Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Jumuiya ya Mtakatifu Raymond Nonnato, Jimbo kuu la Buenos Aires nchini Nigeria: Kimbilio la sala na ibada kwa Mtakatifu huyu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Jumuiya ya Mtakatifu Raymond Nonnato, Jimbo kuu la Buenos Aires nchini Nigeria: Kimbilio la sala na ibada kwa Mtakatifu huyu. 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Jumuiya ya Mt. Raymond Nonnato, Argentina.

Papa amemwandikia ujumbe Padre Rubèn Ceraci, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Raymond Nonnatus, iliyoko Jimbo kuu la Buenos Aires, nchini Argentina. Baba Mtakatifu anawakumbuka wanawake wajawazito waliokuwa wanamwomba baraka kwa ajili ya watoto wao ambao bado walikuwa hawajazaliwa, daima aliwaelekeza kukimbilia ulinzi wa Mtakatifu Raymond Nonnatus. Inalipa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Raymond Nonnatus alizaliwa kunako mwaka 1204, huko Portell- Segarra, Catalonia nchini Hispania. Anaitwa Nonnatus kwa sababu, alitolewa hai tumboni mwa maiti ya mama yake. Mwanzoni, baba yake alimruhusu kwenda shule ili ajipatie ujuzi, elimu na maarifa, lakini ghafla, “akaamua kupindua meza” na kumpeleka mashambani mwake. Alitumia muda huu wa upweke chanya kama fursa ya kusali na kutafakari kuhusu kweli za imani na hivyo akafanikiwa kukuza Ibada kwa Bikira Maria. Kutoka katika undani wa maisha yake, akajisikia kuwa na wito wa kuwa mtawa na akajiunga na Shirika la Watawa wa Bikira Maria wa Mercede, lililokuwa na karama ya kuwakomboa watu kutoka kwenye biashara ya utumwa, wakawafundisha Neno la Mungu na kuwaweka huru, kwa kuthamini utu, heshima na haki zao msingi kama binadamu.

Baada ya malezi na majiundo yake ya kikasisi, kunako mwaka 1222 Mtakatifu Raymond Nonnatus akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alikita sehemu kubwa ya maisha yake katika mchakato wa kuwakomboa watumwa, kutoka kwa wafanyabiashara waliowageuza na kuwafanya kama bidhaa ya kuuzwa na kununuliwa sokoni. Katika maisha, wito na utume huu, alikumbana na mkono wa chuma, kiasi hata cha kujiweka rehani ili kuwakomboa watumwa, hadi pale fedha hiyo ilipolipwa na Shirika lake. Akiwa nchini Algeria alipata fursa ya kuwatembelea, kuwafariji na kuwaongoa watu katika Ukristo. Ushuhuda na utume wake, ulimjengea uadui mkubwa na wafanyabiashara ya binadamu. Akiwa njiani kurudi mjini Barcelona, Hispania mwaka 1239, Papa Gregory IX akamtangaza kuwa Kardinali kutokana na imani na ushuhuda wake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mtakatifu Raymond Nonnatus akafariki dunia tarehe 31 Agosti 1240, akalala usingizi wa amani katika Kristo Yesu. Kunako mwaka 1657, Papa Alexander VII akamtangaza kuwa Mtakatifu.

Ni katika muktadha wa maandalizi ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Raymond Nonnatus, hapo tarehe 31 Agosti 2020, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe wa matashi mema kwa mkono wake mwenyewe, Padre Rubèn Ceraci, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Raymond Nonnatus, iliyoko Jimbo kuu la Buenos Aires, nchini Argentina. Baba Mtakatifu anawakumbuka wanawake wajawazito waliokuwa wanamwomba baraka kwa ajili ya watoto wao ambao bado walikuwa hawajazaliwa, daima aliwaelekeza kukimbilia ulinzi na tunza ya Mtakatifu Raymond Nonnatus. Kama wao ni wananchi wa Argentina, alikuwa anawashauri kwenda kutembelea na kusali kwenye Madhabahu yaliyoko Cervantes, ili kuomba msaada kutoka kwa Mtakatifu Raymond Nonnatus. Baba Mtakatifu amewaandikia ujumbe wanaparokia hawa, ambao tarehe 22 Agosti 2020 wameanza novena ya sala, hata kama wanapaswa kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ataweza kuwakirimia neema, baraka, afya bora na uzao. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Raymond Nonnatus ni “Pamoja na Mtakatifu Raymond tukumbatie matumaini”. Kardinali Mario Polli wa Jimbo kuu la Buenos Aires ndiye anayeongoza novena hii kwa watu wa Mungu Jimboni mwake!

Mt. Raymond
22 August 2020, 14:20