Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu: Injili ya imani, matumaini na mapendo katika Kipindi cha COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu: Injili ya imani, matumaini na mapendo katika Kipindi cha COVID-19. 

Papa Francisko: Injili ya Imani, Matumaini na Mapendo-COVID-19

Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumtaza Kristo Yesu kwa jicho la imani, ili kuweza kuambata na kukumbatia Injili ya matumaini ya Ufalme wa Mungu ambao umeletwa na Kristo Yesu. Huu ni Ufalme wa uponyaji na wokovu; haki na amani inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma na mapendo. Ni Injili ya imani, matumaini na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kumaliza mapumziko yake ya kipindi cha kiangazi, Jumatano tarehe 5 Agosti 2020 ameanza tena shughuli zake za kila siku kwa katekesi kuhusu: “Uponyaji wa Ulimwengu.” Baba Mtakatifu ametoa tafakari hii akiwa kwenye Maktaba yake binafsi. Neno la Mungu lililoongoza Katekesi hii ni juu ya Kristo Yesu anamsamehe dhambi na kumponya mwenye kupooza kule Kapernaumu. Waandishi wakamtuhumu kuwa alikuwa anakufuru, kwa sababu Mwenyezi Mungu peke yake, ndiye aliyekuwa na mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi zao. Yesu akawadhihirishia kwamba, alikuwa na uwezo wa kumwondolea mtu dhambi na kumponya! Akamwambia mwenye kupooza: “Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako”! Rej. Mk. 2-1-5. 10-11. Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 linaendelea kusababisha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, kiasi hata cha kufunua na kuuanika bayana udhaifu wa maisha ya mwanadamu. Kuna watu na familia nyingi zinazoendelea kuteseka kutokana na kukosa uhakika wa usalama wa maisha yao kutokana na matatizo ya kiuchumi na kijamii, ambayo waathirika wakuu ni watu maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumtazama Kristo Yesu kwa jicho la imani, ili kuweza kuambata na kukumbatia Injili ya matumaini ya Ufalme wa Mungu ambao umeletwa na Kristo Yesu. Huu ni Ufalme wa uponyaji na wokovu; haki na amani inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma na mapendo. Baba Mtakatifu amegusia kuhusu fadhila za Kimungu, ambazo zinaweka msingi, zinahuisha, na kuainisha utendaji adili wa Mkristo. Zinapasha habari na kuzihuisha fadhila zote za maadili. Zinamiminwa na Mwenyezi Mungu katika roho za waamini na kuwawezesha kutenda kama watoto wa Mungu na hatimaye, kustahili uzima wa milele. Nazo ni amana ya uwepo na tendo la Roho Mtakatifu katika nguvu ya kibinadamu. Kuna fadhila tatu za Kimungu: Imani, Matumaini na Mapendo. Hizi ni zawadi zinazowaponya waamini na kuwapatia uwezo wa kuponya na hivyo kuwafungulia maono mapya ya maisha, hata wakati huu wanapoendelea kuogelea kwenye bahari iliyochafuka katika nyakati hizi. Rej. KKK. Namba 1812-1813.

Huu ni mkutano mpya unaowawezesha waamini kukutana na Injili ya Imani, Matumaini na Mapendo, na hivyo kuwachangamotisha kuwa na moyo wa ubunifu na upyaisho. Ni katika muktadha huu, waamini wataweza kuganga na kuponya magonjwa yao ya kimwili, kiroho na kijamii. Wataweza kuzama na hatimaye, kuganga na kuponya miundombinu ambayo imekuwa inaendelea kusigina na kuharibu haki msingi za binadamu; kwa kuendekeza ubinafsi na utengano; mambo yanayohatarisha familia ya binadamu na ulimwengu katika ujumla wake. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, ameacha mifano kedekede ya uponyaji, kwa wale waliokuwa wanasumbuliwa na homa kali na wagonjwa wa ukoma. Aliwafumbua macho vipofu na viziwi wakapata kusikia. Aliwaganga na kuwaponya watu magonjwa yao na kuwaondolewa pia dhambi zao: Kwa maneno mafupi, Kristo Yesu alipania kumponya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili kumrejesha tena katika Jumuiya kwa kumwondoa katika upweke na hali ya kutengwa.

