Tafuta

Vatican News
Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Agosti 2020: Utume wa Bahari. Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Agosti 2020: Utume wa Bahari. 

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Agosti 2020: Wafanyakazi Baharini!

Papa Francisko kwa kuguswa na: fursa, matatizo na changamoto za maisha ya mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, anapenda kuelekeza Nia zake kwa Mwezi Agosti 2020 kwa Ajili ya Wafanyakazi Baharini. Watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia wanahimizwa na Mama Kanisa kuwaombea mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao bila kuwasahau watu wa kujitolea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika Utume wa Bahari, kwa Mama Kanisa kusoma alama za nyakati na kuendelea kujibu kilio cha mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na utume wao baharini! Pamoja na mambo mengine, Utume wa Bahari umeendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, mabaharia na wavuvi ambao wanajisadaka usiku na mchana ili kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, wanapata pia fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku. Takwimu zinaonesha kwamba, Utume wa Bahari unatekeleza dhamana na wajibu wake katika bandari 261 zilizoko katika nchi 55 na wanahudumiwa na Mapadre zaidi ya 200 bila kuwasahau watu wa kujitolea.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na: fursa, matatizo na changamoto za maisha ya mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, anapenda kuelekeza Nia zake kwa Mwezi Agosti 2020 kwa Ajili ya Wafanyakazi Baharini. Watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia wanahimizwa na Mama Kanisa kusali na kuwaombea mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao bila kuwasahau watu wa kujitolea. Hawa ni watu wanaonyonywa; wanaofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi; wanakabiliwa na dhuluma pamoja na nyanyaso mbali mbali. Takwimu zinaonesha kwamba, kati ya mwaka 2011 hadi mwaka 2020 zaidi ya mabaharia na wavuvi 745 wamefariki dunia na watu zaidi 9, 000 wamejeruhiwa. Mabaharia wengi wamejikuta wakiwekwa kizuini kwenye bandari mbali mbali duniani. Hili ni kundi la watu linalofanya kazi kubwa za suluba!

Katika miezi ya hivi karibuni, maisha na kazi za mabaharia pamoja na wavuvi zimebadilika sana, kwa sababu wanapaswa kuendelea kujisadaka zaidi bila ya kujibakiza. Kutokana na hofu ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19, mabaharia wengi walizuiliwa kwenye meli zao, hali ambayo imepelekea mabaharia wengi kuanza kusumbuliwa na afya ya akili, uchovu pamoja na kupunguza uwezo wao wa kufanya kazi. Hali ya mabaharia kuendelea kufanya kazi katika mazingira haya magumu na hatarishi ni hatari sana kwa mabaharia weyewe, hali ambayo pia inahatarisha usalama wa vyombo vyao baharini. Baadhi yao wamediriki hata kujinyonga kwa kutoona tena maana ya maisha. Wengi wao bado wanaendelea na matibabu ya muda mrefu, kwa sababu walicheleweshwa kupata huduma ya afya.

Kuna baadhi ya makampuni na wamiliki wa meli hizi wametumia mwanya wa janga la Virusi vya Corona, COVID-19 kukwepa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kushindwa kuwalipa mshahara, kuwahakikishia ulinzi na usalama wa maisha yao pamoja na mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka 2020 kumekuwepo na ongezeko la asilimia 24% ya matukio ya mashambulizi ya kiharamia, ikilinganishwa na mwaka 2019. Maharamia wameendelea kuwa ni tishio kwa usalama na maisha ya mabaharia na wavuvi. Katika hali na mazingira kama haya,  kazi ya mabaharia na wavuvi inahesababika kuwa ni kati ya kazi za hatari sana duniani. Hii inatokana na ukweli kwamba, hawa ni watu ambao maisha yao daima yako hatarini kutokana na kupata kipato “kiduchu” kiasi hata cha kushindwa kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wa kuzitegemeza familia zao kwa hali na mali.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa mabaharia pamoja na familia zao anasema, Jumuiya ya Kimataifa inapitia kipindi kigumu katika historia yake kutokana na janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Maisha na kazi ya mabaharia pamoja na wavuvi imeonesha umuhimu wake wa pekee katika kipindi hiki, kwa sababu wamesaidia sana kutoa chakula pamoja na mahitaji msingi kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza na kuwashukuru kwa sadaka na majitoleo yao. Anatambua fika hatari za maisha wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Katika miezi ya hivi karibuni, maisha na kazi za mabaharia pamoja na wavuvi zimebadilika sana, kwa sababu wanapaswa kuendelea kujisadaka zaidi bila ya kujibakiza. Wametumia muda mrefu zaidi wakiwa kwenye vyombo vyao bila ya kuruhusia kutua nanga kwa hofu ya kusambaza maambukizi mapya ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Wameendelea kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kutengwa na ndugu, jamaa, marafiki na hata nchi zao wenyewe. Matatizo na changamoto zote hizi si rahisi sana kwa wao kuweza kuzibeba na hasa katika kipindi hiki! Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia kwamba, wasidhani wako pweke na kwamba, wamesahauliwa. Kwa njia ya maisha na utume wao baharini unaweza kuwajengea mazingira kwamba, wako pweke, lakini watambue kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawahifadhi na kuwaombea kila wakati kutoka katika undani wa moyo wake. Sala hii inasindikizwa pia na wahudumu wa maisha ya kiroho pamoja na watu wa kujitolea wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwenye Utume wa Bahari, maarufu kama “Stella Maris” yaani “Nyota ya Bahari”. Injili Takatifu inawakumbusha waamini kwamba, Mitume wa kwanza wa Kristo Yesu, walikuwa ni wavuvi. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii, kuwapatia ujumbe; sala ya matumaini na faraja mintarafu matatizo na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao.

Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari ambayo kilele chake, kilipaswa kuwa ni mwezi Oktoba 2020, ungekuwa ni muda muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waliosadaka maisha yao bila ya kujibakiza kwa ajili Utume wa Bahari katika kipindi chote hiki. Ni muda wa kuwashukuru hata mabaharia na wavuvi wanaoendelea kuchakarika usiku na mchana pamoja na familia zao kwa sadaka kubwa na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu duniani! Lengo ni kuweza kuwasaidia mabaharia na wavuvi kutua nanga ya: imani, matumaini na mapendo katika maisha yao. Utume wa Bahari umejiaminisha katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya Bahari. Hii iwe pia ni fursa ya kukuza na kuendelea kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Nyota ya Bahari, inayopata amana na utajiri wake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Papa: Nia Mwezi Agosti 2020

 

 

11 August 2020, 13:01