Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu ya Bikira Maria Mkuu, Roma, tarehe 5 Agosti 2020 ametembelea na kusali Kanisani hapo. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu ya Bikira Maria Mkuu, Roma, tarehe 5 Agosti 2020 ametembelea na kusali Kanisani hapo. 

Kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu, Roma!

Kanisa la Bikira Maria Mkuu, lililoko mjini Roma ni Kanisa la kwanza kujengwa kwa heshima ya Mama wa Mungu mara baada ya Mtaguso wa Efeso, uliofanyika kunako mwaka 431, hapo Kanisa likamtangaza Bikira Maria kuwa ni "Theotokos." Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko, majira ya jioni, alikwenda kutembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 5 Agosti anaadhimisha Siku kuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa la Bikira Maria Mkuu, lililoko mjini Roma. Hili ni Kanisa lililojengwa kwa heshima ya Mama wa Mungu mara baada ya Mtaguso wa Efeso, uliofanyika kunako mwaka 431, hapo Kanisa likamtangaza Bikira Maria kuwa ni "Theotokos" yaani Mama wa Mungu. Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko, majira ya jioni, alikwenda kutembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Katika hali ya ukimya, Baba Mtakatifu alimshirikisha Bikira Maria magumu, machungu na matumaini yaliyoganda moyoni mwake. Kati ya machungu haya ni athari za ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Lakini kwa namna ya pekee kabisa, Jumatano tarehe 5 Agosti 2020 amewakumbuka watu wa Mungu walioathirika sana na mlipuko uliotokea kwenye bandari ya Beirut, nchini Lebanon na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baada ya sala, tafakari na kimya kikuu, Baba Mtakatifu alirejea tena mjini Vatican na kuendelea na shughuli zake za kila siku!

Wakati huo huo, majira ya asubuhi, Kardinali Stanisław Ryłko, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Katika mahubiri yake, ameelezea kwa ufupi historia ya Kanisa hili na umuhimu wake kama kielelezo cha imani na upendo wa watu wa Mungu kwa Bikira Maria. Huu ni utajiri  na amana ya fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kukaa kati ya waja wake. Kanisa hili pia linatunza masalia ya Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani”, faraja ya wale wote wanaomkimbilia kwa imani na matumaini.  Kanisa hili ni ushuhuda wa utenzi wa Bikira Maria, “Magnificat” aliposema “Kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu na jina lake ni takatifu.” Lk. 1:47.

Ujumbe huu wa Bikira Maria umepokelewa na waamini wa vizazi vingi, wanaofika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ili kuadhimisha Sakramenti mbali mbali za Kanisa. Kanisa hili limekuwa ni Madhabahu ya kwanza yaliyojengwa kwa heshima ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa kwa nchi za Magharibi. Madhabahu yote haya anasema Kardinali Stanisław Ryłko ni mahali ambapo waamini wanapata fursa ya kusikiliza Neno la Mungu, Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kujipatia neema ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuandika upya historia ya maisha yao. Kwa wale waliopondeka na kuvunjika moyo, wanaweza kupata faraja kutoka kwa Bikira Maria, afya ya Warumi, hasa katika kipindi hiki cha janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kama ilivyokuwa kwa Mtume Yohane, hata waamini wa nyakati hizi, wanaalikwa kumkaribisha Bikira Maria katika makazi yao, lakini zaidi nyoyoni mwao. Bikira Maria ni Mama ana Mwalimu. Daima yuko tayari kuwasikiliza, kuwajibu na kuwafariji wale wote wanaomkimbilia huku bondeni kwenye machozi, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Kanisa Kuu la B. Maria

 

06 August 2020, 13:22