Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kulijalia Kanisa neema ya kuwa maskini kwa ajili ya huduma kwa maskini na wanyonge zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kulijalia Kanisa neema ya kuwa maskini kwa ajili ya huduma kwa maskini na wanyonge zaidi. 

Papa Francisko: Kanisa Maskini Kwa Ajili ya Huduma kwa Maskini

Papa Francisko: Kwa njia ya furaha ya Injili waamini wamwombe Mungu neema itakayoliwezesha Kanisa kuwa maskini kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maskini wanayo mengi ya kulifundisha Kanisa na waamini wajiruhusu wainjilishwe na maskini. Kimsingi, maskini wanapaswa kupewa upendeleo wa pekee katika Taifa la Mungu. Maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake kuhusu “Uponyaji wa Ulimwengu” mintarafu Mwanga angavu wa Injili, Fadhila za Kimungu pamoja na Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa, Jumatano tarehe 19 Agosti 2020, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kwa njia ya furaha ya Injili, kumwomba Mwenyezi Mungu neema itakayoliwezesha Kanisa kuwa maskini kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maskini wanayo mengi ya kulifundisha Kanisa na waamini wajiruhusu wainjilishwe na maskini. Kimsingi, maskini wanapaswa kupewa upendeleo wa pekee katika Taifa la Mungu. Kristo Yesu, aliyejifanya maskini, akajisadaka bila ya kujibakiza pale Msalabani na hivyo kujitoa kuwa chakula cha kiroho, Ekaristi Takatifu, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, awawezeshe waamini pia kuwa ni Ekaristi safi kwa jirani zao, ili waweze kujimega na kujitoa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anaendelea kuzifikiria familia ambazo kutokana na hali ngumu ya uchumi na ukata wa fedha, hazitaweza kujipatia nafasi ya likizo ya kipindi cha kiangazi. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awajalie kupata furaha, amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu anapenda kuziweka familia zote hizi katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, asili na chemchemi ya upendo, huruma na furaha ya kweli! Likizo ya kipindi cha kiangazi, iwe ni fursa kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kutenga muda zaidi kwa ajili ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa sanjari na kujielekeza zaidi katika majiundo endelevu ya maisha ya Kikristo. Kwa njia hii, waamini wataweza kukuza roho ya umoja, upendo na mshikamano wa kidugu.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwahakikishia wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutafuta suluhu ya:  maisha ya kiroho, kisayansi na kijamii katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwamba, anaunga mkono juhudi zao, ili ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, ili hatimaye, kupata chanjo na tiba ya gonjwa hili hatari kwa maisha, ustawi na maendeleo ya binadamu. Upendo na ukarimu iwe ni njia muafaka ya kuwasaidia wagonjwa pamoja na familia zao; maskini na wazee, ili wasijisikie kwamba, wako pweke!

Kanisa la Maskini

 

19 August 2020, 13:39