Mtakatifu Bernardo Clairvaux, Mwalimu wa Kanisa alikuwa na Ibada sana kwa Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka, mfano bora wa kuigwa kwa kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Mtakatifu Bernardo Clairvaux, Mwalimu wa Kanisa alikuwa na Ibada sana kwa Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka, mfano bora wa kuigwa kwa kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. 

Mtakatifu Bernard Clairvaux na Ibada kwa Bikira Maria Mfariji!

Mtakatifu Bernardo wa Clairvaux, Mwalimu wa Kanisa, alitangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Alexander III, kunako mwaka 1174. Papa Pio wa VIII kunako mwaka 1830 akamtangaza kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Papa Francisko anawaalika waamini kuiga mfano wa maisha na utume wake; kwa kujiaminisha na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mfariji wa wale wote wanaoteseka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe 20 Agosti, Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Mtakatifu Bernardo wa Clairvaux, Mwalimu wa Kanisa aliyeishi kati ya Mwaka 1090 na kufariki dunia tarehe 20 Agosti 1153. Alitangazwa kuwa Mtakatifu  na Papa Alexander III, kunako mwaka 1174. Papa Pio wa VIII kunako mwaka 1830 akamtangaza kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Ni msimamizi pia wa wakulima. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuiga mfano wa maisha na utume wake; kwa kujiaminisha na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mfariji wa wale wote wanaoteseka!

Mtakatifu Bernardo, Mwalimu wa Kanisa alisisitiza kwamba Kristo Yesu tu ni “asali kinywani, wimbo sikioni, shangilio moyoni…Lishe yote ya maisha ya kiroho ni kavu na chakavu isipolainishwa na mafuta hayo; haina ladha isipotiwa chumvi hiyo. Unachoandika hakininogei nisiposoma Yesu ndani yake.” Ndiyo sababu mapokeo yamemwita “Doctor Mellifluus”, yaani “Mwalimu mtamu kama asali”, kwa jinsi masifu yake kwa Kristo Yesu yalivyobubujika kwa utamu kama asali kutoka mwambani. Pamoja na Kristo Yesu, Mtakatifu Bernardo alimmiminia sifa Bikira Maria, kiasi kwamba miaka 150 hivi baada ya kifo chake, Dante Alighieri alimtia mdomoni maneno haya: “Bikira Mama, binti wa Mwanao, mnyenyekevu na mkuu kuliko viumbe vyote, shabaha maalumu ya mpango wa milele”. 

Mtakatifu Bernardo hakuwa na shaka: ni kwa njia ya Bikira Maria kwamba, watu wanamwendea Kristo Yesu, akanogesha maneno haya kwa lugha ya Kilatini kwa kusema: “Per Mariam ad Iesum”). Ndiyo sababu alihimiza, “Katika hatari, katika huzuni, katika shaka, umfikirie Bikira Maria.  Yeye asiache kamwe kuwa midomo yako, asibandukane kamwe na moyo wako; na ili uweze kupata msaada wa sala zake, usisahau kamwe mfano wa maisha yake. Ukimfuata, huwezi kusita; ukimwomba, huwezi kukata tamaa; ukimfikiria, huwezi kukosea. Bikira Maria akikutegemeza, hutajikwaa; akikulinda, huna la kuogopa; akikuongoza, hutaanguka kamwe; akiwa upande wako, utafikia lengo lako”.

Kulingana na Mapokeo ya Kanisa, Mtakatifu Bernardo alishuhudia kwamba Bikira Maria yuko chini ya Kristo, lakini pia alisisitiza nafasi ya pekee aliyonayo Bikira Maria katika mpango wa wokovu, kutokana na jinsi alivyoshiriki kikamilifu sadaka ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, hata akadiriki kusimama chini ya Msalaba na kuona Mwanaye wa pekee, akiinamisha kichwa na kukata roho! Alipenda kusema hivi wakati wa mahubiri yake “Mama mwenye heri, kweli upanga ulichoma roho yako! Ukali wa uchungu ulichoma roho yako kwa ndani hivi kwamba, ni haki tukuite mfiadini, kwa sababu ndani mwako ushiriki wa mateso ya Mwanao unazidi kabisa kwa ukali mateso ya kimwili ya kufia dini.”

Mtakatifu Bernardo

 

19 August 2020, 13:59