Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na vitendo vya kigaidi vilivyofanywa kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Managua, nchini Nicaragua kwa kuchoma Msalaba! Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na vitendo vya kigaidi vilivyofanywa kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Managua, nchini Nicaragua kwa kuchoma Msalaba!  (AFP or licensors)

Papa Francisko Asikitishwa na Vitendo vya Kigaidi Nicaragua!

Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na Msalaba wa Kanisa kuu la Managua, Nicaragua kuchomwa moto hapo tarehe 31 Julai 2020 na mtu asiyefahamika bado. Huu ni Msalaba wa kale, ambao umewasindikiza watu kumwabudu Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kwa hakika, Msalaba huu umekuwa ni sehemu ya maisha ya watu wa Mungu nchini Nicaragua! Ugaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 2 Agosti 2020, kwa majonzi na masikitiko makubwa aliyaelekeza mawazo yake kwa watu wa Mungu nchini Nicaragua ambao wanasikitika sana kutokana na Msalaba wa Kanisa kuu la Managua, Nicaragua kuchomwa moto hapo tarehe 31 Julai 2020 na mtu asiyefahamika bado. Huu ni Msalaba wa kale, ambao umewasindikiza watu kumwabudu  Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Msalaba huu umekuwa ni sehemu ya maisha ya watu wa Mungu nchini Nicaragua. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Nicaragua uwepo wake wa karibu na kwamba, anaendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake!

Kwa upande wake Kardinali Leopoldo José Brenes, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Managua nchini Nicaragua anasema, hili ni tukio la kigaidi linaloonesha chuki na uhasama dhidi ya Kanisa Katoliki nchini Nicaragua. Bomu la kurushwa kwa mkono, lililipuka kwenye Kikanisa cha Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo na kuunguza Msalaba ambao waamini wamekuwa wakiuabudu kwa kipindi cha karne nne. Jimbo kuu la Managua linamshukuru Mungu kwa sababu janga hili la moto liliweza kuzimwa mara moja na hivyo kudhibiti uharibifu mkubwa ambao ungejitokeza. Hakuna watu waliojeruhiwa, lakini, kitendo hili cha kigaidi, kimewaathiri waamini wa Kanisa Katoliki nchini Nicaragua. Hili ni tukio ambalo lilipangwa na kutekelezwa na mtaalam wa mambo haya.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na matukio ya kuharibu na kunajisi Makanisa, mambo ambayo ni kinyume kabisa cha uhuru wa kuabudu na kidini na kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kidini. Matukio haya ya kigaidi, linasema Jimbo kuu la Managua, yanapaswa kufanyiwa upembuzi yakinifu, ili kufahamu sababu zinazopelekea baadhi ya watu wa Nicaragua kuwa na chuki dhidi ya Kanisa. Kardinali Leopoldo José Brenes anawaalika watu wa Mungu nchini Nicaragua kuwa macho na makini; waendelee kuwa watulivu na wavumilifu pamoja na kufuata maagizo yatakayotolewa na Jimbo kuu la Managua nchini Nicaragua. Kwa ufupi waamini waendelee kuonesha ukimya katika sala; wajikite katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na Njia ya Msalaba, ili kuomba toba na wongofu wa ndani. Wamkimbilie Bikira Maria, Msaada wa Wakristo na Malkia wa amani, ili kuombea amani, utulivu na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Nicaragua.

Salam za upendo na mshikamano zinaendelea kububujika kutoka sehemu mbali mbali za dunia, baada ya kusikia na kuona jinsi ambavyo Msalaba huo, ambao ni alama ya ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya dhambi na kifo, ulivyoharibiwa kwa moto! Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako mwaka 1996 alitembelea na kusali kwenye Kikanisa cha Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo. Mtakatifu Yohane Paulo II akawakumbusha watu wa Mungu nchini Nicaragua kwamba, Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kiini cha imani, faraja na upendo wa Mungu kwa waja wake. Katika hali ya uchovu, upweke hasi au hata kutoeleweka na wengine, Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, iwe ni chemchemi ya faraja na matumaini na kwamba, ushindi wake ni nguzo ya matumaini ya ushindi kwa wafuasi wake. Wachunguzi wa masuala ya uhuru wa kidini wanasema, Nicaragua inapitia kipindi kigumu na tete sana katika historia ya maisha na uwepo wake!

Papa: Nicaragua

 

 

03 August 2020, 13:13