Papa Francisko: Muujiza wa Mikate Mitano na Samaki Mawili ni Kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu na hatimaye ni katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Papa Francisko: Muujiza wa Mikate Mitano na Samaki Mawili ni Kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu na hatimaye ni katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. 

Papa Francisko: Muujiza wa Mikate Mitano na Samaki Wawili: Huruma

Muujiza wa Kristo Yesu kuwalisha watu zaidi ya elfu tano ni kielelezo cha nguvu na uweza wake, alama ya upendo na ukarimu wa Mungu. Yesu, akajiingiza katika maisha ya waja wake, akagundua uchovu wao na skawalisha kwa Neno na kuwapatia chakula kilichowarutubisha na kuwaimarisha katika maisha yao, wakawa tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Alama ya Ekaristi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 18 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, Mwinjili Mathayo anaweka mbele ya macho ya  waamini muujiza wa Kristo Yesu kuwalisha watu zaidi ya elfu tano. Rej. Mt. 14: 13-21! Yesu anataka kuwafundisha wafuasi wake umuhimu wa kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya kusikiliza na kujibu kilio, shida na mahangaiko ya jirani zao, kama kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Muujiza huu unatendeka katika eneo la nyikani, mahali ambapo Kristo Yesu pamoja na wafuasi wake, walikuwa wamekwenda kusali faraghani, lakini makutano waliposikia, walimfuata, Yesu akatoka, akawahurumia na kuwaponya wagonjwa wao. Maneno na vitendo vya Kristo Yesu ni chemchemi ya faraja kwa wote waliokuwa wanamsikiliza kwa umakini mkubwa. Jioni ilipowadia, wanafunzi wake, wakamwomba Yesu awaage makutano ili waende zao kujinunulia chakula.

Lakini, Kristo Yesu akawajibu kwa mkato kabisa “Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi kula”. Lakini Yesu mwenyewe alikua anatambua ni jambo gani ambalo angelitenda ili kuwalisha watu hawa wote. Alitaka kwanza kabisa, wabadili mawazo na mwelekeo wao, ili waweze kuwa tayari kusikiliza kwa makini mateso na mahangaiko ya jirani zao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kama utekelezaji wa mantiki ya huruma na upendo wa Mungu, kama  ilivyokuwa jana, leo na hata milele yote!  Mtume mmoja akasema kwamba, wanayo mikate mitano na samaki wawili! Kristo Yesu akaagiza wamletee na kuwaketisha makutano katika majani. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate,  akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Ile mikate mitano na samaki wawili, hawakuisha hata kidogo, wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa.

Huu ni muhtasari wa tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 2 Agosti 2020. Muujiza wa Kristo Yesu kuwalisha watu zaidi ya elfu tano ni kielelezo cha nguvu na uweza wake, alama ya upendo na ukarimu wa Mungu kwa watoto wake ambao wamechoka sana na wana elemewa na baa la njaa! Kristo Yesu, akajiingiza katika maisha ya waja wake, akagundua uchovu wao na wala hakutaka kuona mtu awaye yeyote anapotea wala kunyong’onyea. Akawalisha kwa Neno na kuwapatia chakula kilichowarutubisha na kuwaimarisha katika maisha yao, wakawa tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kwa hakika, muujiza huu, ulikuwa unafanya rejea katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake Azizi, hasa pale anapotazama juu mbinguni, anapobariki, kuimega mikate ile na kuwapatia wanafunzi, na wanafunzi wakawapa makutano. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya Mkate wa Ekaristi Takatifu, Lishe ya maisha na uzima wa milele pamoja na chakula cha kila siku, muhimu sana kwa maisha ya hapa ulimwenguni. Kabla ya Kristo Yesu kujitoa na kujisadaka kama Mkate wa Wokovu ulioshuka kutoka mbinguni, Kristo Yesu, anawapatia chakula cha kimwili, wale wote waliokuwa wanamfuata, kwani licha ya kushinda pamoja na Kristo Yesu huku wakisikiliza Neno lake na kuwaponya wagonjwa wao, walisahau kuchukua masurufu ya njiani.

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu yaani Mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo ni: Kumbu kumbu ya sadaka ya Kristo Yesu na ya Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya sifa katika shukrani, kwa ajili ya kazi ya uumbaji na ukombozi iliyotendwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu.  Ni sadaka ya shukrani na baraka kutoka kwa Mungu Mwenyezi. Kumbu kumbu na uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na wafuasi wake, hadi atakaporudi kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! Hii ni Karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao! Kristo Yesu amewafundisha wafuasi wake kusali kwa ajili ya kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia chakula cha kila siku; yaani chakula na lishe ya mwili na chakula cha kiroho, yaani Ekaristi Takatifu. Waamini washiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa kutambua kwamba, wanapaswa kujisadaka na kujimega, ili kuwa Ekaristi kwa ajili ya jirani zao ambao ni maskini na wanapungukiwa mahitaji msingi katika maisha yao.

Huruma, upendo na kujali mahitaji ya watu wa Mungu ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni changamoto ya kuonesha upendo na mshikamano na wahitaji. Watu waguswe na matatizo pamoja na changamoto zinazosababishwa na: vita, baa la njaa na milipuko ya magonjwa, ili kuwaonesha huruma na upendo. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huu ndio mwelekeo sahihi katika kushiriki na kuadhimisha kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu. Waamini wawe na huruma na mapendo kwa jirani zao; wajiaminishe kwa upendo wa Mungu Baba na wawe na ujasiri wa kuweza kushirikishana matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie waamini kufuata ile Njia inayooneshwa na Kristo Yesu katika Injili ya Jumapili ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa. Hii ni hija inayopania ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu, muhimu sana kwa ajili ya walimwengu wenyewe, kwani mchakato huu umeanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu na unapata hitimisho lake kwa Mwenyezi Mungu.

Papa: Huruma ya Mungu

 

 

02 August 2020, 13:49