Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amewabatizwa watoto mapacha waliotenganishwa vichwa vyao kwa operesheni maalum iliyofanyika kwenye Hospitali ya Bambino Gesù, Roma, Juni 2020. Papa Francisko amewabatizwa watoto mapacha waliotenganishwa vichwa vyao kwa operesheni maalum iliyofanyika kwenye Hospitali ya Bambino Gesù, Roma, Juni 2020.  (ANSA)

Papa Francisko Awabatiza Watoto Mapacha Waliotenganishwa Vichwa!

Baba Mtakatifu Francisko amewabatiza watoto wawili mapacha Ervina na Prefina kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, waliofanyiwa operesheni maalum kwenye Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na Vatican na hivyo kufanikiwa kuwatenganisha vichwa wao. Kwa sasa watoto wanaendelea kuonesha matumaini makubwa kwa leo na kesho iliyo bora hata kwa maskini. Huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika roho, na mlango unaowezesha kuzipata Sakramenti nyingine. Kwa njia ya Ubatizo mwamini anafanywa huru toka dhambini na kuzaliwa upya kama mtoto wa Mungu, na hivyo kuwa ni sehemu ya kiungo cha Kristo na kuingizwa katika Kanisa. Kwa njia hii, mwamini anafanywa kuwa ni mshiriki katika utume wa Kristo Yesu. Ubatizo ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji katika neno. Ubatizo ni kipaji cha Mwenyezi Mungu kilicho kizuri na kitukufu sana. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, mwamini anashiriki: ukuhani, ufalme na unabii wa Kristo Yesu. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amewabatiza watoto wawili mapacha Ervina na Prefina kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, CAR., waliofanyiwa operesheni maalum kwenye Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican na hivyo kufanikiwa kuwatenganisha vichwa wao. Kwa sasa watoto wanaendelea kuonesha matumaini makubwa kwa leo na kesho iliyo bora hata kwa maskini. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, katika mazingira ya faragha.

Hermine Nzotto, Mama wa watoto hawa mapacha amemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko kumshukuru kwa wema na ukarimu wake, aliowatendea watoto wake, ambao tayari walikuwa wanachungulia kaburi. Ni matumaini ya Mama Nzotto kwamba, watoto wake watakuwa ni kati ya watoto waliobahatika sana ulimwenguni. Huu ni muujiza endelevu uliotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 alipozindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, kwa kufungua lango la Kanisa kuu la Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Hili ni lango la huruma ya Mungu ambalo limewawezesha hata watoto maskini kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, wamebahatika kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Watoto hawa wamepewa majina mapya kwa sasa wanatambulikana kama Maria na Franciska, kielelezo cha imani kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko kati na karibu na waja wake anasema Mama Nzotto katika barua yake kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Ikiwa kama watoto hawa kwa neema ya Mungu watafanikiwa kwenda shuleni na kujifunza kama watoto wengine kusoma na kuandika, hata yeye katika umri huu, ataweza kujifunza kusoma na kuandika, ili aweze kuwasimulia watoto wake matendo makuu ya Mungu katika maisha yao na kwamba, wao ni kati ya watoto ambao amebahatika sana kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Misericordia vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni uso wa huruma ya Mungu, muhtasari wa imani ya Kanisa ambayo imefunuliwa naye kwa njia ya: mafundisho, matendo na nafsi yake. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Huruma ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Kusamehe makosa ni kielelezo dhahiri cha upendo wenye huruma. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa mwanadamu. Anajisikia kuwajibika, kwani Mwenyezi Mungu anataka kuwaona watoto wake wakiwa wamesheheni furaha na amani tele.

Hermine Nzotto, Mama wa watoto hawa mapacha yaani Maria na Franciska anaendelea kusema kwamba, mlango wa imani alioufungua Jimbo kuu la Bangui, mwaka 2015 na kufungwa tena baada ya kuhitimisha maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, umegeuka kuwa ni daraja la milele, ambalo hata maskini kutoka pembezoni mwa jamii, kama alivyokuwa yeye na watoto wake pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kupitia mlango huu na kuonja ndani mwao huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mama Hermine Nzotto katika barua yake, daima anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwawezesha madaktari chini ya uongozi, usimamizi na weledi wa Professa Carlo Efisio Marras, Mkuu wa Idara ya Upasuaji, Hospitali ya Bambino Gesù waliofanikisha muujiza huu ambao umefanyika kwa mara ya kwanza na kuokoa maisha ya watoto hawa mapacha!

Je, ni watoto wangapi duniani ambao bado hawajabahatika kuonja neema na huruma ya Mungu katika maisha yao! Mama Hermine Nzotto amehitimisha barua yake ya shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kumpongeza kwa jinsi ambavyo, anajisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anampongeza kwa ujasiri na imani thabiti aliyoionesha kwa watu wa Mungu, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, kwa kuamua kufanya hija ya kitume nchini mwao, bila ya kuogopa hali tete ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, akajitosa na kwenda nchini humo kama hujaji wa amani na upatanisho. Jeshi la mbu wanaosababisha ugonjwa wa Malaria, halikuwa tishio kwake, bali, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu vilipewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu Francisko kwa hakika ni kiongozi ambaye amebahatika kupata ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa!

Papa: Ubatizo Watoto Mapacha

 

11 August 2020, 13:29