Papa Francisko asema kuanzia tarehhe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba 2020, Wakristo wanaadhimisha Kipindi cha Kazi ya Uumbaji, hili ni tukio la kiekumene! Papa Francisko asema kuanzia tarehhe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba 2020, Wakristo wanaadhimisha Kipindi cha Kazi ya Uumbaji, hili ni tukio la kiekumene! 

Papa Francisko: Kipindi cha Kazi Ya Uumbaji 1 Sept- 4 Oktoba 2020

Papa Francisko: Tarehe 1 Septemba 2020 ni Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote. Tangu wakati huo hadi tarehe 4 Oktoba ni Kipindi cha Kuadhimisha Kazi ya Uumbaji kwa kushirikiana na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu yote ya Kikristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mwaka huu, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Mama Dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki inayoadhimishwa tarehe 1 Septemba 2020, ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015 kama sehemu ya mchakato endelevu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa ya uumbaji sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Mama Dunia na Maskini, “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.”

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika Bwana, Jumapili tarehe 30 Agosti 2020 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 1 Septemba 2020 ni Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote. Tangu wakati huo hadi tarehe 4 Oktoba ni Kipindi cha Kuadhimisha Kazi ya Uumbaji kwa kushirikiana na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu yote ya Kikristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mwaka huu, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Mama Dunia. Matukio kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika kipindi hiki chote, yanapania pamoja na mambo mengine, kufafanua na kumwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu taalimungu ya kiekolojia. Lengo ni kudumisha ukweli kuhusu utu, heshima ya binadamu, haki msingi pamoja na uelewa wa kazi ya uumbaji kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kazi ya uumbaji iliyokuwa nzuri machoni pa Mwenyezi Mungu na kuikabidhi kwa binadamu kama zawadi imeharibiwa kwa uwepo wa dhambi, ubinafsi na uchoyo unaotaka kuinyonya kwa uchimbaji wa madini na nishati ya mafuta; kilimo cha mashamba makubwa pamoja na uchomaji na ukataji ovyo wa misitu hali ambayo imesababisha kupanda kwa joto duniani pamoja na kuongezeka kiwango cha bahari.

Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira unaofanywa kwa kutupa ovyo taka za plastiki; mambo yanayotishia usalama wa maisha ya viumbe hai duniani. Ni katika muktadha huu pia, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, linayounganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka katika nchi thelathini na tatu kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa Ulaya, CEC, yanayaalika Makanisa wanachama, kuungana pamoja ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kutokana na amana na utajiri wa imani kama kielelezo makini cha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya vinasaba na utajiri wa imani ya Kikristo. Hii inatokana na ukweli kwamba, uumbaji ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya binadamu pamoja na viumbe vyote hai. Kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanawajibika kulinda, kutunza na kutetea mazingira bora nyumba ya wote, kama watumishi waaminifu wa Mungu. Mzaburi anasema, Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake. Rej. Zab. 24:1.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si”, yaani: “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.”. Familia ya binadamu inapaswa kushirikiana na kushikamana pamoja ili kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu na kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya hatima ya sayari dunia. Haya ni majadiliano shirikishi na wala hakuna sababu ya mtu awaye yote kutengwa wala kuacha nyuma, kwa sababu changamoto za mazingira zinazomsibu mwanadamu katika ulimwengu mamboleo zina kita mizizi yake katika maisha na utu wa binadamu na kwamba, binadamu wote wanaathirika. Kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika utekelezaji wa ekolojia ya mazingira bora, kwa kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji.

Maadhimisho haya yenye mwelekeo wa kiekumene yanapata chimbuko lake kutoka kwa Patriaki Dimitrios wa kwanza kunako mwaka 1989 na tangu wakati huo, Makanisa yameendelea kuboresha maadhimisho haya kwa mwelekeo wa kiekumene kufuatia maamuzi yaliyofanyia huko Basel kunako mwaka 1989, Graz mwaka 1997 na Sibiu mwaka 2007. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, limedhihirisha umuhimu wa mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Huu ni mwaliko wa kuwa macho na makini kulinda mazingira ili kuenzi Injili ya uhai na maendeleo fungamani ya binadamu. Huu ni wakati wa kusimama kidete kupambana na changamoto na athari za mabadiliko ya tabianchi. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE., na Baraza la Makanisa Ulaya, CEC., yanayaalika Makanisa wanachama kuadhimisha kipindi hiki kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei inayopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu, ili kuweka uwiano mzuri kati mambo ya kijamii, kiuchumi na kiekolojia, sanjari na kuweka uwiano mzuri katika maisha ya mwanadamu.

Jambo la msingi ni kukuza na kudumisha usawa, haki na maendeleo fungamani ya binadamu, ili Kanisa liendelee kuwa ni sauti ya kinabii kwa ajili ya kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Viongozi, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kuwa makini katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kuendelea kuishi huku wakiwa na moyo wa kiekumene, wakiwa wameungana katika sala na matendo. Ujumbe huu wa pamoja wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE., na Baraza la Makanisa Ulaya, CEC., umetiwa mkwaju na Christian Krieger, Rais wa CEC pamoja na Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa CCEE.

Papa: Mazingira
31 August 2020, 07:42