini Msumbiji na kwamba, Mkataba huu utaimarisha zaidi Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi mjini Roma kunako mwaka 1992. Matunda ya mchakato huu yameanza kuonekana kwa kutambuana kama ndugu, wenye dhamana na wajibu wa kuendeleza ustawi wa nchi ya Msumbiji. Ujasiri unaleta amani ya kweli, unatafuta na kudumisha ustawi na maendeleo ya wengi. Wananchi wa Msumbiji wameteseka sana na madhara ya vita na kinzani za kijamii, lakini hawakutaka kukubali kutawalia na chuki, uhasama na mtindo wa kutaka kulipizana kisasi na kwamba, vita haikuwa na usemi wa mwisho katika mustakabali wa wananchi wa Msumbiji. Vita imeharibu sana makazi ya watu, imewatumbukiza wananchi katika baa la njaa, ujinga na maradhi. Vita imewakosesha watu nyumba za sala na ibada; imepelekea watu kukosa fursa za ajira na kwamba, kuna umati mkubwa wa wananchi wa Msumbiji walilazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta: usalama na hifadhi ya maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Septemba, 2019 aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Zimpeto uliosheheni watu kutoka sehemu mbali mbali za Msumbiji. Katika mahubiri yake alikaiza umuhimu wa familia ya Mungu nchini Msumbiji kujikita katika mchakato wa upatanisho ili kuondokana na vita, chuki na uhasama. Ni wakati wa kusamehe na kusahahu, ili kumwilisha Amri ya upendo inayovunjilia mbali kuta za utengano. Ni muda muafaka wa kujizatiti katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Amani ya kweli inabubujika kutoka katika undani wa mwamini mwenyewe! Baba Mtakatifu alisema, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kuwasikiliza na kuwapenda adui zao. Haya ni maneno ambayo yanapaswa kupewa uzito wa pekee hata na watu wa Mungu nchini Msumbiji kwa kutambua na kuguswa na uhalisia wa maisha yao. Adui ni watu wanao wachukia na kuwatenga wengine; ni watu wanaowachafulia wengine utu na heshima yao pamoja na kuwakashfu jirani zao. Wananchi wengi wa Msumbiji bado wana madonda ya vita, chuki na uhasama.

Ni madonda yanayowagusa hata watu wengine ambao tayari wamekwisha tangulia mbele za haki, lakini kuna wengine bado wako hai. Kuna hatari kwamba, madonda ya zamani yataibuliwa tena na hivyo kukwamisha maendeleo yaliyokwisha kupatikana hadi wakati huu kama ilivyojitokeza huko Cabo Delgado. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 23 Agosti 2020 mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa mara nyingine tena alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji na kwa namna ya pekee wale ambao wako Cabo Delgado, Kaskazini mwa Msumbiji, wanaoteseka kutokana na vitendo vya kigaidi kimataifa. Baba Mtakatifu asema, amewataja watu wa Mungu nchini Msumbiji, kwa kukumbuka hija yake ya kitume nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 iliyoongozwa na kauli mbiu “Matumaini, amani na upatanisho.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso ya wananchi wa Msumbiji, hivi karibuni, alimpigia simu Askofu Fernando Lisboa wa Jimbo Katoliki la Pemba, Msumbiji, ili kumfariji na kutaka kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji. Alisema, anafuatilia matukio yote ya Cabo Delgato kwa wasi wasi mkubwa na kwamba, daima amewaweka katika sala zake. Katika hali ngumu na wasi wasi wa maisha, kamwe wasisite kumpatia taarifa mapema. Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 12 Aprili 2020, aliadhimisha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baadaye, akatoa ujumbe wa Pasaka: “Urbi et Orbi”. Alisikika akisema kwamba, dharura ya wakati huu kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 isiifanye Jumuiya ya Kimataifa ikasahau majanga mbali mbali yanayoendelea kuwakumba watu wengi sehemu mbali mbali za dunia.

Papa Francisko alimwomba, Bwana wa uzima awe karibu na familia ya Mungu Barani Afrika na Asia inayokabiliwa na mateso makubwa ya kibinadamu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu alilitaja Jimbo la Cabo Delgado, lililoko Kaskazini mwa Msumbiji kuwa linakabaliwa na changamoto kubwa. Kundi la kigaidi la Al Shabab kutoka Somalia linaendesha mashambulizi kwa raia wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu Francisko anaangalia uwezekano wa kupeleka msaada wa dharura nchini Msumbiji. Askofu Fernando Lisboa wa Jimbo Katoliki la Pemba, Msumbiji, mara kadhaa amepokea vitisho vya kifo, kutokana na kujipambanua kuwa ni sauti na mtetezi wa maskini na wanyonge Jimbo la Cabo Delgado.

Papa: Msumbiji
24 August 2020, 14:15