Tafuta

Ziara ya Kitume nchini Ireland kwenye Mkutano wa IX wa Familia Ulimwenguni jijini Dublin tarehe 25 Agosti 2018 Ziara ya Kitume nchini Ireland kwenye Mkutano wa IX wa Familia Ulimwenguni jijini Dublin tarehe 25 Agosti 2018 

Ni miaka 2 tangu Papa Francisko afanye Hija ya Kitume nchini Ireland!

Tarehe 25 /26 Agosti 2018 Papa Francisko alifanya ziara yake nchini Ireland katika maadhimisho ya siku ya Familia ulimwenguni iliyofanyika katika mji wa Dublin kuanzia tarehe 21-26 Agosti.Familia bado ni kitovu cha maisha ya mwanadamu hadi miisho ya ulimwengu.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Tarehe 25 Agosti ni siku ya kukumbuka mwaka wa Pili tangu Papa Francisko alipofanya ziara yake nchini Ireland katika fursa ya Siku ya Familia Ulimwenguni iliyofunguliwa kunako tarehe 21 hadi 26 Agosti 2018  jiji Dublin. Alikwenda huko kushiriki na kukumbatia familia nyingi kutoka ulimwenguni zilizojumuika katika jiji la Dublin ili   kusheherekea pamoja siku hiyo ambayo ilikuwa ni sababu ya ziara ya 24 kimataifa kwa wakati huo. Haikuwa ni mara ya kwanza kwa Papa Francisko kukunyaga katika  mji huo wenye historia nzuri ya kikristo kwa maana aliwahi kuwa mjini humo mwaka 1980 wakati ana anajifunza lugha ya kiingereza. Katika siku mbili za kukaa nchini humo Papa alitoa hotuba sita na miongoni mwake ni pamoja na mahubiri, tafakari na sala ya Malaika wa Bwana na mazungumzo na vijana wa ndoa na wachumba  katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria, baadaye kukaa kidogo na kusali kwa ajili ya kumbu kumbu ya waathirika wa manyanyaso.

Furaha ya watu wawili ni nusu ya furaha na kuchukuliana uchungu na mateso

Papa Francisko akiwapongeza katika mkutano huo kwenye Kanisa la Mtakatifu Maria alibanisha ni kwa jinsi gani katika miaka mingi ndani ya Kanisa hilo, kumeadhimishwa sakramenti nyingi za ndoa. Na akiwatazama vijana kwa wingi wao alijiuliza kuwa si kweli kwamba vijana hawataki kuoa na kuolewa. Aliwashukuru kwa sababu ya kuoana na kushirikishana maisha na kwamba ni jambo jema. Alikumbusha msemo wa kisipanyola usemao “kuchukuliana uchungu watu wawili ni nusu ya uchungu, furaha ya watu wa wawili ni nusu ya furaha hiyo” na kwa maana  hiyo ndiyo njia ya ndoa” alisisitiza. Bado kumbu kumbu ni hai ya kumwona Papa Francisko mbele ya masalia ya Mtumishi wa Mungu  Matt Tabot  katika Kanisa hilo kuu na ambaye katika maisha yake alipitia uzoefu wa ulevi.

Neema ya kutafakari Yesu katika uso wa maskini

Papa Francsiko katika hotuba yake ya kwanza aliyoitoa katika nyumba ya kifalme jijini Dublin  kwa wana diplomasia na viongozi mbali mbali wa serikali aliwashukuru Rais kwa ukarimu wao  kueleza sababu ya kufika kwake ili kukutana na familia katika mji huo na kwamba Kanisa kiukweli ni familia ya familia na inahisi ulazima wakujumuika pamoja na kufanya sikukuu ya upendo ndani ya familia ya binadamu. Papa alitembelea pia kwenye kituo cha mapokezi cha Mapadre Wakapuchini wanaokaribisha familia za wasio na makazi na ambao wanapata pia msaada wa chakula. Akiwapongeza mafrateli wakapuchini aliwambia kuwa, wao wana maelewano ya aina ya pekee na watu wa Mungu zaidi maskini.  Wao wanayo neema ya kutafakari majeraha ya Yesu katika watu ambao wanahitaji na wanateseka, hawana furaha au hawana chochote au wamejazwa na majanga mengi. Kwa upande wao ni mwili ya Kristo. Na ndiyo ushuhuda wao na Kanisa linahitaji ushuhuda huo.

Kutembelea Madabahu ya Kitaifa ya Mama Maria wa Knock

Papa Francisko aidha  alikutana kwa faragha na wajesuit wa Ireland katika ubalozi na baadaye kufika katika Uwanja wa Kroke mahali ambapo waliandaa Tamasha la Siku kuu ya familia.  Siku kuu hiyo iloongozwa na vipindi vya sala, na ushuhuda mbali mbali kutoka katika familia tofauti zilizoandaliwa katika tukio hili. Haitasahaulika siku ya tarehe 26 Agosti 2018, Asubuhi alipokwenda kwenye madhabahu ya kitaifa ya Mama Maria wa Knock. Na kutembelea Kikanisa kidogo, na hapo alibaki katika sala mbele ya sanamu ya Bikira Maria na saa sita alisali sala ya Malaika wa Bwana. Alirudi jijini Dublin na kuadhimisha Misa Takatifu katika Uwanja mkubwa Phoenix kabla ya kurudi Roma.

Injili ya familia:furaha kwa ulimwengu na sala 

Ikumbukwe Kauli mbiu ya Siku hiyo ya IX ya familia duniani ilikuwa ni “Injili ya familia: furaha kwa Ulimwengu. Na kwa maana hiyo tafakari ilikuwa juu ya mafundisho ya Wosia Kitume wa Papa Francisko kuhusu  Furaha ya upendo ndani ya familia  ( Amoris laetitia) ambapo mama Kanisa anataka familia itembee daima katika hija ya ndani kwa udhihirisho halisi la maisha ya upendo. Vile vile ikumbukwe kuwa mara baada ya tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tamasha la siku ya Familia duniani, kwenye  Uwanja wa Croke mjini Dublin  Jumamosi 25 Agosti 2018, ilifuatia  sala iliyotungwa kwa ajili ya fursa hiyo ambayo inasema:

“Mungu Baba yetu, sisi ni ndugu kaka na dada katika Yesu Mwana wa Mungu wa familia moja, katika Roho ya upendo wako. Utubariki sisi sote kwa furaha ya upendo, ili tufanywe tuwe wavumilivu na wema, wenye upendo na ukarimu, wanaokaribisha walio na mahitaji. Tusaide tuishi msamaha wako na amani yako. Utulinde familia zote kwa jina lako, hasa wale ambao sasa wanasali kwako. Tuongezee imani, tutie nguvu ya matumaini ili tudumishe upendo wako na kutambua daima kushukuru zawadi ya maisha ambayo tunashirikishana. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amen.

Maria mama na kiongozi wetu, utuombee.

Mtakatifu Yosefu, baba na msimamizi wetu, utuombee.”

25 August 2020, 08:01