Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amefanya kumbukizi la miaka 75 tangu Miji ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya atomiki kunako mwaka 1945. Baba Mtakatifu Francisko amefanya kumbukizi la miaka 75 tangu Miji ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya atomiki kunako mwaka 1945. 

Miaka 75 ya Shambulizi la Atomiki Hiroshima na Nagasaki Japan

Papa Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 9 Agosti 2020 amefanya kumbukizi la Miaka 75 tangu Miji ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya atomiki. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan mwezi Novemba, 2019 ilipambwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni majira ya saa mbili na robo asubuhi kwa saa za Japan, tarehe 6 Agosti 1945, miaka 75 iliyopita, ndege ya kijeshi ya Marekani chapa “B-29 Enola Gay” ilipodondosha bomu la atomiki na kuwauwa hapo hapo watu 140,000 kati ya wenyeji wapatao 350,000 wa mji wa Hiroshima, nchini Japan. Takribani saa sita mchana ya tarehe 9 Agosti 1945, bomu la nyuklia liliangushwa tena na Marekani kwenye mji wa Nagasaki na wingu zito lilienea mjini humo na huo ukawa ni mwanzo wa maafa makubwa kwa watu na mali zao. Na huo ukawa ni mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kielelezo cha: ukatili wa hali ya juu kabisa, ubinafsi na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko. Silaha za nyuklia bado ni tishio kubwa kwa: amani, usalama, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani. Watu wengi walipoteza maisha kutokana na kiu iliyosababishwa na mionzi mikali ya silaha za nyuklia. Leo hii, watu wa kiu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 9 Agosti 2020 amefanya kumbukizi la Miaka 75 tangu Miji ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya atomiki.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019 ilipambwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe unaowataka watu wa Mungu nchini Japan kusimama kidete kulinda: utu, haki na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha. Japan inatambua fika madhara ya vita na matumizi ya silaha za atomiki; maafa ya tetemeko kubwa la ardhi na tsunami iliofuatia vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 nchini Japan. Uharibifu uliosababishwa kwenye mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daichi ukapelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Haya ni mambo ambayo bado yameacha kumbu kumbu hai katika maisha ya wananchi wa Japan. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, kweli dunia inakuwa huru dhidi ya vitisho vya silaha za nyuklia.

Kwa upande wake Askofu mkuu Tarcisius Isao Kikuchi wa Jimbo kuu la Tokyo nchini Japan amesema, janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ili kuweza kudhibiti maambukizi mapya na hatimaye kuweza kupata chanjo na tiba muafaka wa gonjwa hili la hatari, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa hali na mali. Huu ni wakati wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuzingatia sera na masharti yanayotolewa na madaktari na wataalamu wa sekta ya afya katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ni muda muafaka wa kuadhimisha kumbukizi la Miaka 75 tangu miji ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya atomiki, ili kuendelea kuombea: umoja, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, CBCJ., linasema kwamba, amani inatishiwa sana na mashindano, utengenezaji, biashara pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambayo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu! Baraza la Maaskofu Katoliki Japan katika ujumbe wake wa Siku 10 za kuombea Amani Duniani, kwa mwaka 2020 linasema: Linda maisha yote, Amani ni safari ya Matumaini. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, CBCJ., kwa nyakati mbali mbali limekuwa likitoa ujumbe kwa ajili ya kumbukumbu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Leo hii, bado kuna vita baridi, amani inaendelea kutishiwa kwa sababu ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za nyuklia sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi na sasa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, GBC., “Deutsche Bischofskonferenz” kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa ya Kiinjili Ujerumani yanasema, mashambulizi ya silaha za nyukilia si jambo la kufikirika hata kidogo, kwa sababu hata wakati huu, kuna mashindano ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za nyuklia, hali inayotishia usalama, amani na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Leo hii kuna vitisho vya mashambulizi ya silaha za nyuklia, kuna vitendo vya kigaidi ambavyo ni kinyume kabisa cha uhuru wa kuabudu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Zaidi ya hayo, kuna mashindano ya biashara ya silaha duniani, ambayo ni chanzo cha vita, kinzani na migogoro sehemu mbali mbali za dunia. Kuna baadhi ya nchi zinapenda sera za kutengeneza, kumiliki na kulimbikiza silaha za nyuklia kama mpango mkakati wa masuala ya kisiasa. Lakini, Baba Mtakatifu Francisko anasema, utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema!

Papa: Nagasaki

 

09 August 2020, 12:15