Mwinjili Marko anaonesha jinsi ambavyo Kristo Yesu anamsamehe dhambi na kumponya mwenye kupooaza kule Kapernaumu. Waandishi wakamtuhumu kuwa alikuwa anakufuru, kwa sababu Mwenyezi Mungu peke yake, ndiye aliyekuwa na mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi zao. Yesu akawadhihirishia kwamba, alikuwa na uwezo wa kumwondolea mtu dhambi na kumponya! Akamwambia mwenye kupooza: “Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako”! Rej. Mk. 2-1-5. 10-11. Katika hali na mazingira haya, watu wengi walipigwa na bumbuwazi kwa sababu Yesu alitoa jibu makini kwa imani ya watu waliokuwa wamembeba yule mgonjwa, matumaini yao kwa Kristo Yesu na upendo waliokuwa nao kati yao, kiasi hata cha kujitaabisha kumpeleka mgonjwa wa Kristo Yesu. Hapa mgonjwa anaponyeshwa na kuondolewa dhambi zake. Hii ni inakuwa ni chemchemi ya upyaisho wa maisha kwa marafiki wa yule mgonjwa mwenye kupooza.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni uponyaji wa kimwili na kiroho, matunda ya kukutana na Kristo Yesu kama mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake. Urafiki, upendo na imani ya wale wote waliokuwa ndani ya nyumba ile viliongezeka maradufu. Hii ni kutokana na kukutana na Kristo Yesu Mponyaji. Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaweza kusaidia mchakato wa uponyaji wa ulimwengu mamboleo. Kwa sababu wao ni wafuasi wa Kristo Yesu, Bwana na Mponyaji wa magonjwa ya kiroho na kimwili. Yeye alisamehe dhambi za mwenye kupooza, akawarudishia wagonjwa afya zao. Kristo Yesu alitaka Kanisa lake liendeleze, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kazi yake ya uponyaji na ya wokovu, hata miongoni mwa viungo vyake. Huu ni uponyaji wa kimwili, kijamii na kiroho.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Mama Kanisa anatoa neema ya uponyaji unaofanywa na Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti na huduma katika sekta ya afya na hasa vijijini. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuzuia na kuponya magonjwa na wala halina mwelekeo unaofungamana na mambo ya kisiasa na kijamii. Huu ni wajibu msingi unaopaswa kutekeleza na wanasiasa na wafanyakazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii. Lakini kadiri ya nyakati zilivyozidi kuyoyoma katika mwanga wa Injili, Mama Kanisa ameibua kanuni msingi za Mafundisho ya Jamii nazo ni: Utu na heshima ya binadamu, Ustawi, Mafao na Maendeleo ya wengi; Upendeleo kwa Maskini; matumizi bora ya rasilimali za dunia kwa ajili ya wengi. Kanuni nyingine ni mshikamano unaoongozwa na kanuni auni; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhtasari wa fadhila ya: Imani, Matumaini na Mapendo.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia sasa, anapenda kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujiunga pamoja naye ili kutafakari kuhusu janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa kuangalia madhara yake, mintarafu magonjwa ya kijamii. Tafakari hii makini, itaongozwa na Mwanga angavu wa Injili, Fadhila za Kimungu pamoja na Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hii ni nafasi muafaka ya kutumia Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kuisaidia familia ya binadamu kuweza kuganga na kuponya ulimwengu huu unaoteseka kutokana na magonjwa makubwa na mazito! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwa pamoja wataweza kushiriki tafakari hii kama wafuasi wa Kristo Yesu anayeganga na kuponya, ili kujenga ulimwengu bora zaidi unaosimikwa katika matumaini kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Papa: Katekesi
05 August 2020, 14:18